May 29, 2020 23:53 UTC
  • Jumamosi, 30 Mei, 2020

Leo ni Jumamosi tarehe 7 Mfunguo Mosi Shawwal 1441 Hijria mwafaka na tarehe 30 Mei 2020 Milaadia.

Siku kama hii ya leo miaka 1438 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, kulipiganwa vita vya Uhud kando kando ya mlima wenye jina hilo kaskazini mwa mji wa Madina, kati ya Waislamu na Washirikina. Baada ya washirikina wa Kiquraishi kushindwa vibaya na Waislamu katika vita vya Badr walianzisha vita hivi vya Uhud kwa kuandaa jeshi la watu 3,000 waliokuwa na zana kamili kwa ajili ya vita hivyo, huku wapiganaji wa Kiislamu wakuwa 700 tu. Kabla ya kuanza kwa vita hivyo, Mtukufu Mtume Muhammad (s.a.w) aliwashauri masahaba zake juu ya namna atakavyopambana na Maquraishi na iliamuliwa kuwa vita hivyo vipiganwe nje ya mji wa Madina. mwanzoni mwa vita hivyo, Waislamu walionekana kushinda, hata hivyo kufuatia kughafilika na baadhi yao kuasi amri ya Mtume (saw) aliyewataka kuendelea kubakia mlimani, Waislanu hao walishuka mlimani kwa tamaa za kupata ngawira hali iliyowafanya washirikina kuwashambulia Waislamu na kudhoofika nguvu na uwezo wao. Waislamu 70 waliuawa shahidi katika vita hivyo akiwemo Hamza ami yake Mtume (s.a.w). Hata hivyo washirikina hawakuweza kupata ushindi wa moja kwa moja na hivyo wakalazimika kurejea Makka.***

Vita vya Uhud

 

Katika siku kama ya leo miaka 1135 (kwa mujibu wa baadhi ya vyanzo vya historia) alifariki dunia Ahmad bin Hiihani msomi wa Kiirani. Jiihani alikuwa msomi, mwanasiasa na mtaalamu mashuhuri wa Kiirani elimu ya Jiografia. Alipata umashuhuri katika ulimwengu wa Kiislamu kutokana na utafiti mkubwa na wenye thamani alioufanya. Moja ya vitabu vyake mashuhuri katika elimu ya jiografia kinaitwa: Al-msaalik wal-Mamamalik.***

Ahmad bin Hiihani

 

Miaka 242 iliyopita katika siku kama  ya leo, Francois - Marie Arouet maarufu kwa jina la Voltaire, mwanafalsafa na mwandishi wa Kifaransa alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 84. Katika maisha yake, Voltaire aliwahi kuwekwa mahabusu mara mbili na kubaidishwa kwa muda wa miaka mitatu nchini Uingereza. Kitendo hicho kilimkasirisha sana Voltaire na kumfanya kuwa dhidi ya utawala wa Ufaransa. ***

Francois - Marie Arouet

 

Miaka 48 iliyopita inayosadifiana na tarehe 7 Shawwal 1393 Hijria, alifariki dunia Ayatullah Mirza Abul Hussein Sha'rani mfasiri wa Qurani Tukufu inayojulikana kwa jina la 'Manhaj Swadiqiin', akiwa na umri wa miaka 73. Msomi huyo licha ya kubobea katika elimu za kidini alikuwa mahiri katika kuzungumza lugha za kigeni kama vile Kifaransa, Kiingereza na Kiarabu. Licha ya kuonyesha uwezo wake katika tafsiri ya Qurani Tukufu ya Manhaj Swadiqiin yenye juzuu 10 vilevile ameandika kitabu cha Sharh Kifayatil - Usuul.

Ayatullah Mirza Abul Hussein Sha'rani

 

Siku kama ya leo miaka 39 iliyopita, aliuawa Zia ur Rahman Rais wa Bangladesh baada ya kupigwa risasi katika mji wa Chittagong ulioko kusini mashariki mwa nchi hiyo. Rais Zia ur Rahman aliuawa baada ya kuchungulia dirishani kwenye nyumba ya wageni ya serikali katika mji huo. Watu wanane waliuawa kwenye shambulio hilo, wakiwemo wasaidizi na walinzi wa rais huyo. ***

Zia ur Rahman

Na katika siku kama ya leo miaka 28 iliyopita, Dakta Jalal Samimi mtafiti na mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Ufundi cha San'at Sharif cha mjini Tehran alifanikiwa kugundua vyanzo vitano vya mionzi ya Gamma katika mzunguko wa kundi la sayari na nyota au Milky Way Gallaxy, baada ya kufanya utafiti na majaribio kwa miaka 20 katika uwanja huo. Inafaa kukumbusha hapa kuwa Dakta Samimi alizaliwa mwaka 1319 Hijiria Shamsia katika mji wa Zabol kusini mashariki mwa Iran na kuhitimu daraja ya udaktari katika somo la Fizikia. Dakta Jalal Samimi alifanikiwa katika ugunduzi huo muhimu baada ya kutwalii na kufanya uchunguzi wa kina na majaribio mengi kuhusiana na Nuclear Emulsion.

Dakta Jalal Samimi