Jun 11, 2020 00:03 UTC
  • Alkhamisi tarehe 11 Juni 2020

Leo ni Alkhamisi tarehe 19 Shawwal 1441 Hijria sawa na Juni 11 mwaka 2020.

Siku kama ya leo miaka 1007 yaani tarehe 19 Shawwal 434 iliyopita alizaliwa Abu Zakaria Yahya bin Muhammad mashuhuri kwa jina la Ibn Mandeh ambaye alikuwa mwanahadithi, faqihi na mwanahistoria wa Kiirani. Alikuwa wa mwisho katika kizazi cha Ibn Mandeh na baada ya kupata elimu za zama zake alianza kufunza na kuandika vitabu. Mwanahistoria huyo wa Kiislamu ameandika vitabu vingi kikiwemo kile cha Maisha ya Tabarani.

Katika siku kama ya leo miaka 448 iliyopita sawa na tarehe 11 Juni mwaka 1572, alizaliwa Benjamin Jonson mshairi na mwandishi wa filamu wa Uingereza. Jonson kwa muda mrefu alikuwa mcheza tamthilia na alikuwa rafiki wa Shakespare mwandishi maarufu wa Uingereza, ambapo urafiki wao ulikuwa na athari kubwa katika kukamilisha fasihi ya mshairi huyo. Baadhi ya athari zilizoachwa na Benjamin Jonson ni Mwanamke Aliyezimwa' pamoja na Historia ya Dunia. Malenga huyo Muingereza alifariki dunia mwaka 1637.

Benjamin Jonson

Siku kama ya leo miaka 165 iliyopita inayosadifiana na tarehe 11 Juni mwaka 1855, mwanga wa jua ulitambuliwa kwa kutumiwa njia za taaluma ya uchanganuzi na wigo wa rangi. Jaribio hilo lilifanywa kwa mara ya kwanza katika historia ya utafiti mpya wa fizikia na wanasayansi wawili wa Ujerumani walioitwa Kirchhoff na Bunsen. Si vibaya kuashiria hapa kwamba, mionzi ya jua katika hewa wakati wa mvua pamoja na kutokea upinde wa mvua wenye rangi mbalimbali, ni tukio la kuvutia ambalo linasababishwa na kuchanganuliwa nuru ya jua na matone ya maji mawinguni. Hata hivyo suala hilo mwanzoni lilifafanuliwa na wanasayansi wa Kiislamu kama vile Ibn Sina, Ibn Hisham na Qatwibidin Shirazi na baadaye kuthibitishwa na Kirchhoff na Bunsen.

Miaka 25 iliyopita katika siku kama ya leo, aliaga dunia Sheikh Muhammad Ghazali mwanazuoni na mwanamageuzi mkubwa wa Misri. Alizaliwa mwaka 1917 huko nchini Misri. Akiwa na umri wa miaka 10 tu, tayari Muhammad Ghazali alikuwa amehifadhi Qur'ani Tukufu yote. Muhammad Ghazali alihitimu Chuo Kikuu akiwa na umri wa miaka 24. Fikra zake zilijengeka juu ya msingi wa mageuzi ya maarifa ya kidini, kukurubisha baina ya madhehebu za Kiislamu na kupinga fikra za kikaumu. Muhammad Ghazali aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 79 kwa mshtuko wa moyo na kuuzikwa katika makaburi ya Baqii mjini Madina. 

Sheikh Muhammad Ghazali