May 31, 2020 23:59 UTC
  • Jumatatu tarehe Mosi Juni 2020

Leo ni Jumatatu tarehe 9 Shawwal 1441 Hijria sawa na tarehe Mosi Juni mwaka 2020.

Siku kama ya leo miaka 1328 iliyopita katika siku kama ya leo, Ibn Sirin mpokezi wa hadithi na faqihi mashuhuri wa karne ya pili Hijria aliaga dunia. Ibn Sirin alizaliwa Basra kusini mwa Iraq. Msomi huyo wa Kiislamu alitoa umuhimu mkubwa kwa hadithi za Mtume Muhammad SAW na alikuwa mahiri katika kuhifadhi na kunukuu hadithi. Alikutana na masahaba 30 wa Mtume Muhammad (saw). Ibn Sirin ameacha vitabu na makala nyingi zilizoandikwa kwa lugha mbalimbali. Kutokana na hali hiyo wataalamu wengi wa hadithi wanatilia maanani sana hadithi zilizopokelewa na Ibn Sirin. 

Hii leo vitabu mbalimbali na kwa lugha tofauti vimeandikwa kutoka kwa msomi huyo. Ibn Sirin anafahamika pia kwa uhodari wake wa kufasiri ndoto.

Siku kama ya leo tarehe Mosi Juni miaka 68 iliyopita, aliaga dunia John Dewey, msomi na mwandishi mashuhuri wa Marekani. Dewey alikuwa amebobea mno katika taaluma ya elimu na malezi na alijifunza mengi alipokuwa katika chuo kikuu cha Colombia. John Dewey alifanikiwa kuandika vitabu vingi kuhusiana na elimu na malezi. Miongoni mwa vitabu mashuhuri vya msomi huyo ni pamoja na "How we Think", "The Public and its Problems" na "Freedom and Culture." John Dewey alifariki dunia mwaka 1952 akiwa na umri wa miaka 93.

John Dewey

Siku kama ya leo Miaka 50 iliyopita, Ayatullah Sayyid Muhsin Hakim, mkuu wa kituo cha kidini cha Najaf aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 92. Baada ya kuaga dunia Ayatullah Burujerdi ambaye alikuwa mar'ja' mashuhuri katika ulimwengu wa Kiislamu, Ayatulah Hakim alichukua nafasi yake na kufuatwa na Waislamu wengi na hasa wa Iraq, kuhusiana na masuala ya kifik'hi. Alipambana vikali na kila kundi au watu waliojaribu kuharibu jina la Uislamu. Fatua yake mashuhuri ya kupinga fikra ya ukomunisti dhidi ya mafundisho ya dini ilileta mabadiliko makubwa nchin Iraq. Fatua hiyo pia ilimpelekea kutoa amri ya kupigana jihadi dhidi ya utawala haramu wa Israel. Ujenzi wa maktaba, shule na vituo vya kidini na kiutamaduni pamoja na uandishi wa vitabu kama vile Mustamsak Urwat al-Wuthqah na Nahjul Faqaha ni miongoni mwa vitabu mashuhuri vilivyoandikwa na mwanazuoni huyo mashuhuri wa Kiislamu.

Ayatullah Sayyid Muhsin Hakim

Na miaka 20 iliyopita katika siku kama ya leo,  sawa na tarehe 12 Khordad mwaka 1379 Hijiria Shamsia, aliaga dunia Hujjatul Islam Sayyid Ali Akbar Abuturabi, akiyekuwa mwanzuoni na mwanaharakati wa Iran katika ajali ya gari akiwa pamoja na baba yake, Ayatullah Sayyid Abbas Abuturabi. Hujjatul Islam Sayyid Ali Akbar Abuturabi alizaliwa mwaka 1318, kwa mujibu wa kalenda ya Iran, katika mji wa kidini wa Qum. Alijifunza elimu ya dini kutoka kwa maulama wakubwa akiwemo Imam Ruhullah Khomeini (M.A).  Katika mapambano ya kabla ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu Hujjatul Islam Abuturabi alikamatwa mara kadhaa na kuteswa na vibaraka wa Shah. Wakati vya vita vya Iran na Iraq mwaka 1359 mwanaharakati huyo alikamatwa mateka na askari wa utawala wa Baath wa Iraq na kufungwa kwa kipindi cha miaka 10 katika jela zenye mateso makali za Iraq. alistahamili mateso makubwa ya utawala wa Saddam kiasi cha kuwa mashuhuri miongoni mwa mateka wa Iran kwenye jela hizo. Baada ya kuachiwa huru na kurejea nchini aliteuliwa kuwa mwakilishi wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika masuala ya mateka na walioachiliwa huru.

Sayyid Ali Akbar Abuturabi