May 03, 2020 03:20 UTC
  • Jumapili, tarehe 3 Mei, 2020

Leo ni Jumapili tarehe 9 Ramadhan 1441 Hijria, inayosadifiana na tarehe 3 Mei 2020 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 591 iliyopita, Jeanne d'Arc alianzisha harakati ya kihistoria ya kuzikomboa baadhi ya ardhi za Ufaransa zilizokuwa zikikaliwa kwa mabavu na Uingereza. Jeanne d'Arc alikuwa kamanda wa jeshi ambaye alipewa jukumu na Mfalme wa Ufaransa la kuongoza mapambano dhidi ya majeshi ya Uingereza yaliyolikalia kwa mabavu eneo la kaskazini mwa Ufaransa. Hatimaye Kamanda huyo alikamatwa na kufunguliwa mashtaka ya kimaonyesho nchini Uingereza kwa tuhuma za kuritadi na kuacha dini na mwaka 1431, aliuawa kwa kuchomwa moto akiwa hai.

Jeanne d'Arc

Siku kama ya leo miaka 551 iliyopita alizaliwa Niccolò di Bernardo dei Machiavelli, mwanahistoria na mwanasiasa wa Italia katika mji wa Florence. Sambamba na shughuli zake za kisiasa, Machiavelli aliandika pia kuhusu historia ya Florence. Katika mtazamo wa kisiasa, Machiavelli alikuwa akiamini kwamba inawezekana kutumia wenzo wowote ule kwa ajili ya kupata madaraka na kwa ajili ya kuyalinda, na kwamba hakuna udharura wowote wa kuheshimiwa misingi ya maadili katika masuala kama hayo. Miongoni mwa kazi za mwanahistoria na mwanasiasa huyo wa Italia ni "The Art of War" na "The Prince."

Niccolò di Bernardo dei Machiavelli

Siku kama ya leo miaka 526 iliyopita, sawa na tarehe 3 Mei 1494 Miladia, Christopher Columbus, baharia wa Uhispania aligundua nchi ya Jamaica, huko Amerika ya Kati katika safari yake ya pili ya uvumbuzi ndani ya bara la Amerika. Licha ya tabia ya upendo na maridhiano ya wakazi asilia wa Jamaica na nchi nyingine zilizogunduliwa, lakini Christopher Columbus na watu wengine waliotumwa na Uhispania, waliwafanyia ukatili wenyeji hao wakazi. Kwa utaratibu huo Jamaica ambayo kutokana na nafasi yake muhimu ya kijografia na kwa kuwa na dhahabu nyingi zilizokuwa zikikodolewa macho na Uhispania, ilikoloniwa kuanzia mwaka 1509 Miladia hadi muda unaokaribia karne mbili. Baada ya Uhispiania nchi hiyo pia ilikoloniwa na Uingereza ambapo katika kipindi hicho akthari ya wakazi wake asilia walifukuzwa au kuuawa. Hatimaye nchi hiyo iliweza kujipatia uhuru wake mwaka 1962 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 505 iliyopita yaani tarehe 3 Mei 1515 Miladia, manowari za Ureno zilianza kushambulia kisiwa cha Hormoz cha Iran na hivyo kuanzisha wimbi la uingiliaji na ukoloni wa nchi za Magharibi katika eneo la Mashariki ya Kati. Kisiwa hicho kiko katika eneo la kiistratijia la lango la Hormoz lililoko katika Ghuba ya Uajemi na Bahari ya Oman, kusini mwa Iran. Kutokana na kuwa Iran ilikuwa dhaifu katika upande wa jeshi la majini wakati huo, wakoloni wa Kireno walivikalia kwa mabavu visiwa kadhaa vya Iran vilivyoko katika Ghuba ya Uajemi, kikiwemo cha Bahrain ambacho wakati huo kilikuwa sehemu ya ardhi ya Iran. Hatua kwa hatua, Iran iliimarisha jeshi lake la majini, na ilipofika mwaka 1652, iliweza kuvikomboa visiwa vyote vilivyokuwa vikikaliwa kwa mabavu na Wareno.

Eneo la Lango Bahari la Hormoz

Siku kama ya leo miaka 116 iliyopita, alifariki dunia Ayatullah Sheikh Muhammad Bahari Hamadani. Ayatullah Bahari Hamadani alikuwa mmoja wa maulama wakubwa na mtaalamu mashuhuri wa elimu ya Irfan wa karne ya 13 na 14 Hijiria nchini Iran. Baada ya kuhitimu masomo yake ya awali, Ayatullah Sheikh Muhammad Bahari Hamadani alielekea mjini Najaf, Iraq na baada ya kukamilisha masomo yake alijishughulisha na kazi ya uwalimu. Miongoni mwa athari zake ni pamoja na kitabu kinachoitwa 'Tadhkiratul-Muttaqiina.'

Ayatullah Sheikh Muhammad Bahari Hamadani.

Siku kama ya leo miaka 173 iliyopita, yaani sawa na tarehe Tatu Mei 1847, alizaliwa Alexander Graham Bell mbunifu wa simu nchini Marekani. Bell alikuwa na shauku kubwa ya kuwa fundi na mhandisi tokea zama za ujana wake. Baada ya kufanya utafiti na uchunguzi kwa muda wa miaka 10, hatimaye alifanikiwa kutengeneza chombo chenye uwezo wa kuhamisha sauti, ambacho kinafanana na simu zinazotumika leo hii. Hali kadhalika mtaalamu huyo wa Kimarekani alifanikiwa kutengeneza chombo kinachonasa sauti au phonograph. Alezander Graham Bell alifariki dunia mwaka 1922.

Alexander Graham Bell