May 30, 2020 21:53 UTC
  • Jumapili, tarehe 31 Mei, 2020

Leo ni Jumapili tarehe 8 Shawwal 1441 Hijria, inayosadifiana na tarehe 31 Mei mwaka 2020 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1491 iliyopita, sawa na tarehe 31 Mei 529, dini ya Ukristo ilitambuliwa rasmi huko Roma kwa amri ya Constantine, mfalme wa wakati huo wa Roma. Kabla ya hapo Wakristo walikuwa wakifanya ibada kwa siri huko Roma. Mwaka 324 Miladia Mfalme Constantine aliamua kuhamia mji wa Byzantine, mji ambao alikuwa ameutangaza kama mji mkuu wa ufalme wake na uliojengwa na Wagiriki yapata karne nane kabla ya kuzaliwa Nabii Isa (as). Miaka sita baadaye na baada ya kuhamia huko mfalme huyo, ndipo dini ya Ukristo ikatangazwa na kutambuliwa rasmi huku wafuasi wake wakiruhusiwa kuabudu kwa uhuru. 

Picha ya mchoro unaonasibishwa na Nabii Issa (as)

Siku kama ya leo miaka 1069 iliyopita, sawa na tarehe 8 Shawwaal mwaka 372 Hijiria, alifariki dunia Adud al-Dawla, mfalme wa pili wa silsila ya Diyalameh wa Fursi. Adud al-Dawla alikuwa mrithi wa Imad Daulah Dailami ambaye katika kipindi cha utawala wake alitawala maeneo mapana ya Iran, Iraq na mashariki mwa Uturuki. Aidha alianzisha pia majengo mengi katika maeneo mengi ya Iraq na Ufursi. Adud al-Dawla alifariki dunia katika siku kama ya leo kutokana na maradhi na akizikwa kando na haramu ya Imam Ali Bin Abi Twalib mjini Najaf, Iraq.

Adud al-Dawla

Siku kama ya leo, miaka 188 iliyopita, yaani tareh 31 Mei mwaka 1832 miladia aliuawa Évariste Galois, mtaalamu mwenye kipawa cha hesabati wa Ufaransa.  Évariste Galois alizaliwa katika mji wa Bourg-la-Reine karibu na mji mkuu wa nchi hiyo, Paris. Hadi kufikia umri wa miaka 12, Galois hakuwa na mwalimu mwengine zaidi ya mama yake. Kuanzia rika la uchipukizi alianza kusoma vitabu vya kiwango cha juu mno vya hesabati na hivyo kuinukia kielimu. Baada ya hapo alijiunga na chuo, ambapo alikuwa akishika nafasi ya kwanza darasani katika kila somo. Baadaye Évariste Galois alianza kutalii elimu ya hisabati. Akiwa na umri wa miaka 18 alikamilisha kazi ya uandishi wa kitabu cha ukweli wa hisabati na baada ya hapo akaandika vitabu vitatu vipya katika taaluma hiyo na kujipatia umashuhuri mkubwa. Galois aliuawa akiwa na umri wa miaka 21 hapo tarehe 29 mwezi Mei mwaka 1832 Miladia, baada ya kutiwa jela wakati wa harakati zake za kisiasa nchini Ufaransa. Weledi wanaamini kuwa, kama Galois hangeuawa mapema, basi angepiga hatua kubwa katika uga wa hisabati duniani.

Évariste Galois

Siku kama ya leo miaka 117 iliyopita, yaani sawa na tarehe 8 Shawwal mwaka 1324 Hijria toleo la kwanza la gazeti la 'Majlis' lichapishwa nchini Iran. Gazeti hilo lilianzishwa na mtu aliyejulikana kwa jina la Mirza Sayyid Muhammad Sadiq Tabatabai. Mbali na gazeti hilo kuandika habari za ndani na nje ya nchi, liliakisi pia mazungumzo yote ya Majlisi ya Ushauri ya Iran yaani Bunge.

Gazeti la 'Majlis'

Na siku kama ya leo miaka 110 iliyopita, yaani tarehe 31 Mei mwaka 1910 Miladia, nchi ya Afrika Kusini iliundwa katika eneo la kusini mwa Afrika kwa kuunganishwa makoloni mawili ya Uingereza na kupewa uhuru. Muungano huo ulipata uhuru kamili mwaka 1931. Hata hivyo hatamu za madaraka ya nchi ziliingia mikononi mwa wazungu wachache. Lakini hatimaye baada ya mapambano makali ya waafrika kusini wazalendo wakiongozwa na shujaa Nelson Mandela, mnamo mwaka 1991 wazungu makaburu walilazimika kuhatimisha mfumo wa ubaguzi wa rangi wa Apartheid katika nchi hiyo.

Bendera ya Afrika Kusini