Ijumaa tarehe 12 Juni 2020
Leo nii Ijumaa tarehe 20 Shawwal 1441 Hijria sawa na Juni 12 mwaka 2020.
Siku kama ya leo miaka 624 iliyopita mtaalamu wa lugha na mwandishi mashuhuri wa zama hizo Majduddin Abu Tahir Muhammad Yaaqub Firuzabadi aliaga dunia. Firuzabadi alikuwa pia hodari katika taaluma za Hadithi na tafsiri ya Qur'ani na ameandika vitabu kadhaa katika taaluma hizo. Hata hivyo kitabu mashuhuri zaidi cha mwanazuoni huyo ni "al Qamus" ambacho ni miongoni mwa kamusi muhimu za lugha ya Kiarabu. Vitabu vingine mashuhuri vya mwanazuoni huyo wa Kiislamu ni "Sifrul Saada" na "Tanwirul Miqyas".

Tarehe 12 Juni miaka 480 iliyopita nchi ya Chile iliyoko magharibi mwa Amerika ya Kusini ilitekwa na wakoloni wa Hispania. Kabla ya hapo Wahindi Wekundu wa Chile walikuwa wamevunja hujuma na mashambulio kadhaa ya Wahispania waliokusudia kuteka na kukalia kwa mabavu ardhi yao. Hata hivyo, hata baada ya kutekwa nchi yao, Wahindi Wekundu hao waliendeleza mapambano dhidi ya wakoloni hadi pale José Francisco de San Martín jenerali wa Argentina alipowasili mwaka 1817 na kuanzisha mashambulio ya kuzikomboa nchi zote zilizokuwa chini ya ukoloni wa Hispania Kusini mwa Amerika, ikiwemo Chile. Kwa msingi huo, Chile akakombolewa na kutangaza uhuru wake mwaka 1818.
Tarehe 12 Juni 1914, kwa mara ya kwanza kabisa yalifanyika majaribio ya kutumia nishati ya joto la jua pambizoni mwa Cairo mji mkuu wa Misri. Mbunifu na mtekelezaji wa mpango huo alikuwa mwanafizikia wa Kijerumani, ambaye aliweza kukusanya miale ya jua na kufanikiwa kuwasha mashine ya mvuke yenye kutumia 'horse power' 50.
Siku kama ya leo miaka 56 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 12 Juni 1964, Nelson Mandela kiongozi wa mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini alihukumiwa kifungo cha maisha jela, baada ya kupatikana na hatia ya kufanya uhaini dhidi ya mfumo na utawala wa ubaguzi wa rangi, Apartheid nchini humo. Mandela alihukumiwa adhabu hiyo pamoja na wenzake saba akiwemo Walter Sisulu aliyekuwa Katibu Mkuu wa zamani wa chama cha African National Congress kilichokuwa kimepigwa marufuku nchini humo.
Katika siku kama ya leo miaka 40 iliyopita, inayosadifiana na 23 Khordad 1359 Hijria Shamsia, Imam Ruhullah Khomeini mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran akiwa na lengo la kufanya mabadiliko katika vyuo vikuu hapa nchini, alitoa amri ya kuasisiwa Baraza la Mapinduzi la Kiutamaduni. Katika ujumbe wake, Imam Khomeini MA aliwataka wajumbe wa baraza hilo kuratibu na kuandaa mipango na mitalaa katika kozi mbalimbali za vyuo vikuu inayokwenda sambamba na mafunzo ya utamaduni tajiri wa Kiislamu.
Siku kama ya leo miaka 37 iliyopita, yaani tarehe 23 Khordad 1362 Hijria Shamsia, Bi. Nusrat Amin faqihi na mfasiri mkubwa wa Qurani Tukufu alifariki dunia katika mji wa Esfahan ulioko katikati mwa Iran. Bi. Nusrat Amin aliutumia muda wake wote katika kuishughulikia Qurani Tukufu, na amefanikiwa kufasiri juzuu 15 za Qur'ani na kuandika vitabu kadhaa.