May 14, 2020 19:57 UTC
  • Ijumaa tarehe 15 Mei, 2020

Leo ni Jumaa tarehe 21 Ramadhani mwaka 1441 Hijria, sawa na tarehe 15 Mei 2020 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1401 iliyopita katika mwaka wa 40 Hijria Qamaria Imam Ali bin Abi Talib (as) Khalifa wa baada ya Mtume Muhammad (saw) na mmoja wa watu wa Nyumba Tukufu ya Bwana Mtume alikufa shahidi. Siku mbili kabla ya hapo Imam Ali (as) alielekea msikitini kwa ajili ya Swala ya asubuhi na akiwa katika sijda alipigwa upanga kichwani na Ibn Muljim aliyekuwa mfuasi wa tapo la Khawarij na kumpasua utosini. Imam Ali (as) alikufa shahidi katika siku kama ya leo na hivyo kufikia saada aliyokuwa akiitaraji daima, yaani kufa shahidi katika njia ya Mwenyezi Mungu. Kuuliwa shahidi Imam Ali (as) kulisababisha pigo na msiba usioweza kusahaulika wala kufutika kwa Uislamu na Waislamu. Kitabu cha Nahajul-Balaghah ni turathi ya thamani ya baadhi ya maneno ya Imam Ali (as) ambacho kinadhihirisha balagha na fasaha ya hali ya juu ya mutukufu huyo. Mawaidha yake hayo ya hekima yamejaa maarifa ya irfani (kumjua Mwenyezi Mungu) na nasaha mbalimbali za akhlaqi na kijamii kuelekea kwenye fadhila na ukamilifu.

Tarehe 21 Ramadhani miaka 337 iliyopita alifariki dunia faqihi na mwanazuoni mashuhuri wa Kiislamu Sheikh Abu Jaafar Muhammad bin Hassan maarufu kwa jina la Sheikh Hurr al Aamili huko Jabal Amil nchini Lebanon. Alitokea kuwa miongoni mwa maulama na watafiti wakubwa wa Kiislamu. Sheikh Hurr al Amili ameandika vitabu vingi vya fiqhi na hadithi na miongoni mwavyo ni kile cha Wasaailu Shia ambacho kina nafasi maalumu katika duru za elimu ya fiqhi.

Sheikh Hurr al Aamili

Siku kama ya leo miaka 244 iliyopita, sawa na tarehe 15 Mei 1776 Miladia, ilitengenezwa meli ya kwanza yenye kutumia mvuke. Meli inayotumia nishati ya mvuke ilitengenezwa miaka 70 baada ya kuvumbuliwa nishati ya mvuke na mhandisi wa Kifaransa Denis Papin. Utumiaji wa nishati ya mvuke katika meli ulileta mabadiliko makubwa katika sekta ya usafiri wa baharini.

Meli ya nishati ya mvuke

Siku kama ya leo miaka 161 iliyopita, sawa na tarehe 15 Mei 1859 Miladia, alizaliwa Pierre Curie msomi na mwanafizikia wa Ufaransa. Kipaji cha masomo ya hesabati na fizikia alichokuwa nacho kilianza kuonekana tokea ujana wake, na hatimaye kuibuka kuwa mtafiti mkubwa katika nyanja hizo. Mwaka 1898 mwanafizikia huyo wa Kifaransa alifanikiwa kugundua Radium akisaidiana na mkewe Bi. Marie Pierre. Pierre Curie aliaga dunia mwaka 1906.

Pierre Curie na Marie Pierre

Siku kama ya leo miaka 158 iliyopita, sawa na tarehe 15 Mei 1862 Miladia, alizaliwa Arthur Schnitzler mwandishi wa visa wa nchini Austria. Bibi na babu wa Arthur walikuwa matabibu na kutokana na hali hiyo, yeye pia akasomea taaluma hiyo na kufanikiwa kupata shahada katika uga huo. Hata hivyo aliachana na taaluma hiyo na kujiunga na taaluma nyingine aliyokuwa akiipendelea, yaani ya uandishi. Arthur Schnitzler pia alikuwa na ujuzi katika masuala ya kisaikolojia ambapo aliandika vitabu kadhaa katika uwanja huo. Miongoni mwa athari zake ni pamoja na kitabu kinachoitwa 'Kasuku wa Kijani' 'Ardhi Pana' na 'Kuruka Kuelekea Kwenye Giza.' Arthur Schnitzler alifariki dunia mwaka 1931 Miladia.

Arthur Schnitzler

Siku kama ya leo miaka 101 iliyopita, sawa na tarehe 15 Mei 1919 mji wa Izmir moja ya miji ya kihistoria na muhimu nchini Uturuki, ulitekwa na wanajeshi wa Mustafa Kamal Pasha, mwasisi wa Jamhuri ya Uturuki, baada ya kujiri mapigano yaliyopelekea kuuawa watu wengi. Izmir iko magharibi mwa Uturuki, na harakati ya Warepublican ya Uturuki ilianzia katika mji huo wa kihistoria.

Mji wa Izmir, Uturuki

Siku kama ya leo miaka 80 iliyopita, sawa na tarehe 15 Mei 1940 Miladia, jeshi la Ujerumani liliivamia na kuikalia kwa mabavu nchi ya Uholanzi baada ya shambulio kubwa lililodumu kwa siku 5 katika Vita Vikuu vya Pili vya Dunia. Wanajeshi wa Kinazi wa Ujerumani walianza kuzishambulia nchi za Ufaransa, Ubelgiji, Uholanzi na Luxemburg huko magharibi mwa Ujerumani tangu tarehe 10 Mei na kufanikiwa kuzidhibiti nchi zote hizo. Uholanzi ilijipatia uhuru wake mwaka 1945.

Wanazi wa Ujerumani wakivamia nchi ya Uholanzi