Apr 28, 2020 20:17 UTC
  • Jumatano tarehe 29 Aprili 2020

Leo ni Jumatano tarehe 5 Ramadhani 1441 Hijria sawa na Aprili 29 mwaka 2020.

Tarehe 10 Ordebehesht kwa mujibu wa kalenda ya Kiirani sawa na tarehe 30 Aprili, inafahamika kuwa siku ya kitaifa ya Ghuba ya Uajemi. Siku hii iliitwa siku ya kitaifa ya Ghuba ya Uajemi kutokana na baadhi ya pande zenye chuki dhidi ya Iran, kufanya njama za kutaka kupotosha historia, kwa kuiita kwa majina mengine yasiyo na msingi Ghuba ya Uajemi. Jina la kihistoria la Ghuba ya Uajemi limetafsiriwa katika lugha mbalimbali kwa jina hilo au kwa jina la Bahari ya Pars. Inafaa kuashiria hapa kuwa, Ghuba ya Uajemi ni ya tatu kwa ukubwa duniani baada ya Ghuba ya Mexico na Ghuba ya Hudson. Kutokana na kuwa na vyanzo vingi vya utajiri yakiwemo mafuta na gesi, Ghuba ya Uajemi na pwani yake inahesabika kimataifa kuwa sehemu yenye umuhimu mkubwa na wa kistratijia. Kwa kuzingatia utambulisho wa kiutamaduni na kihistoria wa taifa la Iran, Baraza Kuu la Mapinduzi ya Utamaduni la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, liliitangaza siku ya leo ambayo inakumbusha tukio la kuwaondoa Wareno kutoka lango la Hormuz, kuwa siku ya kitaifa ya Ghuba ya Uajemi.

Ghuba ya Uajemi

Miaka 338 iliyopita, Peter the Great alichukua madaraka ya nchi huko Russia akiwa na umri wa miaka 10. Peter alikuwa ndugu wa Feodor katika kizazi cha tatu cha Tzar katika ukoo wa Romanov. Baada ya kuchukua madaraka Peter alivuliwa uongozi na dada yake na kubaidishwa katika kijiji kimoja karibu na mji wa Moscow. Baada ya muda Peter aliandaa jeshi kubwa na kwenda kupambana na dada yake. Katika vita hivyo Peter alishinda na kutawala nchi hiyo kwa mara nyingine. Kadhalika Peter alifanya marekebisho makubwa ndani ya Russia. Peter the Great alifariki dunia mwaka 1725. 

Peter the Great

Siku kama ya leo miaka 166 iliyopita, alizaliwa Henri Poincaré, mtaalamu wa sayansi na hisabati wa Ufaransa katika mji wa Nancy nchini humo. Poincare alikuwa mahiri katika somo la hisabati na alianza kufanya utafiti katika uwanja huo. Chunguzi mbalimbali zilizofanywa na mwanahisabati huyo wa Kifaransa kuhusiana na masuala ya uchanganuzi wa kimahesabu, mwangaza, umeme n.k zimetajwa kuwa muhimu na sahihi. 

Henri Poincaré

Katika siku kama ya leo miaka 92 iliyopita,  sawa na tarehe 29 mwezi Aprili mwaka 1928 Miladia, nchini Uturuki herufi za Kilatini zilitambuliwa rasmi na kuchukua nafasi ya zile za Kiarabu. Hatua hiyo ilichukuliwa katika njama za kuipiga vita dini ya Kiislamu na badala yake kuingizwa tamaduni za Kimagharibi katika jamii ya wananchi Waislamu wa Uturuki. Mchakato huo ulianzishwa na Mustafa Kamal maarufu kama Ataturk kuanzia mwaka 1923. Mfumo wa Jamhuri ulishika hatamu za uongozi huko Uturuki chini ya Ataturk kuanzia mwezi Oktoba mwaka 1923 baada ya kuanguka kwa utawala wa Othmania uliodumu kwa miaka 623 nchini humo. 

Kamal Ataturk

Miaka 75 iliyopita katika siku kama ya leo, majeshi ya waitifaki yalipata pigo kubwa mwishoni mwa Vita vya Pili vya Dunia. Vikosi vya nchi waitifaki wa Ulaya vilifanya shambulizi la pamoja dhidi ya Italia baada ya kusambaratishwa safu ya ulinzi ya Ujerumani. Italia ilikuwa muitifaki wa Ujerumani chini ya uongozi wa Benito Musolini. 

Hitler baada ya kuchapo katika vita vya dunia

Siku kama ya leo miaka 69 iliyopita, alifariki dunia Ludwig Wittgenstein, mwanafalsafa mashuhuri wa Austria. Alizaliwa mwaka 1889 Miladia mjini Vienna, mji mkuu wa nchi hiyo na baada ya kuhitimu masomo ya msingi aliendelea na masomo nchini Uingereza katika fani ya uhandisi. Kukutana kwake na Bertrand Russell, mwanafalsafa mkubwa wa Uingereza kulimvutia sana Ludwig Wittgenstein na kumfanya ajiunge na fani hiyo. Baada ya kusoma kitabu cha Russell alidai kwamba masuala yote ya falsafa yametatuliwa, hata hivyo baada ya miaka kadhaa alitambua kosa lake na mwaka 1929 alifikia daraja ya PHD katika falsafa na kufanikiwa kuwa mhadhiri katika chuo kikuu cha Cambridge. Ameacha athari kadhaa katika fani hiyo na moja ya athari hizo ni kitabu cha 'Tafiti za Kifalsafa'. 

Ludwig Wittgenstein

Tarehe 10 Ordibehesht miaka 41 iliyopita Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilikata uhusiano wake na Misri. Amri ya kukatwa uhusiano wa Jamhuri ya Kiislamu na Misri ilitolewa na hayati Imam Ruhullah Khomeini baada ya Rais wa wakati huo wa Misri, Anwar Saadat kutia saini makubaliano ya aibu na fedheha ya Camp David na utawala wa Kizayuni wa Israel na kusaliti malengo ya Wapalestina. Kutiwa saini makubaliano hayo ilikuwa hatua ya kuhalalisha uvamizi wa Wazayuni dhidi ya Palestina na kusaliti haki za Wapalestina waliokuwa wakipambana na utawala haramu wa Israel na vilevile kupuuza maslahi ya Umma wa Kiislamu. Baadaye kiongozi huyo wa Misri alitiwa adabu na shujaa, Khalid Islambuli aliyemmiminia risasi na kumuua kutokana na usaliti huo.

Anwar Sadat