Jul 04, 2020 00:00 UTC
  • Jumamosi, 4 Julai, 2020

Leo ni Jumamosi tarehe 12 Mfunguo Pili Dhul-Qaadah 1441 Hijria ambayo inasadifiana na tarehe 4 Julai 2020 Miladia.

Tarehe 14 Tir katika kalenda ya Iran imepewa jina la Siku ya Kalamu. Kwa hakika kalamu huhifadhi elimu, maarifa na ni mlinzi wa fikra za wanazuoni na wanafikra na hivyo kuwa kiunganishi cha kifikra na daraja la mawasiliano baina ya watu wa zamani na wa leo. Aidha hata mawasiliano baina ya mbingu na ardhi yamepatikana kupitia kalamu. Hivyo basi kalamu ni mtunza siri wa mwanadamu na hazina ya elimu na mkusanyaji wa tajiriba za karne nyingi. Na kama tunaona katika Qur’ani Mwenyezi Mungu ameapa kwa kalamu kwa kusema: Nuun. Naapa kwa kalamu na yale wayaandikayo, basi hilo linatokana na umuhimu wa jambo hili, kwani kiapo mara nyingi hufanywa kwa jambo au kitu ambacho kina thamani na chenye kuheshimiwa mno. *** 

Sikuu ya Kalamu

Siku kama ya leo miaka 244 iliyopita, wawakilishi wa majimbo 13 ya awali ya Marekani walisaini "Tangazo la Uhuru" wa nchi hiyo katika mji wa Philadelphia. Ardhi ya Marekani kwa maelfu ya miaka ilikuwa makazi ya Wahindi Wekundu. Mwishoni mwa karne ya 15 Miladia wavumbuzi wa Ulaya waliwasili Marekani na nchi mbalimbali za Ulaya zikavamia na kukalia kwa mabavu kila eneo la Marekani. Wazungu hao wa Ulaya waliandamana na mamilioni ya watumwa kutoka Afrika ambao walitumiwa katika kazi ngumu za mashambani na viwandani. ***

Bendera ya Marekani

 

Katika siku kama ya leo miaka 97 iliyopita, Adib Neyshabouri, mshairi na malenga stadi wa Kiirani aliaga dunia. Alizaliwa mwaka 1281 Hijria katika mji wa Neyshabur moja ya miji ya kaskazini mashariki mwa Iran. Akiwa mdogo Adib Neyshabouri alikumbwa na ugonjwa wa ndui na kuwa kipofu. Hata hivyo mapenzi yake makubwa ya kusoma na kujifunza yalimsukuma na kumfanya awe mmoja wa wasomi wakubwa hasa katika uga wa mashairi na fasihi ya lugha. Kuna beti takribani 6,000 za mashairi ya msomi huyo zilizokusanywa hadi sasa.***

Adib Neyshabouri

Miaka 74 iliyopita katika siku kama ya leo, visiwa vya Ufilipino vilijitangazia uhuru wake kutoka kwa Marekani. Fernando Magellan mvumbuzi wa Kireno pamoja na wenzake ndio waliokuwa Wazungu wa kwanza kutoka Ulaya kuwasili katika ardhi ya Ufilipino na hiyo ilikuwa mwaka 1521. Katika kipindi cha nusu karne baadaye, Uhispania ikawa imeidhibiti ardhi yote ya nchi hiyo. Mkoloni Muhispania alipora mali na utajiri wa Ufilipino kwa muda wa karne tatu. ***

Bendera ya Ufilipino

 

Miaka 38 iliyopita katika siku kama ya leo, wanadiplomasia watatu na mwandishi habari mmoja wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran walitekwa nyara na wapiganaji wa chama cha Falanja cha Lebanon kaskazini mwa Beirut. Wanadiplomasia hao na mwandishi wa habari wa Iran walitekwa nyara wakati walipokuwa wakielekea kazini katika ubalozi wa Iran huko Beirut. Wakati tukio hilo lilipojiri jeshi la utawala wa Kizayuni lilikuwa limeishambulia Lebanon na chama cha Falanja kilikuwa na ushirikiano wa karibu na utawala ghasibu wa Israel. Ushahidi na nyaraka zilizopo zinaonyesha kuwa raia hao wa Iran wanashikiliwa na utawala wa Kizayuni wa Israel.***

 

Na katika siku kama ya leo miaka 10 iliyopita,  Ayatullah Sayyid Muhammad Hussein Fadhlullah mmoja wa maulama mashuhuri na marja taqlidi wa Kiislamu alifariki dunia. Allama Fadhlullah alizaliwa mwaka 1935 katika mji mtakatifu wa Najaf nchini Iraq katika familia ya kidini yenye asili ya Lebanon. Allama Fadhlullah alianza kujifunza elimu ya dini katika Chuo Kikuu cha Kidini (Hawza) cha mji wa Najaf  Iraq akiwa bado kijana mdogo. Alijishughulisha na uandishi wa makala na vitabu na alikuwa na alikuwa mshairi. Ayatullah Fadhlullah alikuwa miongoni mwa waungaji mkono wakubwa wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran na Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Lebanon Hizbullah na jambo hilo liliikasirisha sana Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel ambazo zilifanya majaribio kadhaa ya kutaka kumuua. Ayatullah Muhammad Hussein Fadhlullah ameandika vitabu vingi vya thamani ikiwemo tafsiri ya Qur'ani ya "Min Wahyil Qur'an."

 Ayatullah Sayyid Muhammad Hussein Fadhlullah