Jun 25, 2020 22:04 UTC
  • Ijumaa tarehe 26 Juni 2020

Leo ni Ijumaa tarehe 4 Dhulqaada 1441 Hijria sawa na Juni 26 mwaka 2020.

Miaka 184 iliyopita katika siku inayosadifiana na hii ya leo, aliaga dunia Rouget de Lisle, malenga na mtunzi wa nyimbo za kimapinduzi wa Ufaransa. Rouget alihudumu pia jeshini na alikuwa akisoma mashairi ya kuwahamasisha wanamapinduzi wa Ufaransa na kutunga nyimbo za hamasa na za kusisimua. Rouget de Lisle alitunga wimbo wa kimapinduzi kwa jina "La Marseillaise" ambao baadaye ulikuwa wimbo rasmi wa taifa.

Rouget de Lisle

Miaka 75 iliyopita sawa na tarehe 26 Juni 1945, mkutano wa kimataifa wa San Fransisco ulimaliza shughuli zake katika mji unaojulikana kwa jina hilo huko Marekani kwa kupasishwa hati ya Umoja wa Mataifa. Mkutano huo ambao ulikuwa wa kwanza wa kimataifa kuwahi kufanyika baada ya Vita vya Pili vya Dunia, ulihudhuriwa na wawakilishi wa nchi 50 waitifaki katika vita hivyo.

Umoja wa Mataifa

Siku kama ya leo miaka 60 iliyopita kisiwa cha Madagascar kilipata uhuru kutoka kwa mkoloni Mfaransa. Uingereza na Ufaransa zilianzisha ushindani wa kuidhibiti nchi hiyo ya Kiafrika katika karne ya 18. Mwishoni mwa karne ya 19 Ufaransa ilikidhibiti kikamilifu kisiwa cha Madagascar. Hata hivyo wananchi wa Madagascar waliendesha mapambano mengi ya ukombozi dhidi ya wakoloni wa Kifaransa, miongoni mwake ni yale ya mwaka 1947 ambapo karibu watu elfu 80 waliuawa.

Bebndera ya Madagascar

Tarehe 6 Tir miaka 39 iliyopita Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei ambaye wakati huo alikuwa mwakilishi wa Imam Ruhullah Khomeini katika Baraza Kuu la Ulinzi na pia Imam wa Ijumaa wa Tehran, alinusurika jaribio la kutaka kumuua lililofanywa na wanachama wa kundi la kigaidi la MKO. Magaidi hao walilipua bomu katika moja ya misikiti ya Tehran ambako Ayatullah Khamenei alikuwa akihutubia hadhara ya watu na kumjeruhi vibaya. Hata hivyo Imam Khamenei aninusurika jaribio hilo kwa njia ya kimiujiza na baadaye akashika usukani wa kuongoza jahazi la Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini. Ayatullah Ali Khamenei alijeruhiwa vibaya mkono wake wa kulia katika shambulizi hilo.

Ayatullah Ali Khamenei

Na tarehe 26 Juni miaka 23 iliyopita Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa liliitangaza kuwa ni Siku ya Kimataifa ya Kuwatetea Wahanga wa Mateso kwa lengo la kufuta kabisa vitendo hivyo viovu duniani. Vitendo vya mateso vina historia ndefu duniani lakini ilitazamiwa kuwa maovu hayo yangehitimishwa kikamilifu katika zama hizi hususan baada ya kupasishwa nyaraka kadhaa zinazohusiana na haki za binadamu. Hata hivyo bado kuna nchi zinazotumia mateso kuwakandamiza wapinzani. Marekani ambayo inajinadi kuwa mtetezi mkubwa wa haki za binadamu ni miongoni mwa nchi zinazoongoza kutesa wapinzani kote duniani. Vilevile utawala wa Kizayuni wa Israel unaosaidiwa na kuungwa mkono na nchi za Magharibi hususan Marekani umekuwa ukiwatesa na kuwanyanyasa raia wa Palestina katika korokoro na jela zake za kutisha.