Jumatano, tarehe 6 Mei, 2020
Leo ni Jumatano tarehe 12 Ramadhani 1441 Hijria sawa na tarehe 6 Mei mwaka 2020.
Siku kama ya leo miaka 1440 iliyopita yaani tarehe 12 Ramadhani mwaka wa Kwanza Hijria, muda mfupi baada ya Mtume Mtukufu Muhammad (SAW) kuhamia Madina akitokea Makka, aliunga udugu baina ya Muhajirina na Ansar. Muhajirina ni watu ambao walihama na Mtume (SAW) kutoka Makka kwenda Madina na Ansar ni Waislamu wa mjini Madina waliowakaribisha na kuwanusuru Muhajirina katika mji huo. Kwenye sherehe hiyo ya kuunga udugu wa Waislamu, Mtume (SAW) alimtangaza Ali bin Abi Talib (AS) kuwa ndugu yake hapa duniani na Akhera.
Siku kama ya leo yaani mwezi 12 Ramadhani kwa mujibu wa baadhi ya nukuu za historia ni siku ambayo Nabii Issa Ibn Maryam AS aliteremshiwa kitabu kitukufu cha Injili. Neno Injili ni la Kigiriki na lina maana ya bishara. Jina hilo limetajwa mara 12 katika Qur’ani Tukufu na kitabu hicho kinaitambua Injili kuwa ni kitabu cha Mwenyezi Mungu SW chenye sheria na kanuni za mbinginu. Hata hivyo kitabu kinachojulikana hivi sasa kwa jina la Injili si kile kilichoteremshwa kwa Nabii Issa Masih bali ni riwaya na kumbukumbu zilizokusanywa na wanafunzi wake baada ya Yeye kupaa mbinguni.
Tarehe 12 Ramadhani miaka 844 iliyopita, alifariki dunia Ibn Jawzi, faqihi na mtaalamu mkubwa wa hadithi katika karne ya 6 Hijria. Ibn Jawzi alizaliwa mwaka 510 Hijria na kufanya safari nyingi kwa ajili ya masomo. Mbali na kubobea katika masuala ya elimu ya fiq'hi na hadithi, alikuwa mtaalamu katika uwanja wa kutoa mawaidha na hata akaweza kuaminiwa na maulamaa wakubwa wa zama zake. Mwanazuoni huyo ameandika vitabu vingi na mashuhuri zaidi ni Al Muntadhim na Mawaidhul Muluk.
Siku kama ya leo miaka 161 iliyopita alifariki dunia mtaalamu wa masuala ya kimaumbile na msomi mkubwa wa Kijerumani Alexander Humboldt. Alizaliwa mwaka 1769 huko Berlin, Ujerumani. Alifanya safari ndefu katika mabara ya Asia na Amerika kwa ajili ya kufanya utafiti. Tafiti nyingi za msomi huyo zilihusu namna dunia ilivyoumbwa.
Siku kama ya leo miaka 138 iliyopita yaani tarehe 6 Mei 1882, ilitangazwa habari ya mafanikio ya kugunduliwa vijidudu maradhi vya ugonjwa wa kifua kikuu na Robert Koch. Wiki mbili kabla ya hapo, mtaalamu huyo wa masuala ya baiolojia alikuwa amegundua vijidudu maradhi hivyo ambavyo vilikuwa vimeua zaidi ya watu bilioni moja katika kipindi chote cha historia. Baadaye Prof. Robert Koch aligundua njia ya kufubaza na kutenga vijidudu maradhi hivyo ambavyo vilikuwa sugu mkabala wa dawa na vilikuwa na uwezo wa kujificha mwilini kwa miaka mingi na kisha kujitokeza baadaye. Mbali na kugundua vijidudu maradhi vya kifua kikuu, Prof. Robert Koch pia aligundua vijidudu maradhi vya kipindupindu katika safari zake katika nchi za Misri na India na mwaka 1906 alitengeneza dawa ya Atoxy inayoshabihiana na Quinine. Prof. Robert Koch anatambuliwa kuwa mtaalamu mkubwa zaidi wa vijidudu maradhi duniani baada ya Luis Pastore na alitoa huduma kubwa sana kwa elimu na sayansi ambayo kamwe haitasahaulika.
Katika siku kama ya leo miaka 98 iliyopita, alifariki dunia Ayatullah Sheikh Mahdi Khalisi, faqihi na mujtahidi mkubwa wa zama hizo. Ayatullah Khalisi alizaliwa huko Kadhimiya nchini Iraq mwaka 1277 Hijiria na akiwa kijana alijishughulisha na kuamrisha mema na kukataza maovu sambamba na kustahamili shida nyingi kipindi cha masomo na kutafuta elimu. Katika kipindi cha Vita vya Kwanza vya Dunia, msomi huyo akishirikiana na baadhi ya mujtahid wa Iraq, alianzisha mapambano dhidi ya uvamizi wa wakoloni Waingereza nchini humo. Baada ya muda alirejea nchini Iran na kujishughulisha na kazi ya ualimu na kufunza elimu za kidini. Miongoni mwa vitabu vya msomi huyo mkubwa ni Kifayatul Usuul na Anawinul Usul.