May 20, 2020 00:56 UTC
  • Jumatano, tarehe 20 Mei, 2020

Leo ni Jumatano tarehe 26 Ramadhan mwaka 1441 Hijiria, inayosadifiana na tarehe 20 Mei mwaka 2020 Miladia.

Miaka 514 iliyopita katika siku kama ya leo, yaani tarehe 20 Mei mwaka 1506 Miladia, aliaga dunia baharia mashuhuri wa Kiitalia Christopher Columbus. Columbus alizaliwa Septemba 21 mwaka1 451 Miladia huko kusini mwa Italia. Mwezi Agosti mwaka 1492 Miladia, Christopher Columbus, alianza safari yake kuelekea Bahari ya Atlantiki. Watu wengi wanamtambua Columbus kuwa mtu wa kwanza kutoka Ulaya aliyevumbua bara la Amerika. Tangu wakati huo historia ya bara hilo ikaandikwa kwa mujibu wa matakwa ya wazungu na wahamiaji wapya. Historia hiyo iliambatana na machungu ya ukoloni kutoka maeneo tofauti ya dunia dhidi ya wakazi asili wa ardhi hizo, huku ubaguzi ukiwa ndizo siasa kuu zilizotekelezwa na wahamiaji hao. 

Christopher Columbus

Miaka 316 iliyopita katika siku kama ya leo  sawa na tarehe 26 Mwezi wa Ramadhani mwaka 1125 Hijria Qamaria, aliaga dunia Mohammad Khonsari aliyekuwa na lakabu ya Jamaluddin, alim na mwanazuoni mkubwa Muirani wa zama zake. Alizaliwa katika familia yenye kufungamana kikamilifu na mafundisho ya Kiislamu katika mji wa Isfahan, mmoja kati ya miji ya kati mwa Iran. Alisomea taaluma mbali mbali za Kiislamu kama vile itikadi, mantiki, falsafa, fiqhi na tafsiri. Jamaluddin Khonsari aliandika vitabu kadhaa ikiwa ni pamoja na ufafanuzi kuhusu kitabu cha Shifaa cha Abu Ali Sina, msomi maarufu Muirani. 

Mohammad Khonsari

Siku kama ya leo miaka 214 iliyopita alizaliwa John Stuart Mill mwanafalsafa na mwanauchumi wa Uingereza. Stuart Mill alilelewa na kufunzwa na baba yake elimu za mantiki na uchumi na baadaye kuanza kuandika magazeti. Mill pia alichaguliwa kuwa mwakilishi wa bunge la Uingereza kwa duru moja. Vitabu muhimu vya mwanauchumi huyo wa Kiingereza ni vile alivyoviita "Principals of Political Economy" na "Principals of Political Science." Mill aliaga dunia mwaka 1873.

Stuart Mill

Siku kama ya leo miaka 118 iliyopita jamhuri huru ilitangazwa huko Cuba na wanajeshi wote wa Marekani wakaondoka katika ardhi ya nchi hiyo. Cuba ambayo iligunduliwa na Christopher Columbus tangu mwaka 1492 Miladia, ilikuwa koloni la Uhispania hadi kufikia mwaka 1898 Miladia. Lakini Marekani iliingiza vikosi vyake nchini humo na kuchukua nafasi ya mkoloni Uhispania baada ya kutoa pigo na kuifukuza nchi hiyo huko Cuba, kwa kisingizio eti cha kuwaunga mkono wanamapambano wapigania uhuru wa Cuba.

Bendera ya Cuba

Miaka 60 iliyopita katika siku kama ya leo, nchi ya Kiafrika ya Cameroon ilijipatia uhuru kutoka kwa mkoloni Mfaransa. Kwa miaka mingi nchi hiyo ilikuwa chini ya ukoloni wa nchi za Ulaya ikiwemo Ujerumani ambayo iliikalia kwa mabavu Cameroon kuanzia mwaka 1884.  Baada ya Ujerumani kushindwa katika Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia Ufaransa na Uingereza ziligawana baina yao ardhi ya Cameroon. Hata hivyo haukupita muda kabla ya kuanza mapambano ya kupigania uhuru nchini humo. Hatimaye mapambano ya kupigania uhuru nchini Cameroon yalizaa matunda katika siku kama ya leo baada ya nchi hiyo iliyoko magharibi mwa Afrika kujipatia uhuru.

Bendera ya Cameroon

Siku kama ya leo, miaka 57 iliyopita, mwafaka na tarehe 20 Mei mwaka 1963, kongamano la kihistoria la nchi za Afrika lilifanyika huko Addis Ababa, Ethiopia. Madola mengi ya Kiafrika yalijinyakulia uhuru katika miaka ya 60 na 70, na katika kipindi hicho hayakuwa na uhusiano baina yao. Ili kuunda jumuiya ya kwanza iliyokusudiwa kuzikurubisha pamoja nchi za Afrika, kongamano la kwanza la nchi hizo lilifanyika katika mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa tarehe kama ya leo. Kongamano hilo ilikuwa hatua ya kwanza ya kuasisiwa Jumuiya ya Nchi za Afrika OAU. Ni vyema kuashiria hapa kwamba, Umoja wa Afrika (AU) ulichukua nafasi ya Umoja wa Afrika (OAU) ambao uliundwa mwaka 1963 kwa shabaha ya kusimamia maslahi ya nchi wanachama, kuhamasisha maendeleo ya bara hilo na kutatua migogoro kati ya nchi Afrika

Nembo ya  Umoja wa Afrika