May 26, 2020 02:21 UTC
  • Jumanne, Mei 26, 2020

Leo ni Jumanne tarehe 3 Mfunguo Mosi Shawwal 1441 Hijria, sawa na tarehe 26 Mei, 2020 Miladia.

Siku kama ya leo, miaka 221 iliyopita sawa na tarehe 26 Mei 1799 Miladia, alizaliwa Alexander Pushkin, malenga na mwandishi mkubwa wa Urusi mjini Moscow. Pushkin, alipata umaarufu mkubwa mwaka 1820, baada ya kusambaza majmui ya kitabu kilichosheheni mashairi. Muda mfupi baadaye malenga huyo alitunga shairi lililohusu uhuru, suala lililopelekea kubaidishwa kwake. Katika shairi hilo Alexander Pushkin alielezea kwa kina umuhimu wa uhuru. Akiwa amebaidishwa aliendelea kujishughulisha na kazi ya uandishi ambapo kitabu cha ‘Mfungwa wa Caucasus’ ni miongoni mwa kazi zake. Aidha aliandika vitabu vingine kadhaa.

Alexander Pushkin

Siku kama ya leo miaka 140 iliyopita sawa na tarehe 26 Mei 1880, Charles Louis Alphonse Laveran, daktari wa Kifaransa aligundua chanzo cha ugonjwa wa malaria duniani. Baada ya kupata shahada yake ya uzamifu, Daktari Alphonse Laveran alisafiri Algeria kwa lengo la kuhudumia watu wa nchi hiyo kuhusiana na masuala ya afya na tiba. Akiwa huko alipata fursa ya kuchunguza na kufanya utafiti wa kina kuhusiana na malaria, ugonjwa ambao ulikuwa ukiwaangamiza watu wengi katika pembe tofauti za dunia, ambapo mwaka 1880 alifanikiwa kupata chanzo cha ugonjwa huo. Aligundua kuwa ugonjwa huo ulisababishwa na mbu waanaoitwa Anopheles ambao huishi katika sehemu za unyevunyevu na zilizo na maji yaliyotuama. Mwaka 1907 Alphonse Laveran alitunukiwa zawadi ya Nobel kutokana na juhudi kubwa alizofanya katika uwanja wa tiba na ugunduzi wake wa chanzo cha ugonjwa wa malaria.

Charles Louis Alphonse Laveran

Siku kama ya leo miaka 138 iliyopita sawa na tarehe 26 Mei 1881 Miladia, Ufaransa iliikoloni rasmi nchi ya Kiarabu ya Tunisia. Kabla ya hapo Wafaransa waliingia nchini humo kama wafanyabiashara. Kwa miaka mingi nchi hiyo ilikuwa chini ya himaya ya Ufaransa, lakini katika muongo wa 1930 wananchi wa Tunisia wakaanzisha harakati za ukombozi chini ya uongozi wa Habib Bourguiba, ambapo mwaka 1975 waliung'oa madarakani utawala wa kifalme na kumtawaza Bourguiba kuwa rais wa nchi hiyo. Baada ya kuingia madarakani, Bourguiba alianza kuitawala nchi hiyo kidikteta hadi mwaka 1987 ambapo alipinduliwa na Zein al-Abedeen bin Ali, afisa mkuu wa polisi wakati huo. Zein al-Abedeen pia aliitawala nchi hiyo kwa mkono wa chuma na ukanadamizaji hadi Januari 2011 ambapo alipopinduliwa na wimbi la mwamko wa Kiislamu katika nchi za Kiarabu na kulazimika kukimbilia Saudi Arabia.

Bendera ya Tunisia

Siku kama ya leo miaka 102 iliyopita sawa na tarehe 26 Mei 1918 Miladia, nchi ya Georgia ilijitangazia uhuru na siku hii huadhimishwa nchini humo kwa anwani ya siku ya kitaifa. Awali yaani mwaka 654 Miladia Georgia ilidhibitiwa na Waislamu kama ambavyo kwa muda mrefu pia ilikuwa chini ya udhibiti wa Iran na Roma. Kuanzia karne ya 16 hadi 18 Miladia pia tawala za Iran na Othmania zilizozania udhibiti wa nchi hiyo. Hatimaye kuanzia mwishoni mwa karne ya 18 ufalme wa Tsar ulipenyeza nchini Georgia na taratibu ukaidhibiti nchi hiyo. Baada ya mapinduzi ya mwezi Oktoba 1917 Miladia, tarehe 26 Mei mwaka 1918 Georgia ilijitangazia uhuru na miaka miwili baadaye ikatambuliwa na Russia. Aidha nchi hiyo ilishambuliwa na majeshi ya Urusi ya zamani mwaka 1921 ambapo mwaka 1936 iligeuzwa na kuwa sehemu ya taifa hilo. Hata hivyo kuliibuka vuguvugu la hisia za utaifa nchini Georgia lililowafanya wananchi wake kukataa kuwa chini ya Urusi ya zamani ambapo hatimaye tarehe 9 Aprili mwaka 1991 ilifanikiwa kujitawala.

Nchi ya Georgia

Siku kama ya leo miaka 54 iliyopita, yaani sawa tarehe 26 Mei mwaka 1966 Miladia, Guyana inayopatikana kaskazini mwa Amerika ya Kusini ilipata uhuru wake. Ardhi ya Guyana iligunduliwa na mabaharia wa Kihispania huko kaskazini mwa Amerika ya Kusini karibu miaka 500 iliyopita na baadaye nchi hiyo ikawa chini ya mkoloni Mhispania. Hata hivyo mwanzoni mwa karne ya 17 Miladia, vita vilizuka kati ya wakoloni wa Ulaya kwa ajili ya kulidhibiti eneo hilo ambalo lilijumuisha Guyana, Guyana ya Ufaransa, Surinam na baadhi ya maeneo ya Brazil na Venezuela ya sasa. Mwaka 1815 kulifanyika mkutano wa Vienna ambao uliainisha mipaka ya sasa ya nchi ya Guyana.

Bendera ya Guyana

Na siku kama ya leo miaka 39 iliyopita, sawa na tareje 26 Mei 1981 Miladia, Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi lilibuniwa rasmi. Baraza hilo linazijumuisha nchi sita zilizoko kusini mwa Ghuba ya Uajemi za Saudi Arabia, Kuwait, Imarati, Bahrain, Qatar na Oman. Lengo kuu la kubuniwa baraza hilo lilikuwa ni kuimarisha ushirikiano wa kisiasa, kiuchumi na kijeshi na kuungana mkono dhidi ya uchokozi na vitisho vya nje. Pamoja na hayo lakini baraza hilo hadi sasa limeshindwa kudhamini usalama wa eneo hili nyeti pamoja na maslahi ya kitaifa ya nchi wanachama kutokana na kutegemea kwake nguvu za kigeni na vilevile kutoshirikishwa vyema wanachama wake katika msuala yanayowahusu. Viongozi wa nchi wanachama hukutana mara mbili kwa mwaka ili kuchunguza masuala ya ndani ya baraza hilo na vilevile ya kieneo.

Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi

Tags