Jumatano, tarehe 3 Juni, 2020
Leo ni Jumatano tarehe 11 Shawwal 1441 hijria sawa na tarehe 3 Juni 2020 Miladia.
Tarehe 11 Shawwal miaka 1444 iliyopita Mtume Muhammad (S.A.W) alielekea katika mji wa Twaif karibu na Makka kwa lengo la kuwalingania Uislamu watu wa kabila la Thaqif. Safari hiyo ya Mtume mtukufu ilifanyika katika kipindi ambacho alikuwa ameondokewa na ami yake na mlezi wake kipenzi Abu Twalib, jambo lililowafanya Maquraishi wa Makka wazidishe maudhi na manyanyaso dhidi ya Mtume Muhammad (S.A.W) na wafuasi wake. Hivyo ilitarajiwa kuwa, iwapo wakazi wa Twaif wangekubali Uislamu, mji huo ungeweza kuwa kituo na makazi salama kwa Waislamu waliokuwa wakidhulumiwa wa Makka. Hata hivyo viongozi wa kabila la Thaqif sio tu kwamba hawakumwamini Mwenyezi Mungu Mmoja na risala ya Mtume Muhammad (S.A.W), bali pia baadhi ya watu wa kabila hilo walimfanyia maudhi, dhihaka na kumjeruhi Mtume mtukufu.
Miaka 518 iliyopita siku kama ya leo, Vasco da Gama baharia wa Kireno alifanya mauaji ya umati huko Calicut, mji ambao hivi sasa imepewa jina la Kozhikode, ni bandari iliyoko huko Madras kusini mwa India. Bandari hiyo ilikuwa eneo la kwanza alipofikia baharia Vasco da Gama mwaka 1498 Miladia na baadaye kulikalia kwa mabavu eneo hilo. Vasco da Gama kama walivyo wakoloni wengine, alidai kuwa mmiliki halisi wa India. Vasco da Gama alitoa amri ya kukatwa, masikio na pua za mabaharia wa Kiarabu wakati walipowasili katika bandari ya Calicut kwa jili ya kufanya biashara ya mchele. Pia aliwauwa kwa umati wafanyabiashara hao wa Kiarabu baada ya kuzichoma moto meli zao.
Miaka 353 iliyopita sawa na leo, kwa mara ya kwanza katika historia ya tiba na upasuaji, kitendo cha kuongezwa damu katika mwili wa binadamu kilifanyika. Damu hiyo iliwekwa kwa mwanadamu na tabibu wa Kifaransa aliyeitwa Jean Bapitiste Denis. Utiaji damu huo kwa wagonjwa, ulihesabiwa kuwa tukio na mafanikio makubwa katika sayansi ya tiba. Hii ni kwa sababu zama hizo wagonjwa wengi walipoteza maisha yao kutokana na kuvuja damu nyingi na ukosefu wa damu. Katika jaribio lake la kwanza, tabibu huyo wa Kifaransa alichukua damu ya kondoo na kuitia katika mwili wa mwanadamu, na baadaye akawa akiwaongeza wagonjwa damu ya wanadamu.
Miaka 57 iliyopita inayosadifiana na leo yaani tarehe Tatu mwezi Juni mwaka 1963 alifariki dunia Nazim Hikmat malenga mashuhuri wa Kituruki. Alizaliwa mwaka 1902 na kuanza kutunga mashairi akiwa na umri wa miaka 12. Malenga huyo wa Kituruki alijiunga na jeshi la nchi hiyo baada ya kuhitimu masomo yake ya shule ya upili. Lakini mwaka 1920, Nazim Hikmat alijiondoa jeshini kutokana na misimamo yake ya kisiasa. Kisha alielekea Moscow mji mkuu wa Urusi ya zamani kwa ajili ya kuendelea na masomo yake na baadaye akarejea Uturuki baada ya kumaliza masomo ya chuo kikuu katika fani ya uchumi wa kisiasa. Baada ya hapo, Nazim Hikmat akaanza kutunga mashairi ya kimapinduzi dhidi ya ufashisti, yaliyokuwa yakiukosoa utawala wa kidikteta wa Ataturk, rais wa kwanza wa Uturuki.
Siku kama ya leo miaka 31 iliyopita, sawa na tarehe 14 Khordad mwaka 1368 kwa mujibu wa kalenda ya Hijria Shamsia sawa na tarehe 4 Juni 1989 Milaadia, Imam Ruhullah Musawi Khomeini (M.A) Muasisi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran aliaga dunia baada ya kuishi kwa miaka 87 katika umri uliojaa juhudi zisizo na kikomo. Kwa kutangazwa kifo cha Imam ulimwengu wa Kiislamu uligubikwa na majonzi na huzuni kubwa. Imam Khomeini (M.A) alizaliwa tarehe Mosi mwezi wa Mehr mwaka 1281 Hijiria Shamsia sawa na tarehe 24 Septemba 1902 Milaadia katika mji wa Khomein ulioko katikati mwa Iran. Alianza kujishughulisha na siasa sambamba na masuala ya kielimu na kiutamaduni. Mapambano ya Imam dhidi ya utawala wa Shah na uingiliaji wa Marekani nchini Iran yalishtadi mwaka 1963 Milaadia sawa na 1342 kwa mujibu wa kalenda ya Hijria Shamsia, na kupelekea Imam kubaidishwa kwa miaka 13 nchini Iraq, Uturuki na Ufaransa. Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yalipata ushindi mwaka 1357 Hijiria Shamsia sawa na tarehe 1979 Milaadia kwa uongozi shupavu wa Imam Khomeini (M.A). Aidha Imam alibobea katika elimu ya dini na mbali na kuwasomesha wanafunzi wengi na kutoa hotuba nyingi za kihistoria, aliandika pia vitabu. Miongoni mwa vitabu vyake tunavyoweza kuashiria hapa ni Tahrirul Wasilah, Kashful Asrar, Misbahul Huda, na Utawala wa Kiislamu na Wilayatul Faqih. Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran inatoa salamu za rambi rambi kwa mnasaba huu wa kukumbuka wakati Imam Khomeini aliporejea kwa Mola wake.

Siku kama ya leo miaka 31 iliyopita inayosadifiana na tarehe 4 Khordad mwaka 1368 kwa mujibu wa kalenda ya Kiirani, Baraza la Wanazuoni Wataalamu wanaomchagua Kiongozi Muadhamu walimchagua Ayatullah Sayyid Ali Khamenei kuwa Kiongozi Muadhamu wa Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Uchaguzi huo ulifanyika masaa machache tu baada ya kufariki dunia Imam Khomeini (M.A) ambapo wasia wa Imam ulisomwa pia mbele ya hadhirina. Hadi sasa Ayatullah Khamenei anaendeleza njia ya Imam Khomeini MA kwa msingi wa mafundisho ya Kiislamu na ameyaongoza Mapinduzi ya Kiislamu kwa hekima, tadbiri, uono wa mbali na ustahiki.
