Alkhamisi tarehe Pili Julai 2020
Leo ni Alkhamisi tarehe 10 Dhulqaada 1441 Hijria sawa na Julai Pili mwaka 2020.
Miaka 95 iliyopita katika siku kama hii ya leo alizaliwa Patrice Lumumba mhandisi wa uhuru wa Kongo. Lumumba alitoa mchango mkubwa katika juhudi za kukombolewa Kongo wakati wa harakati za ukombozi wa nchi za Kiafrika. Lumumba aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu na Waziri wa Ulinzi baada ya kuundwa Jamhuri ya Kongo mwaka 1960. Patrice Lumumba aliuawa mwaka 1961 na vibaraka wa Marekani na Ubelgiji baada ya kuvumilia mateso na unyama mkubwa. Lumumba aliandika vitabu kadhaa wakati wa uhai wake na mashuhuri zaidi ni kile alichokita "Kongo, Nchi Yangu."
Tarehe Pili Julai miaka 59 iliyopita aliaga dunia mwandishi mtajika wa Kimarekani kwa jina la Ernest Hemingway. Alizaliwa mwaka 1899 na kwa muda fulani alijishughulisha na uandishi huko Uingereza na Ufaransa. Hemingway alianzisha mbinu ya kuandika riwaya na tungo fupi fupi na alikuwa akitumia lugha nyepesi na inayoeleweka. Mwaka 1954 mwandishi Ernest Hemingway alitunukukiwa tuzo ya Nobel katika medani ya fasihi. Miongoni mwa vitabu maarufu vya Hemingway ni "The Old Man and The Sea", "A Farewell to Arms" na For Whom The Bell Tolls".
Tarehe 12 Tir 1349 Hijria Shamsia, yaani miaka 50 iliyopita katika siku kama hjii ya leo alifariki dunia Allamah Abdul Hussein Amini, faqihi mkubwa na mwandishi hodari na mashuhuri wa Kiislamu. Kitabu cha kwanza cha mwanazuoni huo alikipa jina la Shuhadaul Fadhila. Hata hivyo kitabu mashuhuri na kikubwa zaidi cha Allamah Amini ni kile cha "al Ghadiir Fil Kitabi Wassunnah". Ndani ya kitabu hicho Allamah Amini amekosoa na kuchunguza vitabu vikubwa na marejeo vya Kiislamu 150 akithibitisha wilaya na haki ya Imam Ali bin Abi Twalib ya kuwa Khalifa na Imam wa Waislamu baada tu ya Mtume Muhammad (saw) kufariki dunia. Mwanazuoni huyo alisafiri kwa taabu katika nchi nyingi kama India, Uturuki, Syria, Misri na Iraq kwa ajili ya kukusanya ushahidi mbalimbali wa kihistoria alioutumia katika kitabu hicho.
Siku kama ya leo miaka 32 iliyopita ndege ya abiria aina ya Airbus ya shirika la ndege la Iran iliyokuwa ikitoka Bandar Abbas, kusini mwa Iran na kuelekea Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu, ilishambuliwa kwa makombora mawili ya jeshi la Marekani kwenye maji ya Ghuba ya Uajemi. Manowari ya kijeshi ya Marekani USS Vincennes ilifyatua makombora hayo na kuua shahidi watu wote 298 waliokuwa katika ndege hiyo. Shambulio hilo lilidhihirisha zaidi unyama na ugaidi wa serikali ya Marekani. Viongozi wa Marekani walizidisha ukatili wao pale walipomzawadia medali ya ushujaa nahodha wa meli hiyo kutokana na kitendo hicho kilichoonekana na serikali ya Washington kuwa eti ni cha kishujaa.