Apr 19, 2020 21:58 UTC
  • Jumatatu, Aprili 20, 2020

Leo ni Jumatatu tarehe 26 Shaabani 1441 Hijria inayosadifiana na Aprili 20 mwaka 2020.

Leo tarehe Mosi Ordibehesht katika kalenda ya mwaka wa Hijria Shamsia ni siku ya kumuenzi Sheikh Muslihuddeen Saadi Shirazi malenga, mshairi na mwalimu stadi wa tungo za mashairi na nathari wa Kifarsi. Saadi Shirazi alizaliwa karibu mwaka 606 Hijria Qamariya katika familia ya kielimu kwenye mji wa Shiraz ulioko kusini mwa Iran na baada ya kukipitisha kipindi cha utoto na kuinukia kwake katika mji alikozaliwa wa Shiraz nchini Iran, akiwa kijana Saadi Shirazi aliamua kwenda katika mji wa Baghdad huko Iraq. Akiwa huko alisoma katika shule ya Nidhamiya na baadaye kufanya safari katika maeneo ya Sham, Hijaz, Roma na katika maeneo mengine. Katika safari zake hizo, malenga huyo mashuhuri alifanikiwa kufahamiana na jamii mbalimbali na kuona mengi yaliyoimarisha kipawa chake cha kutunga mashairi. Saadi Shirazi ni miongoni mwa malenga na washairi wakubwa katika ulimwengu wa Kiislamu. Saadi Shirazi ameandika vitabu kadhaa, muhimu zaidi ni kile cha tungo cha Bustan na kitabu chake cha nathari cha Golestan.

Sheikh Muslihuddeen Saadi Shirazi

Siku kama ya leo miaka 1336 iliyopita, alifariki dunia, Yazid bin Abdul-Malik bin Marwan, khalifa dhalimu wa wakati huo. Yazid bin Abdul-Malik aliingia madarakani baada ya kufariki dunia Omar bin Abdul-Aziz hapo mwaka 101 Hijiria. Kiongozi huyo mbali na kufanya dhulma na ukandamizaji, hakuzingatia pia masuala ya Waislamu. Kwa kuzingatia kuwa alikuwa ni mtu wa karibu na ukoo wa Hajjaj Thaqafi, hivyo aliwapa umuhimu mkubwa watu wa ukoo huo.

Siku kama ya leo miaka 686 iliyopita, alifariki dunia Ibn Faswiih, aliyekuwa faqihi, malenga na mtaalamu wa lugha ya Kiarabu, huko mjini Damascus, Syria. Baada ya kusoma elimu ya sheria za Kiislamu na lugha ya Kiarabu, alianza kujifundisha pia elimu ya hadithi na kufikia ujuzi wa hali ya juu katika uwanja huo. Aidha msomi huyo mbali na elimu za dini, alisoma pia mashairi huku akiandika vitabu mbalimbali kuhusu maudhui tofauti ikiwemo fiqhi.

Siku kama ya leo tarehe 20 Aprili miaka 218 iliyopita Mawahabi wa Hijaz (Saudi Arabia) walishambulia mji mtakatifu wa Karbala nchini Iraq na kuua mamia ya Waislamu wa madhehebu ya Shia. Baada ya mawahabi kushika hatamu za uongozi huko Hijaz mwanzoni mwa karne ya 19 walianzisha mashambulizi ya mara kwa mara ya kundi hilo lenye misimamo na fikra za kuchupa mipaka dhidi ya Waislamu wengine hususan wafuasi wa Watu wa Nyumba ya Mtume wetu Muhammad (saw) na miongoni mwa mashambulizi ya mawahabi hao ni yale ya kushambulia miji mitakatifu ya Karbala na Najaf nchini Iraq tarehe 20 Aprili mwaka 1802. Miji hiyo ambayo ni mitakatifu hususan kwa Waislamu wa madhehebu ya Shia kutokana na kuwa na makaburi ya watu wa kizazi cha Mtume wetu Muhammad (saw) imekuwa ikilengwa na mawahabi. Katika mashambulizi hayo mawahabi walishambulia haram ya mjukuu wa Mtume, Imam Hussein bin Ali mwana wa Bibi Fatima (as) huko Karbala na kuvunja quba na kaburi na mtukufu huyo na kisha wakapora mali iliyokuwa hapo. Waislamu zaidi ya elfu mbili waliuawa katika shambulizi hilo la mawahabi. Mashambulizi hayo yaliwakasirisha sana Waislamu katika maeneo mbalimbali ya dunia na kuzidisha chuki yao dhidi ya mawahabi na mafundisho ya kundi hilo potofu. Mawahabi walidumisha mauaji ya Waislamu wa madhehebu ya Shia na madhehebu nyinginezo baada ya kuanzishwa dola la watawala  wa kizazi cha Aal Saud huko Saudi Arabia na walishambulia na kuharibu Haram ya wajukuu wa Mtume Muhammad (saw) na za masahaba zake wakubwa katika makaburi ya Baqii mjini Madina. 

Karbala

Katika siku kama hii ya leo miaka 40 iliyopita aliaga dunia Sohrab Sepehri malenga na mchoraji mashuhuri wa Kiirani. Sohrab alizaliwa mwaka 1307 Hijria Shamsiya katika mji wa Kashan katikati mwa Iran. Awali malenga huyo wa Kiirani alianza kufundisha na baada ya hapo alijiunga na taaluma ya sanaa. Vilevile alikuwa na kipaji kikubwa katika masuala ya uchoraji. Kazi za malenga na mchoraji huyo wa Kiirani zilimpatia tuzo na zawadi nyingi katika maonyesho mbalimbali yaliyofanyika ndani na nje ya Iran. Shairi lake la kwanza alilitunga mwaka 1330 Hijria Shamsiya na kulipa jina la The Death of Colours.

Sohrab Sepehri

Miaka 21 iliyopita 20 Aprili 1999, kulitokea maafa makubwa ya shambulizi lililofanywa na wanafunzi wawili wa Kimarekani kwenye shule moja ya sekondari. Wanafunzi hao waliwamiminia risasi na kuwaua wanafunzi wenzao 12 na mwalimu wao na kuwajeruhi wengine 21. Wanafunzi hao waliovamia shule ya Columbine High School iliyoko Denver, jimbo la Colorado, walijiua wenyewe baada ya kufanya mauaji hayo. Mauaji kama hayo ya kutisha yamekuwa yakitokea mara kwa mara katika maeneo ya umma nchini Marekani. Wataalamu wanasema uhuru wa kununua na kumiliki silaha ni miongoni mwa sababu za maafa hayo yanayotokea kila mwaka nchini Marekani.

Columbine High School iliyoko Denver, jimbo la Colorado

Katika siku kama ya leo miaka 20 iliyopita sawa na 26 Shaaban mwaka 1421 Hijria Qamaria, aliaga dunia faqihi na mwanazuoni mkubwa Ayatullah Sayyid Mahdi Rouhani. Ayatullah Rouhani alizaliwa mwaka 1343 Hijria Qamaria sawa na 1303 Hijria Shamsia katika mji mtakatifu wa Qum. Katika ujana wake alijifunza dini na alipofika umri wa miaka 20 alielekea katika mji wa Najaf al Ashraf nchini Iraq. Baadaye wakati Ayatullah Boroujerdi alipowasili Qum, Ayatullah Rouhani alishiriki katika darsa zake za fiqhi na fiqhi na kisha yeye mwenyewe akaanza kufunza darsa hizo. Ayatullah Rouhani alikuwa mwanazuoni wa kwanza katika Chuo Cha Kidini cha Qum (Hawzah) ambaye alianzisha vikao vya kitaalamu kwa lengo la kuchunguza itikadi ya Umaxi. Baada ya kuanza harakati ya Kiislamu nchini Iran chini ya uongozi wa Imam Khomeini MA, alijiunga na harakati hiyo kubwa na kunufaika na fursa iliyokuwa imejitokeza ya kueneza itikadi za Kislamu. Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu mwaka 1979, alichaguliwa kuwa mwakilishi wa watu wa mikoa ya Markazi na Qum katika Baraza la Wanazuoni wanaomchagua Kiongozi Muadhamu. Mwanazuoni huyo bingwa aliaga dunia tarehe 26 Shaaban mwaka 1421 Hijria Qamaria sawa na 3 Azar mwaka 1379 Hijria Shamsia akiwa na umri wa miaka 76 na alizikwa katika Haram takatifu ya Bibi Maasouma mjini Qum. 

Ayatullah Sayyid Mahdi Rouhani. Ayatullah Rouhani

Na miaka 10 iliyopita katika siku kama ya hii ya leo, mlipuko uliotokea kwenye mtambo wa kuchimba mafuta wa Deepwater Horizon na kuzamisha mtambo huo mali ya Shirika la Mafuta la Uingereza (British Petroleum) kulikosababisha kuvuja mafuta katika Ghuba ya Mexico. Wafanyakazi 11 wa mtambo huo waliuawa na mafuta mengi yaliyokuwa yakivuja kutoka katika kisima hicho yalisababisha uchafuzi mkubwa wa mazingira kuwahi kutokea katika karne moja ya hivi karibuni huko Marekani.

Deepwater Horizon