Jul 19, 2020 02:53 UTC
  • Jumapili tarehe 19 Julai 2020

Leo ni Jumapili tarehe 27 Mfunguo Pili Dhulqaada 1440 Hijria sawa na Julai 19 mwaka 2020 Milaadia.

Miaka 127 iliyopita alizaliwa malenga wa Russia kwa jina la Vladimir Mayakovsky. Mashairi ya Mayakovsky yalikuwa na nafasi kuu wakati wa mapinduzi ya Kikomonisti ya Urusi ya zamani mwaka 1917. Vladimir Mayakovsky alikuwa akiamini kuwa fasihi inapasa kuwa lugha ya watu wengi na inayobainisha maisha yao ya kijamii.

Vladimir Mayakovsky

Miaka 41 iliyopita katika siku kama ya leo mapinduzi ya wananchi wa Nicaragua yalipata ushindi dhidi ya dikteta Anastasio Somoza wa nchi hiyo na muitifaki wake mkubwa yaani Marekani. Dikteta huyo kibaraka wa Marekani alichukua hatamu za uongozi wa Nicaragua mwaka 1967 na tangu wakati huo wimbi kubwa la upinzani lilianza kuenea nchini kote na katika America ya Kati dhidi ya kiongozi huyo. Mapambano ya silaha ya wapiganaji wa msituni ya Harakati ya Ukombozi wa Kitaifa ya Sandinista (FSLN) yaliyoanza mwaka 1963 yalipamba moto zaidi katikati ya muongo wa 1970 na kuungwa mkono na wananchi. Hatimaye Somoza alilazimika kukimbia nchi baada ya jeshi la Sandinista kuingia Managua mji mkuu wa Nicaragua katika siku kama ya leo. Karibu watu elfu 40 waliuawa katika mapinduzi ya Nicaragua.

Bendera ya Nicaragua

Siku kama ya leo miaka 59 iliyopita, Kuwait iliondokana na ukoloni wa Uingereza. Katika kipindi cha utawala wa Achaemenid, Kuwait ilikuwa ikihesabiwa kuwa sehemu ya ardhi ya Iran. Mwaka 1899 Miladia, Kuwait iliwekeana saini na Uingereza, suala lililoifungulia London mlango wa kuikoloni nchi hiyo. Mwenendo huo uliendelea hadi baada ya Vita vya Pili vya Dunia. Kuwepo kwa visima vya mafuta kulipanua uingiliaji mkubwa wa mashirika mengi ya Uingereza na Marekani katika taifa hilo. Hatimaye mwaka 1961 Kuwait na Uingereza zilitiliana saini makubaliano yaliyoifanya nchi hiyo kujipatia uhuru wake.  

Siku kama ya leo miaka 33 iliyopita, azimio nambari 598 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipasishwa likisisitiza umuhimu wa kuhitimishwa vita kati ya Iran na Iraq. Azimio hilo lilijumuisha mada 10 na lilipasishwa kwa kauli moja na wanachama 15 wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Azimio hilo linahesabiwa kuwa, moja ya mambo machache ambayo wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama walikubaliana katika historia ya miaka 40 ya Umoja wa Mataifa. Utawala wa Iraq ulitangaza kulikubali mara moja azimio hilo bila masharti yoyote.

Miaka mitano iliyopita katika siku kama ya leo yaani 27 Dhulqaada mwaka 1436 Hijria Qamaria

Winchi kubwa ya ujenzi ilianguka katika eneo moja la Msikiti Mtakatifu wa Makka na kuua idadi kubwa ya mahujaji wa Baitullah al-Haram yaani Nyumba Tukufu ya Mwenyezi Mungu. Tukio hilo lilijiri Ijumaa saa 17:10 alasiri  Septemba 11 mwaka 2015 kwa mujibu wa kalenda ya Miliadia ambapo winchi hiyo ilipelekea watu 107 kupoteza maisha na wengine 238 kujeruhiwa. Aghalabu ya waliopoteza maisha walikuwa ni kutoka India, Pakistan, Indonezia na Iran. Wakuu wa Saudia walisema winchi hiyo ilianguka kutokana na upepo mkali. Tukio hilo la kusikitisha lilionyesha uzembe wa hali ya juu wa utawala wa Saudia. Tukio hilo la kuanguka winchi na maafa ya Mina wakati wa Siku Kuu ya Idul Adha mwaka huo huo ni kati ya matukio machungu zaidi katika Ibada ya Hija.

Ajali ya Winchi katika Msikiti wa Makka

 

Tags