May 15, 2020 21:57 UTC
  • Jumamosi, Mei 16, 2020

Leo ni Jumamosi tarehe 22 ya mwezi Mtukufu wa Ramadhani 1441 Hijria mwafaka na tarehe 16 Mei 2020 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1168 iliyopita, alifariki dunia Ibn Majah, mpokezi wa hadithi na mfasiri mashuhuri wa Qur’ani wa Kiislamu. Ibn Majah alizaliwa mwaka 209 Hijria katika mji wa Qazvin nchini Iran. Alielekea katika nchi mbalimbali za Kiislamu ili kujifunza elimu ya hadithi. Aliandika kitabu chake mashuhuri kwa jina la "Sunan Ibn Majah" baada ya kuhitimu masomo katika elimu ya hadithi, kitabu ambacho ni moja kati ya vitabu sita vya hadithi vyenye itibari vya Waislamu wa madhehebu ya Suni. Aidha vitabu vingine vya Ibn Majah ni Tafsirul Qur'an na Tarikh Qazvin.***

Ibn Majah al-Qazwini

 

Miaka 518 iliyopita katika siku kama ya leo, ardhi ya Honduras inayopatikana leo huko Amerika Kusini iliunganishwa na makoloni ya Muhispania. Kabla ya hapo Honduras ilikuwa kituo cha utamaduni wa kaumu ya Maya. Hata hivyo baada ya Honduras kuvamiwa na kukaliwa kwa mabavu na Uhispania, kabila hilo liliangamizwa na kupotea. Mwanzoni mwa karne ya 19 Miladia na kutokana na kuvurugika hali ya ndani ya Uhispania, Honduras kama ilivyokuwa kwa makoloni mengine, ilitumia fursa hiyo kuweza kujipatia uhuru wake. ***

Ardhi ya Honduras

 

Katika siku kama ya leo miaka 232 iliyopita, alizaliwa mjini Hamburg Friedrich Ruckert, malenga na mtaalamu wa masuala ya mashariki ya dunia wa nchini Ujerumani. Alikuwa mtafiti mkubwa wa masuala ya mashariki, aliyefundisha katika vyuo vikuu vya Ujerumani. Alifanya juhudi ya kutafsiri mashairi kwa lugha ya Kifarsi, Kiarabu na Kichina. Kadhalika alijifunza fasihi na tamaduni za eneo hilo na kuzitumia katika kusoma mashairi. Aidha Friedrich Ruckert  alikuwa mmoja wa malenga wa Kijerumani aliyefanikiwa kutarjumu diwani ya mashairi ya Hafez (malenga mkubwa wa Kiirani) katika lugha ya Kijerumani ambapo tarjama yake imechapishwa mara kadhaa nchini humo. Miongoni mwa athari ya Friedrich Ruckert ni pamoja na kitabu kinachoitwa 'Msimu wa Machipuko wa Upendo' na 'Sharqiyat.'***

 Friedrich Ruckert,

 

Siku kama ya leo miaka 155 iliyopita, Haj Abdul-Hussein Tehrani, maarufu kwa jina la Sheikhul-Iraaqiyyin, mmoja wa maulama wakubwa wa Iran. Haj Abdul-Hussein Tehrani alitabahari katika elimu ya fiqhi, huku akiwa mcha-Mungu sana. Kadhalika alitambulika kwa kuwa na kumbukumbu ya hali ya juu katika msomo ya dini. Mbali na fiqhi, pia alikuwa alimu katika elimu ya hadithi na tafsiri ya Qur'an Tukufu. Alifanya juhudi kubwa katika kuasisi maktaba na kukusanya turathi za Kiislamu ambapo baada ya kufariki kwake dunia kuliasisiwa maktaba kubwa kwa ajili ya wanafunzi wa Kiislamu. ***

Haj Abdul-Hussein Tehrani, maarufu kwa jina la Sheikhul-Iraaqiyyin,

 

Miaka 32 iliyopita Jeshi Jekundu la Umoja wa Kisovieti lilianza kuondoka nchini Afghanistan. Baada ya Nur Muhammad Taraki kupinduliwa, serikali ya kwanza ya kikomunsti iliyokuwa ikipata himaya ya moja kwa moja ya Urusi ya zamani ilianzishwa nchini Afghanistan. Utawala wa Taraki uliondolewa madarakani mwanzoni mwa mwaka 1979 kupitia mapinduzi mengine yaliyoongozwa na Hafidhullah Amin mmoja wa watu wake wa karibu. Lakini Warusi hawakumpenda Hafidhullah ambaye alikuwa akitaka kujikurubisha kwa Marekani na kuanzisha uhusiano kati ya Afghanistan na Mashariki na vilevile Magharibi na hivyo wakaipindua serikali yake. ***

Kuondoka vikosi vya Jeshi Jekundu la Umoja wa Kisovieti katika ardhi ya Afghanistan

 

Katika siku kama ya leo miaka 23 iliyopita, Jenerali Mobutu Sese Seko rais na dikteta wa zamani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Zaire ya zamani, aliikimbia nchi hiyo baada ya vikosi vya majeshi ya waasi vilivyokuwa vikiongozwa na Laurent Kabila kukaribia mji wa Kinshasa. Mobutu alichukua madaraka ya nchi hiyo mnamo mwaka 1965 kupitia mapinduzi ya kijeshi na kisha kutawala kwa muda wa miaka 32. Licha ya kiongozi huyo kuwa dikteta asiye na huruma, lakini alikuwa akiungwa mkono na madola ya Magharibi hasa Marekani na Ufaransa. Kutokana na Congo DR kuwa katika eneo nyeti na muhimu kijiografia katikati mwa bara la Afrika na kuwa na utajiri mkubwa wa madini ikiwemo almasi, imekuwa ikizingatiwa sana na kumezewa mate na nchi za Magharibi. Siku moja baada ya Mobutu kuikimbia nchi hiyo, vikosi vya waasi viliuteka mji wa Kinshasa na kiongozi wao yaani Laurent Kabila, akashika hatamu za uongozi wa nchi. ***

Jenerali Mobutu Sese Seko

 

Na siku kama ya leo miaka 11 iliyopita mwafaka na tarehe 27 Ordibehesht mwaka 1388 Hijria Shamsia, alifariki dunia Ayatullah Muhammad Taqi Bahjat Foumani, mmoja wa Marajii Taqlidi na maurafaa wakubwa wa Kishia. Alizaliwa mwaka 1294 Hijria Shamsia katika mji wa Fouman ulioko katika mkoa wa Gilan kaskazini mwa Iran. Baada ya kupata elimu ya msingi ya kidini, mwaka 1308 Hijria Shamsia alielekea katika Chuo Kikuu cha Kidini cha Najaf nchini Iraq. Ayatullah Bahjat alikuwa mashuhuri sana kutokana na uchaji Mungu wake. Kitabus Swalat, Jamiul Masail na Wasilatun Najat ni baadhi ya vitabu mashuhuri vya msomi huyo.***

Ayatullah Muhammad Taqi Bahjat Foumani, mmoja wa Marajii Taqlidi na maurafaa wakubwa wa Kishia