May 18, 2020 00:43 UTC
  • Jumatatu, 18 Mei, 2020

Leo ni Jumatatu tarehe 24 ya mwezi Mtukufu wa Ramadhani 1441 Hijria mwafaka na tarehe 18 Mei 2020 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 731 iliyopita, alifariki dunia Qutbuddin Shirazi, tabibu, mwanahesabati, mwanafikizia na mwanafalsafa wa Kiirani katika mji wa Tabrizi huko kaskazini magharibi mwa Iran. Qutbuddin Shirazi alikuwa miongoni mwa wanafunzi wa mwanazuoni mashuhuri wa Kiislamu Khaja Nasiruddin Tusi. Alibobea pia katika elimu za mantiki na irfani. Alifanya hima kubwa kutafuta elimu ya tiba na alihudumu kwa miaka mingi kama tabibu katika hospitali ya Shiraz, kusini mwa Iran. Qutbuddin Shirazi alikuwa mtu wa kwanza kufanya uchunguzi kuhusu upinde wa mvua na kupata tafsiri ya kisayansi kuhusu suala hilo. Mwanazuoni huyo mkubwa wa Kiislamu ameandika vitabu vingi katika taaluma mbalimbali. ***

Qutbuddin Shirazi,

 

Miaka 216 iliyopita yaani tarehe 18 Mei mwaka 1804 Miladia, Bunge la Seneti la Ufaransa lilipasisha uamuzi wa kumtangaza Napoleone Bonaparte kuwa mfalme wa Ufaransa na kwa utaratibu huo kwa mara nyingine tena utawala wa kifalme ukatawala nchini humo kwa miaka 15. Hata hivyo, mfumo wa kifalme ulifikia mwisho miaka kumi baadaye, sawa na tarehe 11 Aprili mwaka 1814, baada ya Napoleone Bonaparte kushindwa katika vita vyake na nchi za Ulaya na kubaidishwa. ***

Napoleone Bonaparte

 

Katika siku kama ya leo miaka 190 iliyopita,  jeshi la Ufaransa lilianzisha operesheni ya kuikalia kwa mabavu Algeria. Kisingizio cha Charles wa Kumi mfalme dikteta wa wakati huo wa Ufaransa cha kutoa amri ya kufanywa mashambulio hayo, ilikuwa sababu ya hujuma hiyo kufuatia vitisho vilivyokuwa vimetolewa miaka mitatu kabla na mtawala wa wakati huo wa Algeria akiitaka Ufaransa ilipe deni la nchi hiyo la Franc milioni saba. Hata hivyo, kinyume na ilivyodhania Paris, wananchi wa Algeria walisimama kidete katika kukabiliana na mashambulio hayo. Ijapokuwa Ufaransa ilifanikiwa kuikalia kwa mabavu Algeria na kupora maliasili na utajiri wa nchi hiyo, lakini hatimaye nchi hiyo ya Kiafrika ilijipatia uhuru wake mwaka 1962. ***

Bendera ya Algeria

 

Siku kama ya leo miaka 148 iliyopita, alizaliwa Bertrand Russell mwanafalsafa na mwanahesabati mashuhuri wa Uingereza. Russell baada ya kumaliza masomo yake ya awali alijiunga na Chuo Kikuu cha Cambridge mjini London. Russell alikuwa mpinzani mkubwa wa Vita vya Kwanza na vya Pili vya Dunia, pamoja na vita vya Marekani dhidi ya Vietnam, na hata kufikia hatua ya kufungua mashtaka dhidi ya viongozi wa Marekani, mashtaka yaliyopewa jina lake la Russell. Msomi huyo alifanikiwa kupokea tuzo ya fasihi ya Nobel mwaka 1950. Russell alifariki dunia mnamo mwaka 1970. ***

Bertrand Russell

 

Miaka 46 iliyopita, nchi ya India ilifanya jaribio la kwanza la nyuklia katika jangwa la Rajasthan magharibi mwa nchi hiyo na jirani na mpaka wake na Pakistan. Kwa utaratibu huo, India nayo ikawa nchi ya sita baada ya Marekani, Umoja wa Kisovieti, Ufaransa, Uingereza na China katika uwanja huo wa nyuklia. Miaka 24 baadaye yaani mwaka 1998 India ilifanya majaribio mengine matano ya nyuklia na kufanikiwa kutengeneza silaha za atomiki. ***

Jaribio la nyuklia

 

Na katika siku ama ya leo miaka 43 iliyopita, kwa mujibu wa azimio la Mkutano wa Kumi na Mbili wa Baraza Kuu la Kamati ya Kimataifa ya Makumbusho, siku hii iliainishwa na kutangazwa kuwa "Siku ya Makumbusho Duniani." Moja ya malengo muhimu ya baraza hilo lilikuwa ni kupanuliwa makumbusho katika kona mbalimbali duniani, kuweko ushirikiano wa kila upande wa majumba ya makumbusho ulimwenguni kwa shabaha ya kufikia malengo ya kiutamaduni na wakati huo huo kuzuia kuangamizwa athari za kale za kiutamaduni. Ni vyema kuashiria hapa kwamba, lengo  la kuanzishwa sehemu kwa jina la makumbusho ni kuhifadhi athari za kale za vizazi vilivyopita kwa ajili ya vizazi vijavyo. ***

Siku ya Makumbusho Duniani

 

Tags