Jumanne, Mei 12, 2020
Leo ni Jumanne tarehe 18 Ramadhani 1441 Hijria, inayosadifiana na Mei 12 mwaka 2020 Miladia
Siku kama ya leo miaka 200 iliyopita, alizaliwa Florence Nightingale, mwanzilishi wa uuguzi wa kisasa huko Florence nchini Italia. Nightingale aliyejulikana kwa jina mashuhuri la 'mwanamke mwenye taa mkononi' alikuwa muuguzi na mwanahesabati mashuhuri wa Uingereza. Alipewa lakabu ya 'mwanamke mwenye taa mkononi' kutokana na uvumilivu wake mkubwa na kujinyima usingizi kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa nyakati za usiku. Alifanya juhudi kubwa pia kwa ajili ya kuboresha huduma za afya katika hospitali nyingi za Uingereza. Kazi hiyo aliyoifanya kwa miaka mingi na bila kuchoka bila shaka ilimdhoofisha sana kimwili kwa kadiri kwamba alikuwa kipofu mwishoni mwa umri wake ambapo hatimaye aliaga dunia tarehe 13 Agosti 1910 Milaadia.
Siku kama ya leo miaka 145 iliyopita, yaani tarehe 18 Ramadhani 1296 Hijiria, alizaliwa Abdul-Adhim Khan Qarib, mtaalamu wa fasihi na mtafiti mkubwa wa Iran huko mjini Gorgan moja ya miji ya kaskazini mashariki mwa Iran. Baada ya masomo yake ya awali, alianza kufanya utafiti katika elimu ya swarfu, nahw, mantiki, hisabati na fasihi na kufikia daraja ya ualimu katika elimu hizo. Khan Qarib ameandika vitabu vingi kuhusiana na lugha ya Kifarsi moja ya vitabu hivyo kikiwa ni kitabu cha ‘Kanuni za Kifarsi’ na ‘Mwanzo wa Fasihi na Faida za Fasihi.’ Aidha alifanya kazi ya kusahihisha baadhi ya athari muhimu za fasihi ya lugha ya Kifarsi.
Siku kama ya leo miaka 75 iliyopita, Berlin mji mkuu wa Ujerumani iligawanywa katika sehemu mbili za Mashariki na Magharibi. Kwa mujibu wa mapatano yaliyofikiwa baada ya kumalizika Vita vya Pili vya Dunia kati ya serikali nne zilizoiteka Ujerumani, mji huo uligawanywa na kudhibitiwa na serikali za Russia, Ufaransa, Uingereza na Marekani. Muda mfupi baadaye mji huo ulizingirwa na Urusi ya zamani. Harry Truman rais wa wakati huo wa Marekani alichukua uamuzi wa kuvunja mzingiro huo wa Urusi. Katika kutekeleza hatua hiyo Marekani ilikaribia kupigana vita na Urusi. Matokeo mengine ya hali hiyo ilikuwa ni kugawanywa Ujerumani katika sehemu mbili za Magharibi na Mashariki.
Siku kama ya leo Miaka 50 iliyopita na kwa mujibu wa azimio nambari 278 la Umoja wa Mataifa Bahrain ilitengwa na ardhi ya Iran. Kabla ya kudhihiri Uislamu, nchi hiyo ndogo iliyo katika Ghuba ya Uajemi ilikuwa katika utawala wa Iran na baada ya kubuniwa utawala wa Kiislamu ikawa inadhibitiwa na makhalifa wa Kiislamu. Mwanzoni mwa karne ya 7 Hijiria kwa mara nyingine tena nchi hiyo iliunganishwa na Iran na baada ya hapo ikawa chini ya himaya ya Uingereza. Licha ya hayo Iran iliendelea kudai udhibiti na utawala wake kwa Bahrain na kulalamikia vikali hatua ya Uingereza ya kuitawala nchi hiyo.
Siku kama ya leo miaka 41 iliyopita sawa na tarehe 23 Ordebehesht 1358 Hijiria Shamsia, mkataba wa kutoshtakiwa Wamarekani nchini Iran au Capitulation Accord ulifutwa nchini kufuatia mapambano yasiyosita ya wananchi Waislamu wa Iran, ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Kiislamu na kuasisiwa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu. Kwa mujibu wa mkataba huo, raia yeyote wa Marekani aliyekuwa nchini Iran alikuwa na kinga kamili ya kisheria dhidi ya kufunguliwa mashtaka. Kwa kadiri kwamba hakuna taasisi au chombo chochote cha kisheria cha Iran kilichokuwa na mamlaka ya kumfungulia mashtaka na kumuhukumu raia wa Marekani aliyekuwa Iran na kesi za raia hao wa Kimarekani zilipaswa kusikilizwa katika nchi yao.
Siku kama ya leo miaka 12 iliyopita, tetemeko kubwa la ardhi lililokuwa na ukubwa wa 7.9 kwa kipimo cha rishta, liliukumba mji wa Sichuan ulioko kusini magharibi mwa China. Katika tetemeko hilo la kutisha, watu wapatao 87,000 walifariki dunia na wengine laki tatu na 80,000 kujeruhiwa. Aidha tukio hilo la kutisha liliwaacha bila makazi mamilioni ya watu nchini China. Zilzala hiyo inahesabiwa kuwa moja ya mitetemeko mikubwa ya ardhi iliyowahi kuikumba China katika miongo mitatu iliyopita.