Jun 13, 2020 01:55 UTC
  • Jumamosi tarehe 13 Juni mwaka 2020

Leo ni Jumamosi tarehe 21 Shawwal 1441 Hijria sawa na tarehe 13 Juni mwaka 2020.

Miaka 1349 iliyopita katika siku inayosadifiana na ya leo, ardhi ya Andalusia huko Uhispania ya leo ilidhibitiwa na jeshi la Kiislamu lililoongozwa na Tariq bin Ziyad. Tariq ambaye alikuwa na wapiganaji karibu ya elfu 12, alivuka kwa boti mlango bahari ulioko kati ya Morocco na Uhispania ambao umepewa jina lake Tariq bin Ziad au "Gibraltar". Tariq bin Ziyad aliamuru kochomwa moto boti zote zilizotumiwa na wapiganaji wake kuvukia lango bahari na Gibralta ili kuwahamasisha zaidi kupigana na maadui. Katika kipindi cha karne 8 za utawala wao huko Andalusia, Waislamu walianzisha vituo mbalimbali vya utamaduni na taasisi za kiuchumi na kwa kipindi kirefu ardhi hiyo ilikuwa kituo kikuu cha ustaarabu wa Kiislamu barani Ulaya.

Tari bin Ziad

Miaka 1087 iliyopita mwafaka na siku hii ya leo, alifariki dunia Ibn Habban, mtaalamu wa hadithi, elimu ya fiq'hi na mwanahistoria mashuhuri wa karne ya 14 Hijiria. Alipata elimu ya msingi kwa walimu mashuhuri wa zama zake na kisha akaelekea Neishabur kaskazini mwa mashariki mwa Iran, ambao katika kipindi hicho ulikuwa ni moja ya vituo muhimu vya kielimu. Ibn Habban anahesabika kuwa mtu mwenye nadharia muhimu katika elimu ya hadithi. Miongoni mwa athari muhimu za msomi huyu mkubwa ni pamoja na kitabu cha"At-Thuqat" na Rawdhatul-Uqalaai wa Nazahatul-fudhalaai."

Siku kama ya leo miaka 99 iliyopita muwafaka na tarehe 13 Juni 1921 katika miaka ya mwanzo ya usimamizi wa Uingereza huko Palestina, ilianza harakati kubwa ya kwanza ya wananchi katika ardhi yote ya Palestina dhidi ya Wazayuni. Harakati ya wananchi hao wa Palestina ilibainisha upinzani wao dhidi ya siasa za kikoloni za Uingereza pamoja na uungaji mkono wa nchi hiyo kwa Wazayuni waliokuwa wakiishi Palestina. Katika fremu ya sera hizo za Uingereza mwaka 1923 kulikuwa na Wazayuni 35 elfu huko Palestina na kabla ya kuundwa utawala bandia wa Israel mwaka 1948 idadi hiyo ilikuwa zaidi ya laki sita.

Siku kama ya leo miaka 76 iliyopita sawa na tarehe 13 Juni mwaka 1944, kombora la kwanza la ardhi kwa ardhi la Ujerumani ya Kinazi lililojulikana kwa jina la V-1 lilishambulia ardhi ya Uingereza, katika Vita vya Pili vya Dunia. Kabla ya hapo Ujerumani ilikuwa ikiishambulia ardhi ya Uingereza kwa njia ya anga. Baada ya vita hivyo, nchi nyingine duniani zilitengeneza makombora ya aina hiyo kwa teknolojia ya kisasa zaidi.

Vita vya Kwanza vya Dunia

Na tarehe 24 Khordad miaka 39 iliyopita wawakilishi 120 wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran (Bunge) waliwasilisha muswada wa kutokuwa na imani na Bani Sadr aliyekuwa rais wa wakati huo wa Iran. Hatua hiyo ilichukuliwa baada ya kusambaratika mapambano ya wananchi dhidi ya wavamizi wa chama cha Baath kutoka Iraq katika hujuma iliyofanywa katika ardhi ya Iran kutokana na kukosa misaada ya dharura kutoka kwa Bani Sadr aliyekuwa Kamanda na Amri jeshi Mkuu, na vilevile hitilafu zilizojitokeza baina ya Rais wa nchi na mihimili mingine miwili ya dola.

Bani Sadr