Apr 23, 2020 21:55 UTC
  • Ijumaa, Aprili 24, 2020

Leo ni Ijumaa tarehe 30 Shaabani 1441 Hijria inayosadifiana na tarehe 24 Apili mwaka 2020 milaadia.

Siku kama ya leo miaka 1468 iliyopita kwa mujibu wa mahesabu ya wanahistoria wengi, iliasisiwa kwa mara ya kwanza taasisi ya kuandika na kutarjumu vitabu duniani hapa nchini Iran. Uamuzi huo ulichukuliwa na Khosrow Anushirvan, mfalme wa Sasani nchini hapa. Taasisi hiyo ilijengwa sambamba na maktaba na vilikamilishwa kujengwa mwaka huo huo. Vitabu tofauti vilikusanywa kutoka maeneo mbalimbali ya dunia kwa ajili ya kutarjumiwa na mfalme huyo alimtuma daktari wake kwenda nchini India kwa ajili ya kukusanya vitabu kwa ajili ya shughuli hiyo.

Maktaba ya Iran

Siku kama ya leo miaka 749 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 24 April mwaka 1271, mtalii Marco Polo wa Venice alianza safari ya kihistoria ya kutembelea bara Asia. Kabla yake baba na ami yake walitembelea China kupitia njia ya Asia Ndogo na Iran. Baada ya kurejea ndugu wa Polo kutoka Ulaya, Marco Polo akifuatana na baba yake kwa mara nyingine walielekea China na kutembelea ardhi ya nchi hiyo na visiwa vya kusini mshariki mwa Asia. Baada ya kurejea nchini kwake, Marco Polo aliandika kumbukumbu ya safari iliyoitwa "Maajabu" kuhusiana na hali ya kijiografia ya ardhi za China, Turkemanistan, Mongolia na sehemu za kusini mashariki mwa Asia. Safari ya Marco Polo barani Asia ilichukua karibu miaka 20.

Marco Polo

Katika siku kama ya leo miaka 104 iliyopita, sawa na tarehe 24 Aprili mwaka 1916 kulianza harakati ya tatu ya raia wa Ireland kwa ajili ya kujipatia uhuru wao kutoka kwa serikali ya Uingereza. Harakati hiyo ilienda sambamba na kujiri kwa vita vikali vya kidini baina ya Waprotestanti na Wakatoliki. Vita hivyo vilimalizika kwa kufikiwa makubaliano baina ya David Lloyd George, Waziri Mkuu wa wakati huo wa Uingereza na kiongozi wa harakati ya raia wa Ireland waliokuwa wanataka kujitenga hapo mwaka 1922 Miladia.

Bendera ya Ireland

Siku kama ya leo miaka 93 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 24 April mwaka 1927 chanjo ya B.C.G iligunduliwa. Chanjo hiyo iligunduliwa na madaktari wa kifaransa Albert Calmette na Guerin, baada ya kufanya uchunguzi wa miaka mingi. Chanjo ya B.C.G hutumika kukinga maambukizi ya ugonjwa wa kifua kikuu au TB. Kugunduliwa chanjo hiyo kumepunguza vifo vya watu wanaopatwa na ugonjwa wa TB duniani kote.

(B.C.G)

Siku kama ya leo miaka 40 iliyopita,  inayosadifiana na tarehe 5 Ordibehesht mwaka 1359 Hijiria Shamsia, Marekani ilishambulia kijeshi ardhi ya Iran kwa kutumia helikopta na ndege kadhaa za kivita. Serikali ya Marekani ilifanya mashambulizi hayo baada ya kushindwa njama zake mbalimbali za kutaka kuuangusha mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu wa Iran. Lengo la mashambulio hayo lilikuwa ni kutaka kuwakomboa majasusi wake waliotiwa mbaroni wakati wa kutekwa ubalozi wa Marekani hapa nchini uliokuwa pango la kijasusi. Licha ya kuweko mipango makini, kutumiwa vyombo vya kisasa kabisa na mazoezi mengi yaliyofanywa katika eneo linalofanana na hilo ili kuhakikisha operesheni hiyo inafanikiwa, lakini mashambulizi hayo yalikatishwa na tufani kubwa ya mchanga iliyotokea Tabas na kupelekea kuanguka baadhi ya ndege, kushika moto helikopta za Marekani na kufa baadhi ya askari wa nchi hiyo huku waliobakia wakiikimbia ardhi ya Iran. 

Tukio la Tabas