Jumatatu, 25 Mei, 2020
Leo ni Jumatatu tarehe Pili Mfunguo Mosi Shawwal 1441 Hijria mwafaka na tarehe 25 Mei 2020 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 660 iliyopita, Kundi la mabaharia wa Kifraransa lilifika katika Ghuba ya Guinea. Ghuba ya Guinea inapatikana magharaibi mwa bara la Afrika katika bahari ya Atlantiki. Baada ya muda kupita tangu kundi hilo kufika katika Ghuba ya Guinea, ushawishi wa Ufaransa ndani ya bara hilo ulianza, na taratibu ikaanza kuidhibiti ardhi iliyokuja kujulikana baadaye kama Guinea. Nchi ya Guinea iliendesha harakati za mapambano ya miaka mingi hadi ikafanikiwa kupata uhuru wake mwaka 1958. Guinea ina eneo lenye ukubwa wa kilomitamraba zaidi ya 245,000 na inapakana na nchi za Senegal, Guinea Bissau, Mali, Ivory Coast, Liberia na Sierra Leone. ****

Miaka 128 iliyopita katika siku kama ya leo, alizaliwa Josip Broz Tito, kiongozi wa zamani wa Yugoslavia, huko katika eneo la Hrvatsko Zagorje, kaskazini mwa Zagreb, mji mkuu wa Croatia. Mnamo mwaka 1915, wakati wa Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia Tito alikamatwa katika medani ya vita dhidi ya Urusi; na baada ya kuachiwa huru aliungana na Wakomunisti kupamaba na utawala wa Tsar. Tito aliasisi harakati ya ukombozi wa taifa baada ya Ujerumani kuishambulia Yugoslavia wakati wa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia. Mnamo mwaka 1943 alipewa hadhi ya Jemadari (Marshal), mwaka 1953 akawa Mkuu wa Baraza la Utendaji wa Shirikisho na Kamanda Mkuu wa vikosi vya ulinzi vya Yugoslavia na hatimaye mwaka 1974, Josip Tito akatangazwa kuwa rais wa milele wa nchi hiyo. Katika sera za nje, Tito aliilinda Yugosalvia na ushawishi wa Shirikisho la Kisovieti la Urusi (USSR), na kwa sababu hiyo akajitoa kwenye kambi ya nchi za Kikomunisti duniani. Jemadari Josip Tito aliaga dunia tarehe 4 Mei mwaka 1980 baada ya kuugua kwa muda mrefu. ***

Katika siku kama ya leo miaka 112, kisima cha kwanza cha mafuta cha Iran kilianza kuchimbwa huko katika mji wa Masjid Suleiman kusini magharibi mwa Iran. Mafuta ya kisima hicho yalifikiwa umbali wa kina cha mita 600, mafuta ambayo hatimaye yaliruka hadi kufikia urefu wa mita 25 kutoka uso wa ardhi. Mji wa Masjid Suleiman una umuhimu mkubwa kutokana na upatikanaji wa madini na vyanzo vya mafuta. Ni vyema kutaja hapa kuwa Iran ni moja ya nchi muhimu duniani kwa kuwa na akiba kubwa ya mafuta na ni nchi ya pili yenye akiba kubwa ya gesi duniani baada ya Russia. ***

Siku kama ya leo miaka 57 iliyopita, hati ya Umoja wa Nchi Huru za Kiafrika (OAU) ilisainiwa mjini Addis Ababa, Ethiopia kwa kuhudhuriwa na viongozi wa nchi 32 za bara hilo. Marais Gamal Abdel Nasser wa Misri, Kwame Nkrumah wa Ghana na Ahmed Sekou Toure wa Guinea walikuwa miongoni mwa waasisi wa jumuiya hiyo. Jumuiya ya OAU ilielekeza jitihada zake katika kuleta umoja kati ya nchi za Afrika, kutatua hitilafu kati ya nchi hizo, kutetea haki ya kujitawala ya nchi wanachama na ukombozi wa nchi nyingine za Kiafrika zilizokuwa zingali zinakoloniwa. Mnamo mwezi Julai mwaka 2002, viongozi wa nchi wanachama wa OAU walifanya kikao nchini Afrika Kusini na kuamua kubadilisha jina la jumuiya hiyo kutoka Umoja wa Nchi Huru za Kiafrika (OAU) na kuwa Umoja wa Afrika (AU) sambamba na kuanzisha taasisi kadhaa kwa ajili ya utekelezaji wa maamuzi ya umoja huo na kustawisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya nchi wanachama. Hivi sasa Umoja wa Afrika una nchi 54 wanachama. Makao Makuu ya umoja huo yako Addis Ababa, Ethiopia na kikao cha viongozi wa nchi wanachama hufanyika kila mwaka katika moja ya nchi hizo. ***

Na miaka 15 iliyopita, aliaga dunia Ustadh Rahim Moazzen Zadeh Ardabili mwadhini mashuhuri wa Kiirani. Alizaliwa katika familia ambayo ilikuwa ikishughulisha zaidi na harakati za kidini na kuuadhini. Rahim Moazzen Zadeh Ardabili alikuwa mtoto mkubwa wa Sheikh Abdul-Karim na alifuata njia ya baba yake kwa nguvu zake zote. Baada ya kufariki dunia baba yake, Rahim Moazzen Zadeh Ardabili akaendeleza kazi ya mzazi wake huyo ya kuadhini. Hatimaye mwadhini huyo mashuhuri wa Iran aliaga dunia katika siku kama ya leo akiwa na umri wa miaka 80. ***
