Jumanne, Juni 9, 2020
Leo ni Jumanne tarehe 17 Mfunguo Mosi Shawwal 1441 Hijria inayosadifiana na tarehe 9 Juni mwaka 2020 Milaadia.
Siku kama ya leo miaka 1952 iliyopita Nero, mfalme katili na mmwagaji damu wa Roma alijiua akiwa na umri wa miaka 31 na baada ya kutawala kwa miaka 14. Inasemekana kuwa Claudius wa Kwanza wa Roma alimchukua Nero na kumfanya mwanaye. Hata hivyo Nero alimuua kwa sumu na baadaye kuchukua nafasi yake ya ufalme. Katika kipindi chote cha utawala wake, Nero aliweza kuwaua ndugu na jamaa zake akiwemo mama, mke na kaka yake. Mfalme huyo katili wa Roma alifanya mauaji makubwa dhidi ya wananchi sambamba na kuwauwa kwa halaiki Wakristo na pia kuuchoma moto mji huo wa Roma. Kwa sababu hiyo kulijitokeza harakati za uasi dhidi yake. Mtawala huyo katili na dhalimu aliamua kujinyonga baada ya kuona harakati za mwisho za uasi dhidi yake zinakaribia kupata ushindi.
Siku kama ya leo miaka 246 iliyopita alizaliwa Joseph von Hammer, mtaalamu wa masuala ya mashariki ya duni wa Austria. Baada ya kujifunza lugha za Kiarabu, Kifarsi na Kituruki aliteuliwa na serikali ya Austria kuwa mfasiri wa ubalozi wa serikali hiyo katika utawala wa Othmania. Ni katika wakati huo ndipo Joseph von Hammer akatumia fursa iliyojitokeza kwa ajili ya kufuatilia masuala ya utamaduni ya nchi za Iran, Russia, Syria, Lebanon na Misri, kama ambavyo pia alijifunza mafunzo ya dini ya Kiislamu. Kutokana na juhudi zake kubwa za kutambua tamadunia za nchi za Mashariki, alitunukiwa zawadi mbalimbali barani Ulaya. Baadhi ya sentesi na maandishi yake yanaonyesha kwamba Hammer alijiunga na dini ya Uislamu ambapo hata jiwe alilolichonga mwenyewe kwa ajili ya kuwekwa juu ya kaburi lake liliandikwa aya kadhaa za Qur'ani Tukufu. Miongoni mwa athari muhimu za Joseph von Hammer ni pamoja na kitabu cha 'Historia ya utawala wa Othmania' 'Picha za watawala Waislamu' na 'Historia ya Malenga wa Othmania.' Joseph von Hammer alifariki dunia mwaka 1856 Miladia.
Miaka 135 iliyopita muwafaka na siku hii ya leo, jeshi la Ujerumani lilivamia ardhi ya Togo huko magharibi mwa Afrika. Wakati huo maeneo ya pwani ya Togo yalikuwa sehemu bora kwa watu wa Ulaya kwa ajili ya biashara ya utumwa. Ni kwa sababu hiyo ndiyo maana Togo imekuwa maarufu kwa jina la "Pwani ya Utumwa." Wakoloni wa Ujerumani waliendelea kuikalia kwa mabavu ardhi ya Togo hadi wakati wa Vita vya Kwanza vya Dunia. Baada ya hapo Togo ilikoloniwa na Wafaransa na Waingereza. Nchi hiyo ilipata uhuru mwaka 1960.
Siku kama ya leo miaka 58 iliyopita moto mkubwa ulitokea katika Chuo Kikuu cha Algiers mji mkuu wa Algeria. Moto huo ulichoma zaidi ya nakala laki tano za vitabu vyenye thamani kubwa zilizokuwa kwenye maktaba ya chuo hicho. Asilimia kubwa ya vitabu vilivyoungua vilikuwa miongoni mwa marejeo muhimu na nadra. Chuo Kikuu cha Algiers na maktaba yake vilichomwa moto na jeshi la siri la Ufaransa nchini Algeria. Jeshi hilo la siri liliundwa na askari wa Ufaransa waliokuwa wakipinga suala la kupewa uhuru Algeria. Moto huo ulikuwa miongoni mwa makumi ya mioto iliyotokea katika siku hiyo nchini Algeria na mingi ilisababishwa na jeshi la siri la Ufaransa.
Siku kama ya leo miaka 50 iliyopita, aliuawa shahidi Ayatullah Sayyid Muhammad Reza Saeedi, mmoja wa wasomi wakubwa na wanamapambano wa Iran baada ya kuteswa kwa muda mrefu katika jela za utawala wa kitwaghuti wa Shah. Alielekea Qum na kujiunga na hawza ya kielimu kwa ajili ya kujifunza elimu ya dini ya Kiislamu ambapo akiwa mjini hapo alipata kusoma kwa maulama wakubwa akiwemo Ayatullahil-Udhma Borujerdi na Imamu Khomein (MA). Baada ya mwamko wa mapinduzi ya wananchi Waislamu nchini Iran, tarehe 15 Khordad 1342 Hijiria, alishadidisha harakati zake dhidi ya utawala wa kidikteta wa Shah. Katika uwanja huo, Ayatullah Sayyid Muhammad Reza Saeedi aliufanya msikiti wake kuwa ngome katika kuwafungua wananchi hususan vijana upeo wao ambapo hotuba zake nyingi zilijikita katika kufichua njama chafu za ukoloni na jinai za utawala haramu wa Kizayuni dhidi ya raia madhlumu wa Palestina. Ni kwa ajili hiyo ndio maana alikamatwa mara kadhaa na kufungwa jela huku akiteswa vikali. Hata hivyo vitendo hivyo vya utawala wa Shah havikuweza kuathiri hata kidogo azma ya mwanazuoni huyo mtajika wa Kiislamu. Miongoni mwa athari za Ayatullah Sayyid Muhammad Reza Saeedi ni pamoja na kitabu cha ‘Umoja wa Kiislamu’ ‘Uhuru wa Mwanamke’ na ‘Kazi na Uislamu.’
Katika siku kama ya leo miaka 39 iliyopita, Bani Sadr Rais wa kwanza wa Iran baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu aliuzuliwa wadhifa wa Amiri Jeshi Mkuu wa majeshi yote kutokana kufanya hiyana na usaliti. Tangu awali baada ya kuchaguliwa kuwa Rais, Bani Sadr alikumbwa na kiburi na ghururi sana na akawa anafuatilia suala la kuviweka kando vikosi vya mapinduzi vilivyokuwa vitiifu kwa Imam Khomeini, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu. Aidha Bani Sadr alikuwa akishirikiana na makundi yaliyokuwa yakipinga Mapinduzi ya Kiislamu. Bani Sadr alikwamisha utendaji wa serikali kutokana na kukwepa kwake kumkubali Waziri Mkuu Muhammad Rajai mmoja wa wanamapambano mashuhuri aliyekuwa amechaguliwa na Bunge kwa wingi wa kura. Ukwamishaji huo wa Bani Sard ulifikia kilele katika vita vya kichokozi vya Iraq dhidi ya Iran na kupelekea miji mingi ya Iran katika kipindi hicho cha vita kukaliwa kwa mabavu na utawala wa dikteta Saddam Hussein. Hatimaye katika siku kama ya leo, Imam Khomeini alimuuzulu Bani Sadr cheo cha Amiri Jeshi Mkuu. Siku chache baadaye Bunge lilipasisha kwa wingi wa kura mpango kutokuwa na imani na uwezo wa kisiasa Rais huyo.