Jumamosi, 25 Aprili, 2020
Leo ni Jumamosi tarehe Mosi ya mwezi Mtukufu wa Ramadhani 1441 Hijria sawa na tarehe 25 Aprili 2020 Miladia.
Leo ni siku ya kwanza ya mwezi mtukufu wa Ramadhani kwa mujibu wa kalenda ya Hijria Qamaria; mwezi ambao ndani yake iliteremshwa Qurani Tukufu. Ni mwezi wa rehema na baraka za kiroho. Katika kubainisha utukufu wa mwezi huu, Mtume Mtukufu SAW amesema, siku za mwezi huu ndizo siku bora zaidi kuliko siku nyingine zote na kuwataka Waislamu wachume na wafaidike kutokana na fadhila na baraka za kiroho za mwezi huu. Allah SWT anasema: ((Hakika tumeiteremsha (Qurani) katika usiku wa heshima. Na nini kitakujulisha usiku huo wa heshima ni nini? Laylatul Qadr (usiku huo wa heshima) ni bora kuliko miezi elfu.)) Tukio la kuhuzinisha moyo la kuuawa shahidi Imam Ali AS na kuzaliwa Mjukuu wa Mtume SAW, Imam Hassan AS, ni katika matukio muhimu yaliyotimia katika mwezi huu. Tunamuomba Allah SW atupe baraka za kimaanawi za mwezi huu na kwa fadhila za mwezi huu mtukufu tuwe karibu na rehema na msahamaha Wake. ***
Aidha katika siku ya kwanza ya mwezi mtukufu wa Ramadhani, kiliteremshwa kitabu cha Suhf cha Nabii Ibrahim AS. Jina Ibrahim limetajwa mara 69 katika Qur'ani Tukufu kwa heshima na taadhima ambapo maisha yake yameashiriwa kwa njia mbali mbali kama ibra na ruwaza njema kwa waumini. Mwenyezi Mungu amemtaja kuwa ni mtu mwenye kumuabdudu Mungu mmoja na dini imetajwa kuwa ya Hanifa katika aya ya 67 ya Sura Aal Imran na pia katika aya ya 125 ya Sura An Nisaa. Alikuwa Nabii mkweli kama tunavyosoma katika Surat Maryam aya ya 41. Aidha Mwenyezi Mungu alimpa yeye na familia yake neema na mamlaka kama tunavyosoma katika Surat An Nisaa aya ya 54. Kuna vitabu kadhaa vya mbinguni ambavyo waliteremshiwa Mitume kama vile Suhf cha Ibrahim AS na Nuh AS, Taurati ya Musa AS na Injili ya Issa AS na kitabu kilicho kamilika kati ya vyote hivyo ni Qur'ani Tukufu.***
Siku kama ya leo miaka 1013 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, iliyopita alifariki dunia Ibn Sina maarufu kwa jina la Sheikhur Rais, tabibu, mtaalamu wa hisabati, falsafa na mnajimu mkubwa wa Kiirani. Ibn Sina alifariki dunia katika mji wa Hamadan ulioko magharibi mwa Iran akiwa na umri wa miaka 58. Alihifadhi Qur'ani Tukufu akiwa kijana na akapata kusoma elimu za mantiki, uhandisi na utaalamu wa nyota. Baada ya kumtibu Nuh bin Mansur, mmoja wa Wafalme wa Kisamani akiwa kijana, Ibn Sina alipata idhini ya kutumia maktaba kubwa ya mfalme huyo. Katika maktaba hiyo, Ibn Sina alipata kusoma vitabu vingi vya elimu tofauti. Abu Ali Sina alitokea kuwa msomi, mwandishi na mtafiti mashuhuri. Miongoni mwa athari muhimu za msomi huyu mkubwa ni pamoja na kitabu cha "Shifaa" kinachohusu elimu ya falsafa, "Qanun" kinachohusu tiba na "Daneshnameh Allai".***
Katika siku kama ya leo miaka 709 iliyopita, alizaliwa Ibn Khaldun, mtaalamu wa masuala ya kijamii, mwanasiasa na mwanahistoria Mwislamu. Ibn Khaldun alizaliwa huko Tunisia. Maisha ya Ibn Khaldun yanaweza kugawanywa katika sehemu tatu ambapo maisha yake ya awali aliyatumia katika kusoma elimu tofauti. Alitumia sehemu ya pili ya maisha yake katika siasa na kuhudumia nyadhifa tofauti za utendaji nchini ambapo kutokana na njama za maadui zake, alifungwa jela. Baada ya kuachiliwa huru Ibn Khaldun alijitenga na siasa. Hapo ndipo ilianza duru ya tatu ya maisha yake ambapo alijishughulisha na utafiti na uandishi. Alimu na msomi huyo alifariki dunia mwaka 808 Hijiria. ***
Katikka siku kama ya leo miaka 528 iliyopita, serikali ya mwisho ya Kiislamu barani Ulaya ilisambaratika huko Granada. Baada ya kudhihiri dini ya Uislamu na kupanua mamlaka yake katika maeneo ya Asia na kaskazini mwa Afrika, jeshi la Waislamu liliingia kusini magharibi mwa Ulaya kupitia lango bahari la Jabal Tariq (Gibraltar) na kulitawala eneo hilo kwa kipindi cha karne 8. Eneo hilo ambalo kwa sasa linaitwa Uhispania, wakati huo lilijulikana kwa jina la Andalusia. Katika kipindi cha ustawi wa ustaarabu wa Kiislamu eneo la Granada lilikuwa kituo kikuu cha ustaarabu huo na makao makuu ya kueneza Uislamu hususan barani Ulaya. Dola la Kiislamu la Andalusia liliangushwa kupitia njia ya kueneza ufuska na maovu baina ya watawala na makhalifa wa wakati huo. ***
Miaka 122 iliyopita katika siku kama ya leo, serikali ya Marekani ilitangaza vita dhidi ya Uhispania. Kabla ya hapo, Marekani ilikuwa imeitaka Uhispania ilipatie ufumbuzi suala la Cuba kupitia njia za amani. Baadhi ya Wacuba kwa miaka mingi walikuwa wakipigania mamlaka ya kujitawala na mara kadhaa walifanya majaribio ya mapinduzi na kuendesha mapigano ya silaha. Kulipuka manowari ya kijeshi ya Marekani ya Maine katika maji ya Cuba, kilikuwa kisingizio kizuri kwa Marekani cha kuingia katika vita dhidi ya Uhispania. Katika vita hivyo vilivyoanza tarehe 25 Aprili hadi Agosti 12 mwaka 1898 vilimalizika kwa kushindwa Uhispania; na kwa mujibu wa mkataba wa Paris ardhi za Ufilipino, Ouerto Rico, Guam na Cuba zipatiwa Marekani.***
Siku kama ya leo miaka 49 iliyopita, takribani Wamarekani laki mbili walifanya maandamano mjini Washington wakiendeleza upinzani wao dhidi ya mashambulizi ya nchi hiyo huko Vietnam. Maandamano hayo yalikuwa miongoni mwa vielelezo vikubwa vya upinzani wa wananchi wa Marekani dhidi ya siasa za kichokozi za serikali ya nchi hiyo huko Vietnam. Katika vita vya Vietnam vilivyoanza mwaka 1964 Marekani ilituma askari laki tano nchini humo ambako makumi ya maelfu miongoni mwao waliuawa na wengine wengi kujeruhiwa. Kwa sababu hiyo wananchi wa Marekani walizidisha upinzani dhidi ya vita hivyo na mwaka 1975 Marekani ililazimika kufunga virago na kuondoka Vietnam kutokana na mashinikizo ya ndani na ya kimataifa na kushindwa mara kwa mara jeshi la nchi hiyo katika medani za vita.***
Katika siku kama ya leo miaka 95 iliyopita, kwa mara ya kwanza kulianzishwa kituo cha redio nchini Iran na kurushwa matangazo ya moja kwa moja. Awali kituo cha redio kilikuwa chini ya usimamizi wa Wizara ya Posta, Simu na Telegrafu. Miaka mitano baada ya kuanzishwa kituo cha redio mjini Tehran, hatua kwa hatua huduma hiyo ilipanuliwa katika miji mbalimabali hapa nchini. Lakini baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu 1979, zilianzishwa redio na televisheni kadhaa, zikiwemo zile za matangazo ya ng'ambo, zinazotangaza kwa lugha mbalimbali za kigeni ikiwemo Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iliyoanzishwa mwaka 1994.***