May 07, 2020 21:12 UTC
  • Ijumaa, tarehe 8 Mei, 2020

Leo ni Ijumaa tarehe 14 Ramadhani mwaka 1441 Hijria sawa na tarehe 8 Mei mwaka 2020.

Siku kama ya leo miaka 1374 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 14 Ramadhani mwaka 67 Hijria, aliuawa shahidi Mukhtar bin Abi Ubaida al Thaqafi, kiongozi wa harakati ya kulipiza kisasi cha damu ya Imam Hussein bin Ali AS, mjukuu wa Mtume Mtukufu Muhammad SAW. Imam Hussein AS akiwa pamoja na wafuasi wake na watu wa familia yake, aliuawa shahidi na wafuasi wa Yazid bin Muawiya, akilinda dini tukufu ya Kiislamu. Mukhtar alianzisha harakati zake katika mji wa Kufa. Kabla yake, kulijitokeza kundi la 'Tawwabiin' ambalo lilianzisha mapambano dhidi ya utawala wa Bani Umayya, kwa lengo la kulipiza kisasi cha damu ya Imam Hussein AS. Mukhtar al Thaqafi alitawala Kufa kwa muda wa mwaka mmoja hivi, na hatimaye alishindwa na jeshi la Mus'ab bin Zubair na kuuawa shahidi katika siku kama hii ya leo.

Kaburi la Mukhtar

Tarehe 8 Mei 1794 aliuawa Antoine Laurent - de Lavoisier mtafiti, mvumbuzi na msomi wa Kifaransa na mmoja kati ya waanzilishi wa elimu ya kemia ya kisasa, baada ya kuhukumiwa adhabu ya kifo kwa kukatwa kichwa kutokana na amri ya utawala wa Kifalme baada ya mapinduzi ya Ufaransa. Lavoisier aligundua elementi zinazounda hewa katika utafiti wake. Baada ya hapo, mkemia huyo wa Kifaransa aliweza kuvumbua gesi ya oksijeni. Lavoisier anafahamika kama 'Baba wa Kemia ya Kisasa.

Antoine Laurent - de Lavoisier

Siku kama ya leo miaka 203 iliyopita tatibu James Parkinson wa Uingereza aligundua ugonjwa wa Parkinson. Dalili kuu za ugonjwa huo ni zile zinazohusiana na kutetemeka sana kwa baadhi ya viungo vya mwili, kukaza misuli, mwendo wa pole yaani mtu hushindwa kutembea haraka pamoja na kupepesuka. Ugonjwa huo unasababishwa na baadhi ya matatizo ndani ya ubongo na hadi kufikia sasa tiba mujarabu ya maradhi hayo haijapatikana.

James Parkinson

Miaka 193 iliyopita tarehe 14 Ramadhani 1248 Hijria alifariki dunia Shamsuddin Behbahani aliyekuwa mwanafalsafa na msomi mashuhuri wa Kiislamu katika karne ya 13 Hijria. Behbahani alipata elimu kwa wanazuoni wakubwa wa zama hizo akiwemo Muhaqiq Behbahani. Alikuwa faqihi aliyebobea, alimu na arifu mkubwa na alipitisha kipindi kikubwa cha umri wake katika kufanya uhakiki na kuandika vitabu. Shamsuddin Behbahani ameandika sherhe ya kitabu cha "Maalimul Usul" na vitabu vingine vingi vya falsafa na teolojia.

Shamsuddin Behbahani

Siku kama ya leo miaka 118 iliyopita mwafaka na tarehe 8 Mei 1902, mji wa Saint-Pierre uliangamia baada ya kulipuka volkano kwenye mlima Pelee kusini mwa Ufaransa. Watu wasiopungua elfu 30 walipoteza maisha yao kwenye maafa hayo yaliyochukua muda wa dakika tatu tu.

Volkano ya Saint-Pierre

Siku kama ya leo miaka 75 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 8 Mei 1945, vilimalizika Vita vya Pili vya Dunia barani Ulaya baada ya Wanazi wa Ujerumani kusalimu amri bila ya masharti. Ujerumani ilianza kushindwa vita hivyo tokea mwaka 1943. Vita vya Pili vya Dunia vinahesabiwa kuwa vita vikubwa zaidi kutokea katika historia ya mwanadamu, kwani karibu watu milioni 55 waliuawa katika vita hivyo vilivyosababisha pia hasara kubwa.

Kumalizika kwa Vita vya Pili vya Dunia

Na tarehe 14 Ramadhani miaka 27 iliyopita Mzayuni mmoja aliyekuwa na misimamo ya kufurutu ada aliwashambulia na kuwamiminia risasi Waislamu waliokuwa wakitekeleza ibada ya Swala katika Msikiti wa Haram ya Nabii Ibrahim mjini al Khalil (Hebron), Palestina inayokaliwa kwa mabavu na kuua shahidi 29 miongoni mwao. Mauaji hayo, yaliyotekelezwa na mlowezi wa Kizayuni Baruch Goldstein aliyekuwa daktari katika jeshi la Israel, yalitokea wakati Waislamu hao walipokuwa katika ibada ya funga ya mwezi mtukufu wa Ramadhani. Waislamu wengine wengi walijeruhiwa katika shambulizi hilo la kikatili. Mauaji hayo ambayo yalidhihirisha tena uhasama na chuki za Wazayuni wa Israel dhidi ya Waislamu, yalilaaniwa na Waislamu kote duniani. Ukatili huo ulizusha wimbi kubwa la machafuko katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina ambapo wananchi walizidisha mapambano dhidi ya maghasibu wa Tel Aviv. Israel ilimshika kwa muda na kumuachia huru mhalifu huyo katili kwa kisingizio kwamba alikuwa punguani!

Jinai za Wazayuni dhidi ya raia wasio na ulinzi wa Palestina