Jumanne, tarehe 25 Agosti, mwaka 2020
Leo ni Jumanne tarehe 5 Muharram 1442 Hijria sawa na Agosti 25 mwaka 2020.
Katika siku kama ya leo miaka 925 iliyopita sawa tarehe 25 Agosti mwaka 1095, vilianza Vita vya Msalaba kati ya Wakristo na Waislamu. Watu wa msalaba walianzisha vita hivyo kidhahiri wakiwa na lengo la kuteka Baitul Muqaddas, ingawa shabaha halisi ya wapiganaji hao ilikuwa ni kudhibiti ardhi kubwa za Waislamu na kuwanyonya na kuwakoloni wafuasi wa dini hiyo. Katika vita hivyo wafuasi wa kanisa walichora alama za msalaba kwenye mabega na mavazi yao, na kwa sababu hiyo vita hivyo vimekuwa maarufu kwa jina la Vita vya Msalaba. Baada ya vita vingi na Waislamu, wapiganaji wa msalaba hatimaye waliuteka na kuukalia kwa mabavu mji wa Baitul Muqaddas mnamo mwaka 1099, ambako waliua raia wengi na kupora mali zao. Mji huo ulikombolewa mwaka 1187 na wapiganaji wa Kiislamu waliokuwa wakiongozwa na Salahuddin Ayyubi.
Miaka 195 iliyopita mwafaka na siku hii ya leo, Uruguay ilipata uhuru. Tangu Uruguay ivumbuliwe na wagunduzi wa Kihispania mwaka 1516, ilitawaliwa na Wareno na Wahispania. Baina ya mwaka 1810 na 1814 kulitokea uasi uliopelekea umwagaji damu mkubwa, ambapo baada ya matukio hayo, nchi hiyo ikawa huru kwa kiasi fulani. Hata hivyo mwaka 1820 Brazil ikaikalia tena kwa na miaka mitano baadaye Uruguay ikajikomboa na kujipatia uhuru kamili.
Miaka 153 iliyopita katika siku kama hii ya leo alifariki dunia msomi mashuhuri wa Uingereza Michael Faraday. Faraday alizaliwa mwaka 1791 mjini London na licha ya kuwa hakuwa na elimu ya juu lakini alifanikiwa kupata maendeleo muhimu katika fizikia na kemia kwa kutumia majaribio na tajiriba. Tarehe 24 Novemba miaka 184 iliyopita, Michael Faraday aligundua chombo cha mkondo wa umeme kinachojulikana kwa kitaamu kama ''Electric Current''. Kwa ugunduzi huo Faraday akawa amefanikiwa kupiga hatua kubwa katika elimu ya fizikia. Miongoni mwa mafanikio mengine makubwa yaliyoletwa na mtaalamu huyo ni pale alipogundua mota ya umeme pamoja na kubadilisha nguvu za sumaku kuwa nguvu za umeme.
Katika siku kama hii ya leo miaka 41 iliyopita katika siku kama ya leo ya tarehe 4 Shahrivar 1358 Hijria Shamsia, Mahdi Iraqi na mwanawe Hissam waliuawa shahidi na magaidi wa kundi la Munafiqin (MKO). Mahdi Iraqi alikuwa mmoja wa shakhsia watajika wa Mapinduzi ya Kiislamju ya Iran na alifanya mapambano kwa miaka kadhaa dhidi ya utawala wa Shah. Iraqi alikuwa na uhusiano wa karibu na Imam Khomeini MA. Mwanamapambano huyo muumini alifungwa jela na utawala wa Shah kwa miaka kadhaa na kukumbana na mateso mengi.
Na siku kama ya leo miaka 32 iliyopita, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilitoa azimio nambari 620 likilaani hatua ya Iraq ya kutumia silaha za kemikali. Baada ya utawala wa zamani wa Iraq kushambulia kwa mabomu ya kemikali makazi ya raia nchini Iran na kufuatia mashtaka yaliyowasilishwa na Iran, ujumbe wa Umoja wa Mataifa ulitumwa katika nchi za Iran na Iraq na ukatoa ripoti mbili ambazo zilieleza kuwa, utawala huo ulitumia mara kadhaa silaha za kemikali dhidi ya majeshi na raia wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Hii ilikuwa mara ya kwanza kwa Umoja wa Mataifa kukiri waziwazi kwamba, jeshi la Iraq lilitumia silaha za kemikali dhidi ya Iran. Katika kipindi chote cha vita vya miaka 8 vilivyoanzishwa na Iraq dhidi ya Iran, utawala wa Saddam Hussein uliua shahidi maelfu ya wanajeshi na raia wa Iran kutokana na kutumia silaha za gesi yenye kemikali. Kwa sababu hiyo Iran inatambuliwa kuwa mhanga mkubwa zaidi wa silaha za kemikali duniani baada ya Vita vya Pili vya Dunia.