Jun 27, 2020 00:30 UTC
  • Jumamosi tarehe 27 Juni mwaka 2020

Leo ni Jumamosi tarehe 5 Dhulqaada mwaka 1441 Hijria inayosadifiana na Juni 27 mwaka 2020.

Tarehe 5 Dhilqaadi miaka 777 iliyopita aliaga dunia Radhiyuddin Ali bin Mussa bin Ja'far maarufu kwa jina la Ibn Twaus, faqihi, mpokezi wa hadithi na mwanazuoni mashuhuri wa Kiislamu katika eneo la Hillah nchini Iraq. Alipitisha kipindi cha utotoni katika mji huo na baadaye alihamia Baghdad ambako aliishi kwa kipindi cha karibu miaka 15. Ibn Twaus alipata umashuhuri mkubwa katika elimu na ucha-Mungu na ameandika vitabu vingi ambavyo ni marejeo ya taaluma za Kiislamu. Kitabu mashuhuri zaidi cha msomi huyo ni "al Luhuf" ambacho ndani yake anazungumzia matukio ya Siku ya Ashura na harakati ya Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib (as) katika medani ya Karbala na katika uwanja huo hakina kifani.

Ibn Twaus

Siku kama ya leo miaka 43 iliyopita Djibouti ilipata uhuru baada ya kukoloniwa kwa miaka kadhaa na serikali ya Ufaransa. Djibouti ilikuwa chini ya mkoloni Mfaransa tangu mwaka 1896 ikijulikana kwa jina la Somalia ya Ufaransa. Hata hivyo Djibouti hatimaye ilipata uhuru wake baada ya miongo minane ya mapambano. Djibouti ni miongoni mwa nchi za mwisho kujiunga na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu.

Bendera ya Djibouti

Katika siku kama ya leo miaka 39 iliyopita mwafaka na tarehe 7 mwezi wa Tir mwaka 1360 Hijria Shamsiya, Ayatullah Dakta Muhammad Beheshti aliuawa shahidi akiwa pamoja na watu wengine 72 waliokuwa miongoni mwa shakhsiya bora wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran baada ya kuripuliwa kwa bomu ofisi kuu ya chama cha Jamhuri ya Kiislamu. Ayatullah Beheshti pia alikuwa miongoni mwa shakhsiya wa awali waliotoa mchango mkubwa katika Mapinduzi ya Kiislamu. Dakta Beheshti pia alikuwa mmoja kati ya wasaidizi wakuu wa Imam Khomeini Mwenyezi Mungu amrehemu. Mlipuko huo wa bomu uliwaua shahidi Dakta Beheshti na wasaidizi 72 wa Imam Khomeini wakiwemo mawaziri na wabunge kadhaa.

Ayatullah Dakta Muhammad Beheshti

Na miaka 33 iliyopita katika siku kama ya leo mji wa Sardasht huko magharibi mwa Iran ulishambuliwa kwa mabomu ya kemikali na ndege za kivita za utawala wa zamani wa Iraq. Raia wasio na ulinzi 110 wa Iran wakazi wa mji huo waliuawa shahidi na wengine 530 kujeruhiwa katika mashambulizi hayo ya utawala wa zamani wa Saddam Hussein. Utawala wa Saddam ambao ulikuwa umekata tamaa ya kupata ushindi katika medani za vita dhidi ya Iran ulikuwa ukidhani kwamba kwa kufanya mashambulizi yake hayo ya kemikali dhidi ya raia wa mji wa Sardasht ungeweza kulitwisha taifa la Iran matakwa yake. Taasisi muhimu za kimataifa na madola makubwa duniani hata hivyo hazikuchukua hatua yoyote ya jadi ya kuuzuia utawala wa Saddam kutumia silaha za kemikali wala hata kulaani jinai hizo ulizozifanya dhidi ya raia wasio na hatia wa Iran.