Apr 26, 2020 06:11 UTC
  • Jumapili, tarehe 26 Aprili, 2020

Leo ni Jumapili tarehe Pili Ramadhani 1441 Hijria, inayosadifiana na tarehe 26 Aprili 2020 Milaadia.

Siku kama ya leo 1101 iliyopita, sawa na tarehe pili Ramadhani mwaka 340 Hijiria, alifariki dunia mjini Damascus, Syria Abdur-Rahman Zajaji Nahawandi, fasihi, mtaalamu wa lugha na mtaalamu wa sheria za Kiislamu wa karne ya nne Hijiria. Nahawandi alizaliwa kusini magharibi mwa Iran na akiwa kijana alielekea mjini Baghdad, Iraq na kupata kusoma elimu ya sheria za Kiislamu na lugha kwa wasomi wakubwa wa zama zake kama vile Ibn Durayd. Baada ya muda Abdur-Rahman Zajaji Nahawandi alitokea kuwa mwalimu katika uga huo. Mwaka 311 Hijiria alielekea Sham ambapo aliishi huko hadi mwishoni mwa uhai wake. Miongoni mwa athari za msomi huyo ni pamoja na kitabu cha ‘Aamal Zajaji’ ‘Al-Idhaahul-Kaafi’ na ‘Iidhahu fi Ilalin-Nahw.’ 

Siku kama ya leo miaka 415 iliyopita, sawa na tarehe 26 Aprili 1605 Miladia, lilichapishwa gazeti la kwanza kabisa duniani nchini Ufaransa. Mhariri Mkuu wa gazeti hilo lililopewa jina la Relation alikuwa Johann Carolus. Gazeti hilo liliendelea kuchapishwa kwa kipindi cha miaka 70. Hii leo maelfu ya magazeti huchapishwa kila siku katika pembe mbalimbali za dunia na Wajapani wanahesabiwa kuwa wasomaji wakubwa zaidi wa magazeti kuliko watu wa maeneo mengine ya dunia.

Gazeti la kwanza kuchapishwa duniani nchini Ufaransa

Siku kama ya leo miaka 87 iliyopita, Shirika la Kuogofya la Gestapo la  Ujerumani liliasisiwa. Shirika hilo liliasisiwa na Hermann Wilhelm Goering aliyekuwa mmoja wa maafisa wa juu wa Adolph Hitler kiongozi wa Wanazi wa Ujerumani. Shirika hilo lilikuwa polisi wa siri wa Kijerumani katika kipindi cha utawala wa Wanazi. Jukumu la German for Secret State Police, kama lilivyojulikana pia, lilikuwa ni kuwafuatilia, kuwatia mbaroni na kuwanyonga watu waliokuwa wakimpinga Hitler na siasa zake za Kinazi. Kiongozi mashuhuri kabisa wa Gestapo alijulikana kwa jina la Heinrich Himmler na alianza kuwaongoza polisi hao wa siri wa Kijerumani mwaka 1934.

Gestapo

Siku kama ya leo miaka 56 iliyopita, sawa na tarehe 26 Aprili 1964 Miladia, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliundwa baada ya nchi mbili za Tanganyika na Zanzibar kuungana. Kabla ya kuungana huko Tanganyika na Zanzibar zilikoloniwa na nchi mbalimbali ambapo nchi mkoloni wa mwisho ilikuwa Uingereza. Tanganyika ilipata uhuru mwaka 1961 na Zanzibar mwaka 1963 baada ya mapambano ya wananchi ya kupigania uhuru dhidi ya mkoloni Muingereza. Julius Kambarage Nyerere alitoa wito wa kuungana Tanganyika na Zanzibar na ilipofika tarehe 26 mwezi Aprili mwaka 1964 nchi mbili hizo ziliungana na kuunda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.Tanzania iko mashariki mwa Afrika na katika pwani ya Bahari ya Hindi huku ikipakana na Kenya, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Uganda, Rwanda, Burundi, Zambia, Malawi na Msumbiji.

Bendera ya Tanzania

Siku kama ya leo miaka 35 iliyopita, sawa na tarehe 26 Aprili 1985, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilitoa azimio likilaani hatua ya Iraq ya kutumia silaha za kemikali. Baada ya utawala wa zamani wa Iraq kushambulia kwa mabomu ya kemikali makazi ya raia nchini Iran na kufuatia mashtaka yaliyowasilishwa na Iran, ujumbe wa Umoja wa Mataifa ulitumwa katika nchi mbili hizi kutoa ripoti mbili ambazo zilieleza kuwa, utawala huo ulitumia mara kadhaa silaha za kemikali dhidi ya majeshi na raia wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Hii ilikuwa mara ya kwanza kwa Umoja wa Mataifa kukiri waziwazi kwamba, jeshi la Iraq lilitumia silaha za kemikali dhidi ya Iran. Katika kipindi chote cha vita vya miaka 8 vilivyoanzishwa na Iraq dhidi ya Iran, utawala wa Saddam uliua shahidi maelfu ya wanajeshi na raia wa Iran kutokana na kutumia silaha za gesi yenye kemikali. Kwa sababu hiyo Iran inatambuliwa kuwa mhanga mkubwa zaidi wa silaha za kemikali duniani baada ya Vita vya Pili vya Dunia.

Silaha za kemikali

Siku kama ya leo miaka 34 iliyopita, sawa na tarehe 26 Aprili 1986, kituo cha nguvu za nyuklia cha Chernobyl huko Ukraine ambacho kilikuwa kikidhamini sehemu kubwa ya nishati ya umeme ya nchi hiyo kiliripuka na kusambaza mada hatari za miale ya radioactive (nunurishi). Awali Russia ilikadhibisha habari ya kutokea mlipuko katika kituo hicho. Hata hivyo baadaye ililazimika kukiri kutokea mlipuko katika kituo hicho cha nguvu za nyuklia cha Chernobyl baada ya wingu kubwa la nyuklia lililosababishwa na mada za radioactive kuonekana waziwazi katika kituo hicho. Kasoro za kiufundi zilitajwa kuwa chanzo cha mlipuko huo. Katika tukio hilo, makumi ya maelfu ya watu waliathirika kwa namna tofauti kukiwemo kuongezeka maradhi mbalimbali. Mwaka 2000 Ukraine ilikifunga kabisa kituo hicho cha nyuklia cha Chernobyl.

Kituo cha nguvu za nyuklia cha Chernobyl huko Ukraine

Na siku kama ya leo miaka 24 iliyopita, sawa na tarehe 26 Aprili 1996, mashambulizi ya kijeshi ya siku 16 ya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Lebanon kwa jina la "Vishada vya Hasira" yalimalizika. Katika operesheni hiyo jeshi la utawala wa Israel lilifanya mashambulio ya nchi kavu, anga na baharini huko kusini na hata katika ya mji mkuu wa Lebanon, Beirut. Mbali na kuharibu maeneo mengi ya raia na miundo mbinu na taasisi za kiuchumi, utawala haramu wa Israel uliwaua shahidi raia 180 wa Lebanon na kujeruhi mamia ya wengine. Inafaa kuashiria kuwa, operesheni za "Vishada vya Hasira" zilianzishwa na utawala huo katili kwa lengo la kudhoofisha moyo wa wananchi na wanamuqawama wa Kiisamu wa nchini Lebanon na kuwatwisha masharti ya Tel Aviv ya kutoondoka kusini mwa nchi hiyo ya Kiarabu. Hata hivyo Walebanon waliendelea kusisitizia kuondoka haraka na bila ya masharti yoyote utawala huo bandia kusini mwa nchi hiyo kwa msingi wa azimio nambari 424 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Sisitizo hilo pamoja na mapambano ya muqawama wa Lebanon ya mwaka 2000 hatimaye yaliulazimu utawala huo haramu wa Kizayuni kuondoka kusini mwa Lebanon; na hiyo ikawa ni mara ya kwanza kwa utawala huo kurudi nyuma kutokana na muqawama wa wananchi, tangu utawala huo ulipoundwa katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu.