Jumapili, tarehe 17 Mei, 2020
Leo ni Jumapili tarehe 23 ya Ramadhani mwaka 1441 Hijria, sawa na tarehe 17 Mei, 2020 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 271 iliyopita, sawa na tarehe 17 Mei mwaka 1749 Miladia, alizaliwa nchini Uingereza Edward Jenner. Tabibu huyo Muingereza alifanikiwa kugundua chanjo ya ndui akiwa na umri wa miaka 45 wakati alipoelekea nchini India. Kuanzia hapo ugonjwa huo wa ndui uliweza kutibiwa kwa kutumia chanjo hiyo. Na ilipofika mwaka 1979 maradhi hayo yaliweza kutokomezwa kabisa duniani.
Siku kama ya leo miaka 187 iliyopita sawa na tarehe 23 Ramadahni mwaka 1254 Hijria, ilikamilika kazi ya uandishi wa kitabu cha ‘Jawaahirul-Kalaam’ ambacho kimejumuisha masuala muhimu ya sheria za Mwenyezi Mungu juu ya halali na haramu na kadhalika sheria mbalimbali za dini ya Kiislamu. Ni vyema kuashiria kuwa, kitabu cha Jawaahirul-Kalaam kimebainisha kwa undani masuala mengi ya sheria kiasi kwamba hadi sasa hakuna msomi aliyeweza kuandika kitabu kama hicho. Kunukuu kauli za wasomi wakubwa wa sheria za Kiislamu na kuzitolea ushahidi kwa umakini wa hali ya juu, ni kati ya nukta muhimu za kitabu hicho. Ayatullah Muhammad Hassan Najafi, mtunzi wa kitabu hicho, alianza kazi ya uandishi wa kitabu cha Jawaahirul-Kalaam akiwa na umri wa miaka 25 huku akitumia karibu miaka 30 kukiandika na kutokea kuitwa kwa lakabu ya ‘Sheikhul-Fuqahaa.’ Katika kipindi cha maisha yake kulitawala hujuma za fikra potofu za genge la Uwahabi na watu wa kundi la Ikhbariyyun suala ambalo lilimfanya Ayatullah Muhammad Hassan Najafi kuelezea umuhimu wa kuwa na kiongozi wa Umma wa Kiislamu. Ni baada ya hapo ndipo kukazaliwa fikra ya kuwepo waliyyu Faqihi ‘walii kiongozi' anayesimamia masuala ya sheria za Kiislamu.
Siku kama ya leo miaka 155 iliyopita, yaani tarehe 17 Mei mwaka 1865, mkataba wa kwanza wa kimataifa kuhusiana na mawasiliano ulitiwa saini mjini Paris na wawakilishi wa nchi 20 duniani na kuasisiwa Taasisi ya Kimataifa ya Telegrafu. Kwa sababu hiyo siku ya leo imepewa jina la 'Siku ya Kimataifa ya Mawasiliano.' Mwaka 1932 Miladia na kwa mujibu wa maamuzi ya kongamano la mjini Madrid, Uhispania, jina la Umoja wa Kimataifa wa Telegrafu ya Mawasiliano ya Mbali lilibadilishwa na kuitwa ITU.
Siku kama ya leo miaka 81 iliyopita, sawa na tarehe 17 Mei 1939 Miladia, dola la Uingereza ambalo Palestina ilikuwa chini ya mamlaka yake, lilichapisha kitabu kwa jina la "Kitabu Cheupe" na hivyo kukawa kumepigwa hatua nyingine katika njia ya kuasisiwa utawala ghasibu wa Israel. Wapalestina ambao walikuwa wakifahamu vyema uungaji mkono na upendeleo wa Uingereza kwa Wazayuni, waliukataa mpango uliokuwa umependekezwa katika kitabu hicho kwa ajili ya kuipatia ufumbuzi kadhia ya Palestina.
Siku kama ya leo miaka 49 iliyopita yaani tarehe 23 Ramadhani mwaka 1392 Hijria Qamaria, Allamah Muhammad Hussein Tabatabai mwanafalsafa, arifu na faqihi mkubwa wa Kiirani alikamilisha kazi ya uandishi wa tafsiri kubwa na ya aina yake ya Qur’ani ya al Mizan. Tafsiri hiyo ya Qur’ani ni moja kati ya tafsiri kubwa na makini zaidi za Qur’ani Tukufu na iliandikwa katika kipindi cha karibu miaka 20. Sifa kubwa zaidi ya tafsiri hiyo ni kwamba imefasiri aya za Qur’ani kwa msaada wa aya nyingine za kitabu hicho cha Mwenyezi Mungu. Tafsiri hiyo kubwa na adhimu iliandikwa na Allamah Tabatabai kwa lugha ya Kiarabu na hadi sasa imetarjumiwa katika lugha mbalimbali kama Kifarsi, Kiingereza na Kihispania.