Jul 08, 2020 19:37 UTC
  • Alkhamisi, Julai 9, 2020

Leo ni Alkhamisi tarehe 17 Mfunguo Pili Dhulqaada 1441 Hijria sawa na Julai 9 mwaka 2020 Milaadia.

Siku kama ya leo miaka 9 iliyopita Sudan Kusini ilitangazwa rasmi kuwa nchi huru inayojitawala. Nchi mpya ya Sudan Kusini iliundwa baada ya kujitenga na Sudan. Raia wa Sudan Kusini tarehe Tisa mwezi Julai mwaka 2011 walishiriki kwenye kura ya maoni kwa ajili ya kuainisha mustakbali wa eneo la kusini mwa Sudan na lile la kaskazini, kura ambayo hatimaye ilipelekea eneo la kusini mwa Sudan kujitenga na lile la kaskazini na kuundwa nchi inayojitawala ya Sudan Kusini.

Ramani ya Sudan Kusini

Miaka 18 iliyopita mwafaka na tarehe 9 Julai mwaka 2002 Umoja wa Afrika (AU) ulichukua nafasi ya Umoja wa Nchi Huru za Kiafrika (OAU) baada ya kuidhinishwa na wakuu wa nchi za Kiafrika. OAU iliundwa mwaka 1963 ili kusaidia juhudi za kupigania uhuru wa nchi za Kiafrika na kutatua hitilafu miongoni mwa nchi hizo. Hata hivyo siku baada ya siku kulijitokeza hisia kwamba katika mazingira ya ulimwengu wa leo kuna udharura wa kuundwa taasisi yenye nguvu za utendaji na yenye malengo mapya zaidi. Kwa msingi huo katika siku kama ya leo mwaka 2002 wakuu wa nchi wanachama wa Umoja wa Nchi Huru za Kiafrika (OAU) waliunda Umoja wa Afrika (AU) katika mji wa Durban, Afrika Kusini. Taasisi kama vile bunge, kamisheni ya utendaji, benki kuu, mfuko wa fedha na mahakama zimezingatiwa katika umoja huo kwa ajili ya kuratibu mawasiliano na kusaidia ustawi wa kiuchumi wa nchi za Kiafrika.

Umoja wa Afrika

Siku kama ya leo miaka 72 iliyopita na baada ya usitishaji vita wa mwezi mmoja, vita kati ya Waarabu na utawala haramu wa Israel vilianza tena. Vita hivyo vilianza baada ya kuasisiwa utawala ghasibu wa Israel unaoikalia Quds Tukufu kwa mabavu mwezi Mei 1948. Vita hivyo vilisimama mwezi Juni mwaka huo kufuatia ombi la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Vita kati ya utawala wa Kizayuni na Waarabu vilipelekea kukaliwa kwa mabavu asilimia 78 ya ardhi ya Palestina na Wapalestina 750,000 kuwa wakimbizi.

Utawala wa Kizayuni wa Israel

Siku kama ya leo miaka 1262 iliyopita Imam Mussa al Kadhim (as) ambaye ni miongoni mwa Ahlubait wa Mtume wetu Muhammad (saw) alibaidishwa kutoka Madina na kupelekwa Iraq kwa amri ya mtawala dhalimu, Haroun Rashid. Mtukufu huyo aliwasili Iraq tarehe 7 Dhilhijja 179 Hijria na kufungwa katika jela mji huo. Kwa muda, Imam aliwekwa katika jela ya Issa bin Jaafar aliyekuwa mtawala wa Basra lakini mtawala huyo alimwandikia barua Haroun Rashid akimuomba amkabidhi Imam kwa mtu mwingine kwa sababu hakupata ushahidi wowote dhidi ya mtukufu huyo. Haroun Rashid alimpeleka tena uhamishoni Imam mjini Baghdad na akamtaka waziri wake, Fadhl bin Rabii amuue mjukuu huyo wa Mtume. Waziri huyo alikataa na hivyo Haroun alimtaka mtu aliyejulikana kwa jina la Yahya bin Khalid Barmaki atekeleze amri hiyo. Hatimaye Imam Kadhim (as) aliuuliwa shahidi na muovu huyo kwa amri ya mtawala Haroun Rashid.