Jun 17, 2020 02:47 UTC
  • Jumatano tarehe 17 Juni mwaka 2020

Leo ni Jumatano tarehe 25 Shawwal 1441 Hijria sawa na Juni 17 mwaka 2020.

Siku kama ya leo miaka 1293 iliyopita Imam Ja'far Sadiq mmoja kati ya wajukuu wa Mtume Mtukufu Muhammad SWA, aliuawa shahidi kwa amri ya mtawala dhalimu wa Kiabbasi, Mansur al Dawaniqi. Imam Sadiq alizaliwa mwaka 83 Hijria katika mji mtakatifu wa Madina. Alishika hatamu za kuongoza Umma wa Kiislamu akiwa na umri wa miaka 31 baada ya kuuawa shahidi baba yake, Imam Muhammad Baqir. Imam Sadiq ambaye kipindi cha uongozi wake kilisadifiana na zama za mapigano makali kati ya watawala wa Kiumawi na Kiabbasi, alitumia fursa hiyo kueneza elimu na maarifa sahihi ya Kiislamu. Alifanikiwa kulea na kutayarisha wasomi hodari katika taaluma mbalimbali kama tiba, kemia, hesabati, nujumu hadithi na kadhalika. Jabir bin Hayyan ambaye anatambuliwa hii leo kuwa ndiye baba wa elimu ya kemia alikuwa mwanafunzi wa Imam Ja'far Saqid (as). Ushawishi wa Imam ulienea kwa kasi katika ulimwengu wa Kiislamu, jambo ambalo halikuwafurahisha watawala wa Kiabbasi. Hatimaye mtawala Mansur al Dawaniqi aliamuru Imam apewe sumu. Mtukufu huyo aliuawa shahidi kwa sumu hiyo katika siku kama ya leo na akazikwa katika makaburi ya Baqii mjini Madina.

Miaka 444 iliyopita mwafaka na siku hii ya leo, yaani tarehe 17 Juni 1576, William Silent kiongozi wa harakati ya wananchi wa Holland dhidi ya Uhispania, alitangaza uhuru wa nchi hiyo. Harakati hiyo ilianza mwaka 1568 na iliandaa uwanja wa kuundwa nchi moja baada ya kuungana majimbo 8 ya Holland. Ingawa Holland ilitangazwa kuwa huru lakini wananchi wa nchi hiyo waliendelea kukandamizwa na wanajeshi wa Uhispania hadi mwaka 1609 yalipotiwa saini makubaliano ya amani kati ya viongozi wa Holland na mafalme wa Uhispania, na kutambua rasmi kujitawala kwa Holland. Nchi hiyo baada ya kujitawala taratibu ilianza kuzidhibiti na kuzikalia kwa mabavu nchi nyinginezo na ilipofika karne ya 17 Miladia Holland iliingia katika kundi la nchi zenye nguvu za Ulaya zilizozikoloni nchi nyinginezo.

Siku kama ya leo miaka 95 iliyopita sawa na tarehe 17 Juni 1925, ulitiwa saini mkataba wa kupiga marufuku matumizi ya silaha za vijidudu na kemikali mjini Geneva Uswisi. Kwa mujibu wa makubaliano hayo, utumiaji vitani wa aina yoyote ya silaha za vijidudu, gesi zinazoua, sumu za kemikali na nyinginezo kama hizo ulipigwa marufuku. Licha ya kufikiwa makubaliano hayo, lakini baadhi ya nchi bado ziliendelea kutumia silaha hizo zilizopigwa marufuku dunia. Ujerumani ilitumia silaha za kemikali katika Vita vya Kwanza vya Dunia, Marekani katika vita vya Vietnam na utawala wa zamani wa Iraq kutumia silaha hizo wakati wa vita vyake vya kichokozi dhidi ya Iran.

Siku kama ya leo miaka 76 iliyopita, wakazi wa kisiwa cha Iceland walifanikiwa kupata uhuru wao kutoka mikononi mwa Denmark. Kisiwa cha Iceland kiligunduliwa tarehe 10 Julai 874 Miladia na kuanzia wakati huo, ndipo wahajiri wa Norway, Scotland na Ireland wakaanza kuishi katika kisiwa hicho. Hadi kufikia karne ya 13 Miladia ilikuwa ni nchi huru hata hivyo muda baadaye iliunganishwa na Norway na kisha Denmark. Mwaka 1874 Denmark iliruhusu kuundwa baraza la watunga sheria (yaani bunge) katika kisiwa hicho cha Iceland. Aidha serikali ya ndani ya kisiwa hicho iliendelea kufuatilia haki zake zaidi ingawa bado kiliendelea kutambuliwa kuwa sehemu ya Denmark, hadi tarehe 17 Juni 1944 ambapo kulitangazwa kuvunjwa muungano huo baada ya kurejelewa maoni ya wakazi wa Iceland. Kuanzia wakati huo, wakakazi wa Iceland wanaitambua siku kama ya leo kuwa siku ya kitaifa.

Bendera Iceland