Jumatatu tarehe 24 Agosti mwaka 2020
Leo ni Jumatatu tarehe 4 Mfunguo Nne Muharram 1442 Hijria sawa na Agosti 24 mwaka 2020.
Siku kama ya leo, miaka 1381 iliyopita, Ubaidullah bin Ziyad, mtawala dhalimu na fasiki wa mji wa Kufa, Iraq alitoa hotuba katika msikiti wa mji huo. Katika hotuba hiyo, Ibn Ziyad alitoa vitisho vikali dhidi ya wafuasi wa Imam Hussein (as), mjukuu wa Bwana Mtume Muhammad (swa) akiwataka wasimsaidie mtukufu huyo katika ardhi ya Karbala na kwamba atamuua mtu yeyote ambaye ataasi amri hiyo. Kwa kutumia fatwa ya hila iliyotolewa na Shuraihul-Qadhi ya kuhalalisha damu ya Imam Hussein (as), Ibn Ziyad akafunga njia zote za kuingia na kutoka mji wa Kufa huku akitoa fedha kwa wakazi wa mji huo kwa ajili ya kwenda kupambana na mjukuu huyo wa Mtume huko Karbala tukio lililomalizika kwa kuuawa Imam Hussein na watu wa familia ya Mtume (swa).

Siku kama ya leo miaka 957 iliyopita, alifariki dunia Abul-Qasim Muhammad Baghdadi, maarufu kwa jina la Ibn Naqiya, malenga, mwandishi na fasihi mkubwa wa mjini Baghdad, Iraq. Umahiri aliokuwa nao Ibn Naqiya, ndio uliofanya kuwa mashuhuri ambapo hata wataalamu wa mashairi waliyatumia mashairi yake. Kitabu cha ‘Maqaamaat’ ni moja ya athari zinazonasibishwa kwa malenga huyo. Katika kitabu hicho Ibn Naqiya, alizungumzia maovu ya kijamii kupitia hekaya na tenzi. Athari nyingine inayonasibishwa kwa msomi huyo wa Kiislamu, ni kitabu kinachoitwa ‘Al-Jamaan fi Tashbiihaatil-Qur’an’ ambayo ni tafsiri nyepesi ya Qur’an Tukufu. Katika tafsiri hiyo Ibn Naqiya amefafanua aya 226.

Siku kama ya leo miaka 91 iliyopita, yalianza mapambano ya Ukuta wa Nudba huko Baitul Muqaddas. Ukuta wa Nudba huko magharibi mwa Masjidul Aqswa ni eneo alilotumia Mtume Muhammad (saw) wakati wa kupaa mbinguni katika safari ya Mi'iraj na kwa sababu hiyo eneo hilo likawa na umuhimu wa kidini na kihistoria kwa Waislamu. Tangu wiki moja kabla ya kuanza mapambano hayo ya Ukuta wa Nudba, Wazayuni ambao taratibu walikuwa wameanza kuikalia kwa mabavu Palestina kwa kuungwa mkono na Uingereza, walianzisha harakati dhidi ya Waislamu. Siku hiyo Wapalestina wenye hasira walianzisha mapambano makali dhidi ya Wazayuni hao maghasibu. Mapambano hayo yalienea kwa kasi kwenye miji mingine ya Palestina na Waingereza wakaamua kutangaza utawala wa kijeshi huko Palestina kwa kuhofia hasira za Wapalestina.
Miaka 79 iliyopita katika siku kama ya leo vikosi vya waitifaki viliikalia kwa mabavu Iran wakati wa Vita vya Pili vya Dunia. Kusonga mbele haraka jeshi la Ujerumani ya Kinazi katika ardhi ya Urusi ya zamani kulizitia wasiwasi mkubwa Marekani, Ufaransa na Uingereza. Hii ni kwa sababu maslahi ya Magharibi katika eneo la Mashariki ya Kati na ya Mbali yangekuwa hatarini iwapo Ujerumani ingefanikiwa kuikalia kwa mabavu Urusi ya zamani, suala ambalo pia lingezidisha uwezekano wa Urusi kushinda vita. Kwa sababu hiyo nchi hizo tatu zilichukua uamuzi wa kutumia ardhi ya Iran kwa ajili ya kutuma misaada ya silaha na chakula huko Urusi. Kwa msingi huo mapema asubuni tarehe 3 Shahrivar mwaka 1320 Hijria Shamsia vikosi vya majeshi ya Urusi kutokea kaskazini magharibi na jeshi la Uingereza kutokea kusini vilifanya mashambulizi ya anga, baharini na nchi kavu dhidi ya Iran. Baada ya majeshi hayo ya kigeni kushinda jeshi dhaifu la Shah yaliuteka na kuukalia kwa mabavu mji wa Tehran.
Na siku kama leo miaka 29 iliyopita, Ukraine ilipata uhuru toka kwa Umoja wa Kisovieti. Russia ilianza kuikalia kwa mabavu Ukraine ambayo wakati huo ilikuwa chini ya udhibiti na utawala wa Poland, katikati mwa karne ya 17. Hata hivyo mwaka 1922, nchi hiyo iliunganishwa na mataifa yaliyokuwa yakiunda Umoja wa Sovieti. Hatimaye katika tarehe kama ya leo, Ukraine ilipatia uhuru wake.
