Apr 17, 2020 20:11 UTC
  • Jumamosi, 18 Aprili, 2020

Leo ni Jumamosi tarehe 24 Shaaban mwaka 1441 Hijria mwafaka na tarehe 18 Aprili mwaka 2020 Miladia.

Siku kama leo miaka 129 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, aliaga dunia Mirza Muhammad Hassan Shirazi, mmoja wa wanazuoni na mamar'ja' mashuhuri wa Kiislamu. Alizaliwa katika mji wa Shiraz wa kusini mwa Iran na baada ya kuhitimu masomo yake ya msingi alielekea katika mji mtakatifu wa Najaf nchini Iraq kuendeleza masomo yake ya kidini ambako alisomo kwa wanazuoni mashuhuri wa mji huo kama Sheikh Murtadha Ansari. Bidii yake kwenye masomo ilimuwezesha kukwea haraka daraja za elimu na kuwa mhadhiri na mwanazuoni wa ngazi za juu katika ulimwengu wa Kiislamu. Jina la Mirza Shirazi ni mashuhuri mno kutokana na fatuwa yake ya kuharamisha tumbaku katika kipindi cha utawala wa Nasiruddin Shah kutoka ukoo wa Qajaar. Fatuwa hiyo ya kuharamisha tumbaku na matumizi ya sigara, bidhaa ambayo ilikuwa ikihodhiwa na Uingereza, ilitoa pigo kubwa kwa ukoloni wa Uingereza nchini Iran. Fatuwa hiyo ilitambuliwa kuwa mapambano ya moja kwa moja dhidi ya utawala wa Shah na ukoloni wa Uingereza nchini Iran na iliandaa uwanja wa mapambano ya baadaye ya wananchi wa Iran dhidi ya dhulma na ukoloni hapa nchini. ***

Mirza Muhammad Hassan Shirazi,

 

Miaka 66 iliyopita katika siku kama ya leo, Gamal Abdel Nasser alifanya mapinduzi dhidi ya Muhammad Nagib na kuwa Rais wa nchi hiyo. Gamal Abdel Nasser ndiye aliyeitafisha na kuitangaza kuwa mali ya taifa Kanali ya Suez na alikuwa na nafasi muhimu katika juhudi za kukabiliana na ubeberu katika ulimwengu wa Kiarabu na barani Afrika.  Aidha Rais huyo wa zamani wa Misri alikuwa na nafasi muhimu katika kuasisiwa Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote NAM. ***

Gamal Abdel Nasser

 

Katika siku kama ya leo miaka 66 iliyopita, mkutano wa kwanza wa wawakilishi wa nchi za Asia na Afrika uliojulikana kwa jina la Mkutano wa Bandung ulifanyika katika mji wenye jina hilo nchini Indonesia. Mkutano huo uliowashirikisha wajumbe kutoka zaidi ya nchi 29 za Asia na Afrika, ulikuwa na lengo la kujenga umoja wa nchi hizo za ulimwengu wa tatu katika kukabiliana na kambi kubwa mbili duniani za Mashariki na Magharibi. Mkutano wa Bandung ndio ulioandaa mazingira ya kuundwa Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote (NAM).  ***

Mkutano wa Bandung

 

Siku kama ya leo miaka 40 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 18 Aprili 1980, Zimbabwe ambayo wakati ule ilikuwa ikijulikana kwa jina la Rhodesia, ilipata uhuru. Zimbabwe ilikoloniwa na Uingereza mwishoni mwa karne ya 19. Mara baada ya Vita vya Pili vya Dunia na kufuatia kudhoofika Uingereza, zilianza harakati za wananchi za kupigania uhuru na hatimaye harakati hizo zilipelekea kuundwa makundi ya mapambano ya silaha. Zimbabwe ina ukubwa wa zaidi ya kilomita mraba 390,000 na inapakana na nchi za Msumbiji, Zambia, Botswana na Afrika Kusini. ***

Zimbabwe

 

Na miaka 24 iliyopita katika siku kama ya leo, yaani tarehe 18 Aprili 1996 , jeshi la anga la utawala wa Kizayuni wa Israel lilishambulia makao ya kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa katika kijiji cha Qana, kusini mwa Lebanon. Katika shambulizi hilo la kinyama la Wazayuni, takribani raia 110 wa Lebanon waliuawa shahidi wakiwemo wanawake na watoto. Licha ya hayo, Marekani ilizuia kupasishwa katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa azimio la kulaani mauaji ya kijiji cha Qana yaliyofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel. ***

Mauaji ya Qana