Ijumaa tarehe 3 Julai mwaka 2020
Leo ni Ijumaa tarehe 11 Dhulqaada 1441 Hijria sawa na Julai 3 mwaka 2020
Siku kama ya leo miaka 1293 iliyopita, sawa na tarehe 11 Dhulqaada mwaka 148 Hijria, alizaliwa Imam Ali bin Mussa Ridha (as), mmoja kati ya Watu wa Nyumba ya Mtume Muhammad (as) katika mji wa Madina. Imam Ridha alichukua jukumu la kuwaongoza Waislamu mara baada ya kufariki dunia baba yake, Imam Mussa al-Kadhim (as), mnamo mwaka 183 Hijria. Shakhsia huyo alikuwa mbora zaidi katika ulimwengu wa Kiislamu wakati wa zama zake. Kwa minajili hiyo, Ma'amun, Khalifa wa Kiabbasi alijaribu kumpatia wadhifa Imam Ridha (as) kwa shabaha ya kuimarisha nafasi yake na wakati huo huo kumdhibiti mjukuu huyo wa Mtume. Imam Ridha (as) alikubali pendekezo hilo kwa kulazimishwa na kwa mashinikizo ya utawala wa Ma'amun. Mtukufu huyo aliwaeleza Waislamu wote, wakiwemo watu wa eneo la Khorasan, ukweli wa mambo ulivyo, na kuwaathiri mno wananchi kuhusiana na uhakika wa Ahlul-Bait wa Mtume (as). Redio Tehran inatoa mkono wa heri na fanaka kwa Waislamu wote duniani hususan wapenzi wa Watu wa Nyumba ya Mtume (as) kwa mnasaba huu.

Siku kama ya leo miaka 1105 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 11 Dhulqaada 336 Hijria, ilizaliwa Muhammad bin Muhammad mwenye lakabu ya Sheikh Mufid, msomi na mwanafaqihi mkubwa wa ulimwengu wa Kiislamu katika mji wa Baghdad. Sheikh Mufid alilelewa katika familia ya kielimu, kidini na yenye imani na kisha kujipatia elimu kutoka kwa wanazuoni wakubwa katika zama hizo. Miongoni mwa harakati za kifikra na kiutamaduni za Sheikh Mufid ni kufanya midahalo na mafaqihi na wasomi wa madhehebu mbalimbali. Sheikh Mufid ametuachia vitabu vingi vyenye thamani vikiwemo al Irshaad, al Arkaan na Usulul Fiqh.

Katika siku kama ya leo miaka 116 iliyopita inayosadifiana na 3 Julai 1904, alifariki dunia Theodor Herzl, mwasisi wa harakati ya Kizayuni. Herzl alizaliwa mwaka 1860 huko Bucharest mji mkuu wa Hungary na kisha kuelekea Austria. Mnamo mwaka 1897 aliunda Taasisi ya Kimataifa ya Kizayuni kwenye kongamano lililofanyika nchini Uswisi. Herzl alibuni mikakati ya kuasisiwa utawala ghasibu na wa Kizayuni wa Israel kwenye ardhi za Palestina, utawala ambao hadi leo unaendelea kufanya jinai kubwa na kusababisha maafa yasiyo na kifani dhidi ya raia madhlumu wa Palestina.
Tarehe 3 Julai miaka 7 iliyopita rais wa zamani wa Misri kutoka harakati ya Ikhwanul Muslimin, Muhammad Morsi aliondolewa madarakani katika mapinduzi yaliyoongozwa na jeshi la nchi hiyo. Mapinduzi hayo yaliongozwa na Jenerali Abdel Fattah al Sisi. Morsi alichaguliwa kuwa rais wa kwanza wa Jamhuri ya Misri baada ya mapinduzi ya wananchi ya mwaka 2011. Hata hivyo mwanasiasa huyo hakuweza kutatua matatizo ya kisiasa na kiuchumi ya muda mrefu ya nchi hiyo. Vilevile licha ya kwamba alihesabiwa kuwa katika safu za wanaharakati wa Kiislamu lakini alidumisha uhusiano wa karibu na utawala haramu wa Israel na akatangaza kutambua rasmi mkataba ya Camp David na utawala huo haramu. Vilevile alitekeleza siasa zisizo sahihi kuhusu baadhi ya nchi za Kiislamu na hatimaye akasalitiwa na nchi alizozitegemea ambazo ziliwaunga mkono na kuwasaidia wale waliomuondoa madarakani.