Apr 21, 2020 03:01 UTC
  • Jumanne tarehe 21 Aprili mwaka 2020

Leo ni Jumanne tarehe 27 Shaabani 1441 Hijria sawa na Aprili 21 mwaka 2020.

Siku kama ya leo miaka 1191 iliyopita, Egbert Mfalme wa Kwanza wa Uingereza alichukua madaraka baada ya vita vya muda mrefu. Kabla ya hapo Uingereza ilikuwa ikiongozwa na wafalme wa kiukoo huku ikiwa imegawika katika sehemu kadhaa za kijiografia na kila mtawala akitawala eneo lake maalumu. Egbert aliyekuwa mfalme wa Wessex, eneo lililokuwa Kusini mwa Uingereza ya sasa, baada ya kupambana na watawala wa kitabaka na kuwashinda, mwaka 829 alifanikiwa kuingia madarakani akiwa Mfalme wa Kwanza wa Uingereza na kuasisi silsila ya utawala wa Wasaxoni wa Magharibi.

Egbert

Siku kama ya leo miaka 175 iliyopita aliuawa Sayyid Ali Muhammad Shirazi aliyekuwa mashuhuri kwa lakabu ya “Bab” ambaye alidai kuwa ndiye Imam Mahdi (AF) na baadaye akadai kuwa ni Mtume. Alizaliwa mwaka 1235 Hijria Qamariya katika mji wa Shiraz nchini Iran na alionekana kuwa na itikadi potofu akiwa bado shuleni. Muhammad Ali Bab ambaye hakuwa na elimu ya juu alifuatwa na watu majahili na kuungwa mkono na wakoloni. Baada ya kudai kuwa ndiye Imam wa mwisho katika kizazi cha Mtume Muhammad (saw) yaani Imam Mahdi (AF), Bab alikwenda mbali zaidi na kudai kuwa ni Mtume wa Mwenyezi Mungu na kwamba dini ya Uislamu imefutwa. Wanazuoni wa zama hizo walifichua urongo wake na kuchukulia hatua. Hata hivyo aliendelea kulingania itikadi zake potofu na katika siku kama ya leo Amir Kabiir aliyekuwa kiongozi wa zama za Qajar alitoa amri ya kunyongwa kwake.

Siku kama ya leo miaka 82 iliyopita, alifariki dunia Allamah Muhammad Iqbal Lahore mwanafikra, mwanafalsafa na malenga wa Kiislamu. Allamah Iqbal alizaliwa mnamo mwaka 1877 katika moja ya miji ya Punjab na baada ya kumaliza masomo yake ya awali na kupata shahada ya uzamili alielekea nchini Ujerumani na baadaye Uingereza kwa lengo la kujiendeleza katika elimu ya falsafa na kubaki huko kwa kipindi cha miaka minne. Malenga huyo alianza kutunga mashairi akiwa katika masomo yake ya Sekondari. Baada ya msomi huyo mkubwa kurejea nchini India, alianza kuwaamsha Waislamu wa nchi hiyo na kufanya jitihada za kuwaunganisha pamoja huku akibainisha fikra na mitazamo yake kupitia beti za mashairi.

Muhammad Iqbal Lahore

Siku kama ya leo miaka 41 iliyopita Imam Khomeini (M.A) mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alitoa amri ya kuundwa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (SEPAH). Kwa mujibu wa amri hiyo, jukumu kuu la jeshi hilo ni kulinda Mapinduzi ya Kiislamu dhidi ya maadui wa ndani na nje. Baada ya kuundwa, jeshi la SEPAH lilikabiliana na makundi yaliyopinga Mapinduzi ya Kiislamu, yaliyoanzisha mapambano ya silaha katika pembe mbalimbali za Iran na kuweza kuzima njama za maadui. Aidha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi liliweza kudhihirisha uwezo mkubwa wakati wa vita vya kulazimishwa kati ya Iraq na Iran vilivyoanzishwa na utawala wa dikteta Saddam Hussein kwa lengo la kuyaangamiza Mapinduzi ya Kiislamu na kuigawa Iran.