May 10, 2020 08:23 UTC
  • Jumapili, tarehe 10 Mei, 2020

Leo ni Jumapili tarehe 16 Ramadhan 1441 Hijiria, sawa na tarehe 10 Mei 2020 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 714 iliyopita, yaani sawa na tarehe 16 Ramadhani mwaka 727 Hijria, alifariki dunia Ibn Zamlakani, faqihi na msomi wa Hadithi na Fasihi wa Kiislamu, aliyefahamika kama Dimishqi. Msomi huyo alipata kustafidi na elimu ya dini na hadithi kutoka kwa maulamaa wa zama hizo. Kutokana na kipaji chake cha elimu, msomi huyo aliruhusiwa kutoa fatwa akiwa na umri wa miaka 20, mbali na kufunza masomo mbalimbali ya kidini katika vyuo tofauti, na kuwa kadhi mjini Damascus nchini Syria. Miongoni mwa kazi za msomi huyo ambazo tunaweza kuziashiria hapa ni kitabu alichokipa jina la "Al Burhanul Kaashif Anil I'jaazil Qurani".

Ibn Zamlakani.

Siku kama ya leo miaka 596 iliyopita kwa mujibu wa baadhi ya riwaya yaani tarehe 16 Ramadhani mwaka 845 Hijria, alifariki dunia Taqiyud-Din Abul-Abbas Maqrizi, msomi na mwanahistoria mkubwa wa Kiislamu. Maqrizi alizaliwa mjini Cairo, Misri na baadaye aliekekea katika miji mikubwa ya Ulimwengu wa Kiislamu kwa ajili ya kupata elimu na maarifa zaidi ya Kiislamu. Kwa muda msomi huyo alijishughulisha na ukadhi huko Cairo. Alipendelea sana historia na kuandika vitabu tofauti katika uwanja huo. Miongoni mwa athari za Taqiyud-Din Abul-Abbas Maqrizi ni pamoja na kitabu cha 'as-Suluuk Lima'arifatil-Muluuk' ambacho kinazungumzia historia.

Taqiyud-Din Abul-Abbas Maqrizi.

Siku kama ya leo miaka 191 iliyopita sawa na tarehe 10 Mei 1829 Miladia, alizaliwa François-Marie Raoult, mwanakemia wa Ufaransa. Baada ya kuhitimu masomo yake katika hatua ya PHD katika Chuo Kikuu cha mjini Paris, alipanua wigo wa utafiti wake wa kielimu. Baada ya hapo alifanikiwa kuwa mmoja wa waasisi wapya wa elimu ya kemia na fizikia. François-Marie Raoult alifanikiwa pia kubuni nadharia zake katika uwanja huo.

François-Marie Raoult

Siku kama ya leo miaka 45 iliyopita, sawa na tarehe 10 Mei 1975, kundi linalopigania uhuru wa Sahara Magharibi liliasisi Harakati ya Kupigania Uhuru ya Polisario. Harakati hiyo ilikaribishwa na wakazi wa eneo hilo na ikaanzisha mapambano dhidi ya wakoloni wa Kihispania hadi wakoloni hao walipoondoka Sahara mwaka 1975. Hata hivyo serikali ya Uhispania ilikabidhi mamlaka ya eneo hilo kwa serikali za Morocco na Mauritania. Mauritania ililazimika kuondoka Sahara Magharibi kutokana na mapambano makali ya Polisario na hali mbaya ya ndani ya eneo hilo. Morocco iliendelea kukabiliana na wapigania uhuru wa Polisario hadi mwaka 1991 ambapo mapigano kati ya pande hizo mbili yalisitishwa chini ya upatanishi wa Umoja wa Mataifa. Eneo hilo lingali linakaliwa na Morocco. Ilikubaliwa kuwa mustakbali wa kisiasa wa eneo hilo uamuliwe kupitia kura ya maoni lakini hadi leo kura hiyo haijafanyika kutokana na sababu tofauti.

Harakati ya Kupigania Uhuru ya Polisario