Jumapili, Juni 21, 2020
Leo ni Jumapili tarehe 29 Mfunguo Mosi Shawwal 1441 Hijria inayosadifiana na Juni 21 mwaka 2020 Milaadia.
Siku kama ya leo miaka 493 iliyopita aliaga dunia Niccolò Machiavelli, mwanahistoria na mwanasiasa wa Italia katika mji wa Florence. Sambamba na shughuli zake za kisiasa, Machiavelli aliandika pia historia ya Florence. Katika mtazamo wa kisiasa, Machiavelli alikuwa akiamini kwamba yawezekana kutumia wenzo wowote ule kwa ajili ya kupata madaraka na kwa ajili ya kuyalinda, na kwamba hakuna udharura wowote wa kuheshimu misingi ya maadili katika masuala kama hayo. Miongoni mwa kazi za mwanahistoria na mwanasiasa huyo wa Italia ni "The Art of War" na "The Prince."
Miaka 387 iliyopita mnajimu, mtaalamu wa hisabati na mwanafizikia wa Italia Galileo Galilei alilazimika kukana itikadi zake za kisayansi na kielimu mbele ya viongozi wa Kanisa. Mwaka 1632 Galilei aliandika kitabu akijibu na kukosoa mitazamo ya Betlemosi kuhusu sayari ya jua na kutangaza kuwa dunia inazunguka jua. Mwaka mmoja baadaye Papa wa Kanisa Katoliki alimwita Galileo mjini Roma na kuitaja mitazamo hiyo ya kisayansi kuwa ukafiri. Kwa msingi huo, kanisa lilimlazimisha Galileo akane itikadi zake za kielimu la sivyo akabiliwe na adhabu ya kifo. Japokuwa msomi huyo alikana mitazamo yake hiyo ya kielimu kidhahiri tu lakini wakati alipotoka nje ya mahakama alipiga chini mguu wake na kuiambia ardhi: "Licha ya haya yote lakini wewe unazunguka."
Siku kama ya leo miaka 50 iliyopita yaani sawa na tarehe 21 Juni 1970, alifariki dunia Dakta Ahmed Sukarno mpigania uhuru wa Indonesia. Sukarno alizaliwa mwaka 1901, na alikuwa mstari wa mbele katika mapambano yake dhidi ya mkoloni Mholanzi nchini humo. Kwa minajili hiyo, Sukarno aliwahi kukamatwa na kufungwa jela miaka minne na utawala wa kikoloni wa Uholanzi. Baada ya kifungo hicho alitiwa tena mbaroni na kubaidishwa. Mnamo mwaka 1949 alichaguliwa kuwa rais wa Indonesia na ilipofika mwaka 1965 Ahmed Sukarno aliondolewa madarakani baada ya kufanyika mapinduzi ya kijeshi yaliyoongozwa na Janerali Suharto.
Miaka 39 iliyopita sawa na tarehe Mosi Tir mwaka 1360 kwa mujibu wa Kalenda ya Kiirani, hayati Imam Ruhullah Khomeini alipasisha uamuzi wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu wa kutokuwa na imani na rais wa wakati huo Abul Hassan Bani Sadr na kwa utaratibu huo kiongozi huyo akalazimika kung'atuka madarakani. Bani Sadr ni miongoni mwa watu waliojidhihirisha kuwa wapenzi na watetezi wa harakati za Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran baada ya Imam Khomeini kuhamia Paris, Ufaransa na alifanikiwa kushika madaraka ya nchi na kuwa rais katika uchaguzi wa kwanza wa baada ya Mapinduzi ya Kiislamu nchini kwa kutumia ujanja wa kipropaganda. Muda mfupi baadaye Imam Khomeini alimkabidhi ukamanda wa majeshi ya Jamhuri ya Kiislamu. Hata hivyo Bani Sadr aliyekuwa mtu mwenye uchu wa madaraka, mwenye kiburi na msaliti alianza mara moja kushirikiana na makundi yaliyokuwa yakipinga Mapinduzi ya Kiislamu kwa lengo la kuangusha utawala wa Kiislamu nchini Iran.