Ijumaa, Mei 29, 2020
Leo ni Ijumaa tarehe 6 Mfunguo Mosi Shawwal 1441 Hijiria, sawa na tarehe 29 Mei 2020, Miladia.
Siku kama ya leo miaka 655 iliyopita sawa na tarehe 6 Shawwal nwaka 785 Hijiria, alifariki dunia Ibn Bardes, malenga na mpokeaji wa hadithi wa Kiislamu. Ibn Bardes alizaliwa huko Ba'labak moja ya miji ya Lebanon na kuelekea katika mji wa Damascus baada ya kukamilisha masomo yake ya msingi, ambapo alinufaika na elimu ya maulamaa maarufu wa zama hizo. Msomi huyo wa Kiislamu alisafiri katika nchi mbalimbali za Kiislamu na kuanza kufundisha baada ya kukamilisha masomo yake. Alikuwa mashuhudi baina ya watu kwa kushikamana na dini, kutakasa nafsi na maadili mema. Miongoni mwa vitabu vya msomi huyo ni al I'lamu fii Wafayatil Aalam.
Siku kama ya leo miaka 567 iliyopita, sawa na tarehe 29 Mei 1453 Miladia, ilikombolewa bandari ya Constantine iliyokuwa makao makuu ya Mfalme wa Roma ya Mashariki na vikosi vya Sultan Muhammad Fatih, mtawala wa dola la Othmaniya. Amri ya kwanza iliyotolewa na Muhammad Fatih baada ya kuudhibiti mji huo ilikuwa ni kudhaminiwa usalama na uhuru wa wakaazi wake. Mfalme huyo alitoa amri ya kukarabatiwa mji huo na kujengwa msikiti, ambao leo hii unajulikana kwa jina la Msikiti wa Sultan Ahmed. Ilipofika mwaka 1930 mji wa Constantine ulibadilishwa jina na kuitwa Istanbul, na ni miongoni mwa miji muhimu zaidi ya Uturuki ulioko magharibi mwa nchi hiyo.
Siku kama ya leo miaka 319 iliyopita, sawa na tarehe 29 Mei mwaka 1701 Miladia, alizaliwa Anders Celsius mwanafizikia na mtafiti wa Sweden. Familia yake ilikuwa ya wasomi na baba na babu yake walikuwa wanahisabati. Celsius alivutiwa sana na elimu ya nujumu na mwaka 1730 alifanikiwa kuwa mwalimu wa nujumu katika chuo kikuu cha Uppsala. Mwaka 1742 alipendekeza kutumika daraja ya kipima joto kwa mujibu wa Celsius, iliyoitwa kwa jina lake. Mpangilio huo ulikubaliwa rasmi na kuanza kutumika duniani mwaka 1945, ikiwa ni mwaka mmoja baada ya kufariki dunia mwanafizikia huyo.
Siku kama ya leo miaka 111 iliyopita, sawa na tarehe 29 Mei 1908 Miladia, helikopta ya kwanza iliruka angani kwa mafanikio. Mtengenezaji wa helikopta hiyo alikuwa Igor Sikorsky, raia wa Poland mwenye asili ya Marekani. Utengenezaji wa chombo hicho cha angani ulifungua ukurasa mpya katika mawasiliano na safari za anga. Chombo hicho kilikuwa na sifa kadhaa maalumu zikiwemo za kupaa angani kwa kwenda mbele na kurudi nyuma na pia kuweza kutua na kupaa kikiwa wima. Helikopta hiyo pia iliweza kutulia sehemu moja angani bila kufanya harakati yoyote ile.

Siku kama ya leo miaka 67 iliyopita, sawa na tarehe 29 Mei 1953, Edmund Hillary mpanda milima kutoka New Zealand na Tenzing Norgay mpanda milima kutoka Nepal walifanikiwa kufika kilele cha Mlima Everest, ambao ni mlima mrefu zaidi duniani. Mlima wa Everest wenye urefu wa mita 8,848, ni kilele kirefu zaidi cha silsila ya milima ya Himalaya nchini Nepal. Baada ya Hillary na Norgay kufanikiwa kupanda mlima huo mwaka 1953, makundi mengine ya wapanda milima kutoka katika nchi nyingine duniani pia yaliweza kukwea kilele cha mlima huo katika miaka iliyofuata.