Jumamosi, Pili Mei, 2020
Leo ni Jumamosi tarehe 8 ya mwezi mtukufu wa Ramadhani 1441 Hijria, ambayo inasadifiana na tarehe Pili Mei, 2020.
Siku kama ya leo miaka 766 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, alifariki dunia Najmud-Din Ali Dabirani, maarufu kwa jina la Katibi, tabibu na mtaalamu mkubwa wa elimu ya nyota wa Iran. Awali hakuwa na maarifa yoyote katika uwanja huo. Hata hivyo baada ya Khoja Nasruddin Tusi, mwanafalsafa, mwanahisabati, mnajimu na mwanazuoni mkubwa wa Kiirani kumtaka Katibi amsaidie kujenga kituo kikubwa cha kielimu na akademia ya kwanza ya sayansi yaani mahala pa kuangalilia mwenendo wa nyota, mwezi na jua iliyojulikana kwa jina la Maraghe huko kaskazini magharibi mwa Iran, ndipo msomi huyo naye akainukia kielimu sambamba na kufanya kazi katika kituo hicho. Kuna athari nyingi kutoka kwa Najmud-Din Ali Dabirani (Katibi) na miongoni mwazo ni pamoja ni kitabu kinachoitwa 'Jaamiud-Daqaaiq' na 'Hikmatul-Ain.' ***

Katika siku kama ya leo, alifariki dunia mchoraji na msanifu majengo maarufu wa Italia Leonardo da Vinci. Alizaliwa mwaka 1452 na umahiri wake ulidhihiri haraka katika nyanja mbalimbali za sanaa. Baada ya kufanya safari katika miji kadhaa ya Italia, mwaka 1506 Da Vinci alielekea Ufaransa na kuwa mchoraji wa Mfalme Louis xii. Aliishi katika kipindi cha mchoraji mwingine mashuhuri wa Italia Michelangelo na wasanii hao wawili mashuhuri walitoa mchango mkubwa katika sanaa na kipindi cha mwamko wa Ulaya (Renaissance). Miongoni mwa michoro maarufu ya Leonardo Da Vinci ni The "Last Supper" na "Mona Lisa". Mbali na uchoraji, Leonardo Da Vinci alikuwa amebobea pia katika taaluma nyingine kama hisabati. ***
Miaka 407 iliyopita katika siku kama ya leo, kipindi cha utawala wa Kitsar wa ukoo wa Romanov kilianza huko nchini Russia. Miaka mitatu baada ya mashambulio ya Poland dhidi ya Russia, mmoja wa makamanda wa Kirusi aliibuka mshindi na kuukomboa mji wa Moscow kutoka katika uvamizi wa jeshi la Poland na Mikhail Romanov akachaguliwa kuwa mtawala mpya wa Kitsar. Kwa hatua hiyo, kipindi cha miaka 304 cha utawala wa familia ya Romanov kikawa kimeanza huko Russia. Katika zama za utawala wa ukoo wa Romanov, nchi ya Russia ilipanuka mno, lakini kwa upande wa kiuchumi haikupiga hatua ya kuzingatiwa na udiketa na ukandamizaji wa Waromanov ulizuia wananchi wa Russia kushiriki katika kuainisha mustakabali wao.***
Katika siku kama ya leo miaka 213 iliyopita, hati ya makubaliano yaliyojulikana kama Treaty of Finckenstein ilitiwa saini baina ya Iran na Ufaransa. Kwa mujibu wa mkataba huo, Ufaransa iliahidi kuisaidia Iran kurejesha ardhi zake zilizokuwachini ya wavamizi wa Georgia na wavamizi wengine kwa kuitumia silaha na wataalamu wa kijeshi. Mkabala na msaada huo, Iran nayo iliahidi ingekata uhusiano wake wote wa kisiasa na kibiashara na Uingereza na kutangaza vita dhidi ya nchi hiyo na kwamba, itakuwa muitifaki wa Ufaransa katika vita vya nchi hiyo dhidi ya Uingereza na Russia.
Na katika siku kama ya leo, miaka 166 iliyopita, Mirza Habibullah Shirazi, mashuhuri kwa jina la Qaani mshairi mashuhuri wa Kiirani aliaga dunia. Alizaliwa mwaka 1187 Hijria Shamsia huko Shirazi kusini mwa Iran. Mirza Habibullah Shirazi alifanya safari Mash’had kwa ajili ya kujiendeleza kielimu na kuanza kujishughulisha na utunzi wa mashairi. Baada ya miaka kumi Qaani alifanikiwa kubobea katika elimu za nawh, bayan, nujumu, teolojia, falsafa na mashairi. Alikuwa mshairi wa kwanza Muirani aliyekuwa akiifahamu lugha ya Kifaransa. Mbali na Kiafaransa, Mirza Habibullah Shirazi alikuwa akizifahamu vizuri pia lugha za Kiarabu na Kiingereza. ***