Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu (10)
Assalaam Aalaykum wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo na karibuni katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu ambacho huwatambulisha na kuwazungumzia Maulamaa wakubwa wa Kishia, mchango wao katika Uislamu pamoja na vitabu na athari zao.
Kipindi chetu kilichopita kiliendelea kumzungumzia Muhammad bin Muhammad bin Nu’man mashuhuri kwa jina la Sheikh Mufid, mmoja wa Maulamaa na wanazuoni mashuhuri mno katika ulimwengu wa Kishia. Tulisema kuwa, utendaji wa Sheikh Mufidi katika elimu ya fikihi na teolojia unahesabiwa kuwa ni utendaji wa muelekeo wa kutumia akili. Mwanazuoni huyu alifanya juhudi kubwa katika kufundisha masomo ya dini katika uga wa fikihi, Usul, teolojia, historia na tafsiri na kuzibainisha elimu hizo kwa mtazamo wa akili na kuyatetea hayo kupitia akili.
Tulibainisha pia kwamba, Sheikh Mufid akiwa alimu, mwanazuoni mkubwa na mujtahidi aliyekuwa na mtazamo mpana na wa kisomi, aliendesha harakati zisizo choka za kukabiliana na fikra za upotoshaji mambo. Sehemu ya 10 ya mfululizo huu juma hili, itabainisha sehemu nyingine muhimu ya harakati za Sheikh Mufid katika uwanja wa kuufanya ukite mizizi utambulisho wa maktaba ya Ahlul Baiti (as). Tafadhalini kuweni nami hadi mwisho wa dakika hizi chache za kipindi hiki ili nikusimulieni yale niliyokuandalieni kwa leo.
Baada ya kuanza kipindi cha ghaiba hususan baada ya Ghaibat al-Kubra ya Imam Mahdi (atfs), moja ya hatari zilizokuwa zikiikabili maktaba ya Ahlul-Baiti (as) ni makosa na upotofu wa makusudi au usio wa makusudi wa baadhi ya watu ambao ulipelekea baadhi ya mambo kupungua umuhimu wake au kuonekana kuwa yanatoka nje ya maktaba ya Ahlul-Baiti (as) na kwa muktadha huo, umuhimu wa mkataba hii adhimu ukawa unapungua. Katika kipindi cha uwepo wa Maimamu watoharifu (as) kila mara kulipokuwa kukijitokeza hatari kama hii, Imam Maasumu akiwa mhimili na marejeo ya kuaminika kwa ajili ya kupata uhakika alikuwa akirejewa na watu na hivyo kufanikiwa kupata uhakika wa mambo kupitia miongozo na ubainishaji wake wa mambo. Kwa msingi huo, makosa na upotofu haukuwa na uwezo wa kudumu kwa muda mrefu.
Lakini katika zama za ghaiba hali ya mambo ilikuwa kinyume. Kwa upande mmoja, kila siku kulikuwa kukijitokeza mahitaji mapya katika jamii ambapo kulihitajia majibu ya lazima. Aidha katika upande wa pili, Waislamu hawakuwa na Imam Maasumu wakati huo hali ambayo ingeweza kupelekea kuibuka tofauti za kimitazamo baina ya wasomi wa dini jambo ambalo tabaani lilikuwa ni la kawaida.
Katika mazingira kama haya, njia kwa ajili ya fikra, mitazamo na uelewa tofauti kuhusiana na Misingi ya Dini na matawi yake ilikuwa ikibakia wazi. Mazingira haya kwa hakika yangeweza katika kipindi cha muda mrefu kupindua kikamilifu njia ya maktaba ya Ahlul Baiti (as).
Hapa ndipo jukumu la wasomi na wanazuoni wa uma katika zama zile linapopata umuhimu nalo ni kuwa, Ushia ukiwa mfumo wa kifikra na kivitendo, ulipaswa kuainisha mipaka kwa upande wa kiitikadi na kivitendo. Tabaan uainishaji huu wa mipaka ulipaswa kutimia kwa kustafidi na turathi zenye thamani za maneno ya Maimamu watoharifu (as) na hivyo kuwapa uwezo wanazuoni na wanafikra wa Kishia wa kuzuia upotovu wa kimisingi. Jambo hili halikuwa limefanyika kabla ya zama zama za Sheikh Mufid.
Sheikh Mufid akiwa na nia ya kufikia lengo lake hili kubwa, alifanya harakati nyingi za kielimu ambapo hapa sisi tutaashiria baadhi tu kutokana na ufinyu wa wakati. Katika uga wa fikihi, Sheikh Mufid aliandika kitabu cha Muqni’ah. Kitabu hiki chenye thamani kubwa, takribani kinajumuisha duru nzima na kamili ya fikihi na ndani yake kinaonyesha wazi njia sahihi ya kunyambua hukumu kutoka katika vyanzo vyake vikuu. Aidha katika kitabu chake kingine cha al-Tadhkirat Usul al-Fiqih, kwa mara ya kwanza Sheikh Mufid alionyesha kanuni za kifikihi za kunyambua hukumu na kutoa fatuwa kupitia kanunu hizo.
Katika uwanja wa teolojia pia, alimu huyu alitoa changamoto kwa maktaba nyingine za kiitikadi kwa kuziita katika vikao cha mijadala na midahalo na kisha kujadiliana na wasomi wa maktaba hizo. Kati ya makundi hayo ya kiitikadi, Sheikh Mufid alikuwa na vikao vingi zaidi na kundi la al-Mu’utazilah. Hilo lilitokana na kuwa, baadhi ya misingi ya Mu’tazilah ilikuwa ikishabihiana na Mashia na mshabaha huo ulikuwa ukipelekea baadhi ya kukosea kwa kuyahesabu makundi haya mawili kuwa ni kundi moja au wengine kutambua kwamba, Mu’utazilah ni chimbuko la itikadi nyingi za madhehebu ya Shia.
Kwa muktadha huo, juhudi za Sheikh Mufid za kupinga na kukosoa kwa hoja itikadi za kundi la Mu’utazilah ni mfano na kielelezo cha wazi cha kuchora na kuanisha mpaka wa maktaba ya Ahlul-Baiti (as).
Apenzi wasikilizaji athari muhimu kabisa ya Sheikh Mufid katika uwanja huu ni kitabu cha Awailul Maqaalat Fil Madhaahib Wal-Mukhtaraat (اوائل المقالات فی المذاهب و المختارات), ambacho aliakiandika akibainisha tofauti zilizopo baina ya Mashia na kundi la Mu’utazilah. Kupitia haya inafahamika wazi ni jinsi gani Sheikh Mufid alikuwa na kipaji cha hali ya juu katika historia ya Ushia na Uislamu kwa ujumla; kwani alikuwa mtu wa kwanza kuchora na kuainisha mipaka ya maktaba ya Ushia katika elimu za fikihi na teolojia.
Hatimaye baada ya miaka mingi ya hima na idili kubwa katika kueneza elimu, harakati ambazo zilijaa ikhlasi na nia safi, Sheikh Mufid akaaga duni mwaka 413 Hijria.
Historia inaonyesha kuwa, makumi ya maelfu ya watu walijitokeza na kumswalia Swala ya maiti. Kwa hakika athari za kielimu za Sheikh Mufid na mchango wake mkubwa aliovirithisha vizazi vilivyokuja baadaye umekuwa ni mwenge wenye kuangazia ulimwengu wa Kiislamu. Hata matukio machungu na ya umwagaji damu yaliyotokea katika mji mkuu wa utawala wa Bani Abbas pamoja na dhoruba za taasubi na nia mbaya hazikuweza kuzima taa ya elimu na amali ya Sheikh Mufid ambayo ilikuwa imeunganishwa na mti mwema wa elimu za Qur’ani na maarifa ya Ahlul-Baiti (as).
Sheikh Mufid aliaga dunia katika mji wa Baghdad akiwa na umri wa miaka 77 na kuzikwa katika mji wa Kadhmein. Alimu huyu mashuhuri anaendelea kukumbukwa wengi na utajo wake umebakia kutokana na mchango wake mkubwa alioutoa katika ulimwengu wa Kiislamu ambapo katika zama zake aliheshimiwa hata na wafuasi wa madhehebu nyingine.
Mpenzi msikilizaji wa muda wa kipindi chetu kwa leo umefikia ukingoni. Tukutane tena juma lijalo katika sehemu nyingine ya mfululizo huu.
Ahsanteni kwa kunitegea sikio na kwa herini.