Jun 23, 2020 02:41 UTC
  • Jumanne tarehe 23 Juni mwaka 2020

Leo ni Jumanne tarehe Mosi Dhulqaada 1441 Hijria sawa na Juni 23 mwaka 2020.

Siku kama ya leo miaka 1268 iliyopita, kwa mujibu wa baadhi ya mapokezi, alizaliwa Bibi Fatima Maasuma, binti yake Imam Musa al-Kadhim (as) ambaye ni miongoni mwa wajukuu watukufu wa Bwana Mtume (SAW). Fatima Maasuma (as) alikuwa hatibu hodari, mwalimu mahiri, zahidi na mcha-Mungu mkubwa. Alipatwa na maradhi alipokuwa njiani kuelekea Khorasan huko kaskazini mashariki mwa Iran kwa ajili ya kumtembelea kaka yake yaani Imam Ali bin Musa al Ridha (as) na akafariki dunia katika mji mtakatifu wa Qum baada ya kukaa hapo kwa siku 17. Leo hii ziara la mtukufu huyo linatembelewa na mamilioni ya waumini kila mwaka kutoka pembe mbalimbali za dunia.

Haram ya Bibi Maasuma katika mji mtakatifu wa Qum, Iran

Siku kama ya leo miaka 1100 iliyopita lilindwa bunge la kwanza duniani huko Island. Bunge hilo ambalo wawakilishi wake walikuwa wakichaguliwa na wananchi kupitia masanduku ya kura, lilikuwa na kazi ya kuisaidia serikali kifikra. Bunge la zamani zaidi duniani baada ya lile la Iceland, lilianza kazi zake nchini Uingereza katikati ya karne ya 13.

Siku lama ya leo miaka 484 iliyopita, ilianza harakati ya kiongozi wa kidini na mpenda mageuzi wa Ufaransa Calvin John huko Geneva mji mkuu wa Uswisi. Alizaliwa mwaka 1509 Miladia na kujifunza sheria na masomo ya kidini. Katika zama za ujana wake, Calvin John alijiunga na harakati ya Kiprotestanti ilioasisiwa na Martin Luther. Aliivamia Geneva Uswisi kwa kusaidiwa na wafuasi wa Kiprotestanti na kujaribu kuasisi mfumo wa uongozi wa kidini katika jamii ya nchi hiyo kwa mujibu wa dhehebu la Protestanti. Calvin John pia alianzisha mfumo wa ideolojia ya Kikristo iliyojulikana kama Calvinism na kubainisha itikadi zake katika kitabu chake alichokiita" Institutes of Christian Religion."

Miaka 263 iliyopita na katika siku mwafaka na leo, vilijiri vita vya kwanza kati ya vikosi vya Uingereza na India huko katika eneo la Bengali kaskazini mashariki mwa India. Waingereza walishinda vita hivyo na kulidhibiti eneo hilo ambalo katika zama hizo lilikuwa sehemu ya ardhi ya India. Waingereza ambao walianza kuingia nchini India miaka kadhaa nyuma kupitia East Indian Company, mbali na kuyarejesha nyuma majeshi ya India, katika vita vilivyofuata ilimshinda pia hasimu wake mkubwa Ufaransa na kufanikiwa kuyatoa kabisa majeshi hayo katika ardhi ya India.

Vita vya kwanza kati ya vikosi vya Uingereza na India.

Na tarehe 23 Juni miaka 81 iliyopita, Wafaransa waliikabidhi Uturuki bandari muhimu ya Iskenderun, eneo ambalo katika zama hizo lilikuwa sehemu ya ardhi ya Syria. Kwa miaka kadhaa kabla ya tukio hilo, Uturuki ilikuwa ikidai umiliki wa bandari hiyo. Hata hivyo baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia, eneo hilo lilikabidhiwa Syria kwa mujibu wa makubaliano yaliyokuwa yamefikiwa baina ya Uingereza na Ufaransa. Hata hivyo baada ya kuangushwa utawala wa Othmania na kuchukua hatamu za uongozi nchini Uturuki, Mustafa Kamal Ataturk aliyekuwa na mielekeo ya Kimagharibi Ufaransa ambayo wakati huo ilikuwa ikiikalia kwa mabavu Syria, iliikabidhi Bandari ya Iskenderun kwa Uturuki. Hatua hiyo ilipelekea kuongezeka hisia za chuki dhidi ya Ufaransa nchini Syria na kusababisha mapambano dhidi ya mkoloni huyo kuongezeka. Hadi leo hii serikali ya Syria ingali inasisitiza kwamba, Bandari ya Iskenderun ni mali yake.

Bandari  ya Iskenderun