Jun 07, 2020 22:03 UTC
  • Jumatatu, Juni 8, 2020

Leo ni Jumatatu tarehe 16 Mfunguo Mosi Shawwal 1441 Hijria sana wa Juni 8 mwaka 2020 Milaadia.

Siku kama ya leo miaka 28 iliyopita, shirika la ujasusi la utawala haramu wa Israel, Mossad, lilifanya mauaji ya kigaidi dhidi ya kiongozi mwingine wa Kipalestina katika moja ya nchi za kigeni. Siku hiyo maajenti wa Mossad walimuuwa Atef Bseiso aliyekuwa mmoja kati ya viongozi wa usalama wa Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) huko Paris, Ufaransa. Licha ya kwamba hakukuwepo shaka juu ya kuhusika utawala wa Kizayuni katika mauaji hayo, lakini utawala huo ghasibu ulikana kufanya jinai hiyo ya kinyama kwa kuhofia hasira za walimwengu. Hata hivyo miaka saba baadaye, polisi ya Ufaransa ilitangaza kwamba shirika hilo la ujasusi la Israel ndilo lililopanga na kutekeleza mauaji hayo.

Atef Bseiso

Siku kama ya leo miaka 52 iliyopita, alifariki dunia Ayatullah Sayyid Muhammad Hassan Ilahi Tabatabai, mmoja wa maulamaa na wataalamu wa elimu ya irfani. Sayyid Muhammad Tabatabai alizaliwa Tabrizi huko kaskazini mwa Iran mwaka 1325 Hijiria. Akiwa na miaka 19 alielekea  Najaf, Iraq akiwa na kaka yake mkubwa, Allamah Muhammad Hassein Tabatabai na kusoma elimu ya dini mjini hapo. Baada ya kutabahari katika elimu za Kiislamu alirejea eneo alikozaliwa la Tabriz na kujishughulisha na malezi na kutoa elimu kwa wanafunzi. Mwanazuoni huyo ameandika vitabu kadhaa kikiwemo kile cha Uhusiano wa Kimaanawi Baina ya Roho na Sauti.  

Ayatullah Sayyid Muhammad Hassan Ilahi Tabatabai

Tarehe 8 Juni miaka 165 iliyopita, mji wa Lisbon ambao ni mji mkuu wa Ureno uliharibika kutokana na mtetemeko mkubwa wa ardhi na moto uliosababishwa na zilzala hiyo. Karibu wakazi elfu arubaini wa mji huo walipoteza maisha yao na theluthi mbili ya nyumba na taasisi za kiuchumi za mji huo zilibomolewa. Mbali na maafa hayo, karibu meli elfu mbili, boti na ngalawa nyingi zilizokuwa katika bandari za Ureno zilizama. Mtetemeko huo ni moja ya mitetemeko mikubwa zaidi kuwahi kuikumba Ureno.

Siku kama ya leo miaka 190 iliyopita inayosadiafiana na tarehe 8 Juni 1830, Camberz mbunifu wa Kijerumani alivumbua utengenezaji wa kiberiti. Tofauti kubwa ya kiberiti hicho cha awali na hiki kinachotumiwa hivi sasa, ni uwakaji wake uliokuwa ukiwaka taratibu. Baada ya Camberz walijitokeza watafiti wengine kadhaa waliofanya utafiti kuhusiana na kiberiti na hatimaye Phillips raia wa Kimarekani alifanikiwa kutengeneza kiberiti kama hiki ambacho kinatumika hii leo.