Aug 21, 2020 00:04 UTC
  • Ijumaa tarehe 21 Agosti mwaka 2020

Leo ni Ijumaa tarehe Mosi Muharram 1442 Hijria sawa na 21 Agosti mwaka 2020.

Tarehe Mosi Muharram inasadifiana na kuanza mwaka mpya wa Hijria Qamaria. Mwaka wa Hijria Qamaria unahesabiwa kwa mujibu wa mzunguko wa mwezi na katika nchi nyingi za Kiislamu unatumiwa kwa ajili ya masuala ya kidini au hata kijamii. Mwaka wa Hijria Qamaria pia unatumika katika masuala mengi ya kiibada kama vile kuainisha mwanzo wa funga ya mwezi wa Ramadhani, Hija, kuainisha miezi mitakatifu na kwa ajili ya historia ya matukio mbalimbali. Mwaka wa Hijria ulianzishwa katika zama za utawala wa khalifa Umar bin Khattab kutokana na ushauri uliotolewa na Amirul Muuminin Ali bin Abi Twalib (as) ambaye aliagiza mwanzo wa hijra ya Mtume kutoka Makka na kwenda Madina uwe mwanzo wa mwaka wa Kiislamu.    

Siku kama ya leo miaka 1444 iliyopita yaani tarehe Mosi Muharram mwaka wa 7 tangu Mtume (saw) abaathiwe na kupewa utume kwa mujibu wa nukuu za baadhi ya wanahistoria wa Kiislamu, Makuraishi walifunga mkataba wa kuweka mzingiro wa kiuchumi dhidi ya Mtume Muhammad (saw) na Ahlibaiti zake. Viongozi wa makafiri wa Makka ambao walikuwa na wasiwasi mkubwa kutokana na kasi ya kustawi Uislamu na vilevile kutokana na kufeli njama zao za kuzuia kuenea dini hiyo, waliamua kuweka mzingiro wa kiuchumi ili kufanikisha malengo yao. Kwa msingi huo waliamua kuweka mkataba dhidi ya Waislamu. Mkataba huo uliwakataza watu wote kufanya muamala wa aina yoyote na wafuasi wa dini ya Uislamu. Mtume Muhammad (saw) na masahaba zake walizingirwa kwa kipindi cha miaka mitatu katika bonde lililojulikana kwa jina la Shiibi Abi Twalib wakisumbuliwa na matatizo mengi na mashinikizo ya kiuchumi na katika kipindi hicho Mtume (saw) alipoteza wasaidizi wake wawili muhimu yaani ami yake, Abu Twalib na mkewe kipenzi, Bibi Khadija. Waislamu hao walisimama imara kulinda imani yao na hawakutetereka hata kidogo licha ya matatizo makubwa waliyokabiliana nayo. Mzingiro huo wa kiuchumi dhidi ya Waislamu ulikomeshwa mwezi Rajab mwaka wa kumi baada ya kubaathiwa Mtume.

Shiibi Abi Twalib

Siku kama ya leo miaka 61 iliyopita, iliasisiwa The Central Treaty Organization ambayo ilikuwa ikijulikana kwa jina la Cento na kuchukua nafasi ya mkataba wa Baghdad. Taasisi hiyo iliundwa na Iran, Uturuki, Pakistan na Uingereza mjini Ankara Uturuki. Pamoja na kuwa Marekani haikuwa mwanachama rasmi wa Taasisi ya Cento na ilishiriki kwenye vikao vya jumuiya hiyo kama mtazamaji tu, lakini ilikuwa na nafasi kuu katika maamuzi yote ya taasisi hiyo. The Central Treaty Organization ilivunjika baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran na kujiondoa nchi hiyo katika mkataba huo mwaka 1979.

Mkataba wa The Central Treaty Organization

Tarehe 21 Agosti mwaka 1965 yaani katika siku kama hii ya leo miaka 55 iliyopita Wamarekani wenye asili ya Afrika katika mji wa Alabama walifanya maandamano wakitaka kutekelezwa sheria ya haki ya kupiga kura. Maandamano hayo yalizidisha harakati ya vuguvugu la kupigania haki za kijamii za Wamarekani weusi. Harakati hiyo ilianza mwaka 1955 kwa lengo la kupigania usawa kati ya Wamarekani weusi na wazungu na ilimalizika mwaka 1968 baada ya kupasishwa sheria ya haki za kiraia.

Vuguvugu la kupigania haki za kijamii za Wamarekani weusi

Siku kama ya leo miaka 51 iliyopita, inayosadifiana na 21 Agosti 1969 Miladia, Masjidul Aqsa Kibla cha Kwanza cha Waislamu, kilichomwa moto na Wazayuni. Katika tukio hilo, eneo hilo takatifu na la kihistoria liliharibika vibaya sana. Utawala wa Kizayuni wa Israel ulidai kuwa, kitendo hicho kilifanywa na mtalii wa Kiaustralia. Utawala huo wa Kizayuni ulitayarisha mahakama ya kimaonyesho tu mjini Tel Aviv na kuchukua uamuzi wa kumuachilia huru mhalifu huyo kwa madai kwamba alikuwa na matatizo ya kiakili. Baada ya kutokea kitendo hicho, nchi za Kiislamu zilikutana na kuamua kuunda Jumuiya ya Nchi za Kiislamu (OIC).

Msikiti wa al Aqsa ulichomwa moto na Wazayuni

Na miaka 29 iliyopita katika siku kama hii ya leo Latvia ambayo ni miongoni mwa nchi za Baltic huko magharibi mwa Urusi ya zamani ilijitangazia uhuru. Latvia ilikuwa chini ya satwa ya Urusi ya zamani kufuatia makubaliano ya siri yaliyofikiwa mwaka 1939 Miladia kati ya Hitler na Stalin. Mwaka 1991, karibu asilimia 80 ya wananchi wa Latvia walishiriki kwenye kura ya maoni na kupelekea kutangazwa uhuru wa nchi hiyo katika siku kama hii.

Latvia