Sep 03, 2020 04:04 UTC
  • Alkhamisi, 03 Septemba, 2020

Alkhamisi tarehe 14 Muharram 1442 Hijria sawa na Septemba 3 mwaka 2020.

Siku kama ya leo miaka 102 iliyopita, Damascus mji mkongwe na wa kihistoria wa Kiislamu ulikaliwa kwa mabavu na vikosi vya majeshi ya Uingereza. Moja kati ya malengo makuu ya serikali za Ulaya wakati wa kujiri Vita vya Kwanza vya Dunia ilikuwa kuugawa utawala wa Othmania, lengo ambalo baadaye lilifanikiwa. Wakati utawala wa Othmania ulipokuwa ukigawanywa, maeneo yaliyokuwa chini ya utawala huo, nayo moja baada ya jingine yalidhibitiwa na Ufaransa na Uingereza, ambapo mji wa Damascus katika Syria ya leo, pia ulishambuliwa na katika siku kama ya leo ukakaliwa kwa mabavu. Hata hivyo kwa mujibu wa makubaliano ya hapo kabla kati ya London na Paris, Syria ukiwemo mji mkuu wake, Damascus, ilidhibitiwa na Ufaransa. 

Haram ya Bibi Zainab (as0 katika mji wa Damascus

Miaka 81 iliyopita katika siku kama ya leo, Ufaransa na Uingereza ziliitangazia vita Ujerumani na kwa utaratibu huo Vita Vikuu vya Pili vya Dunia vikaanza. Baada ya jeshi la Ujerumani kuishambulia Poland, serikali ya Uingereza iliitumia Ujerumani ujumbe ikiitaka iondoke haraka katika maeneo inayoyakalia kwa mabavu ya Poland. Hata hivyo Ujerumani ilipuuza takwa hilo la Uingereza. Baadaye Uingereza iliipatia Ujerumani makataa ya kuhitimisha operesheni zake za kijeshi. Hata hivyo Adolph Hitler kiongozi wa wakati huo wa Ujerumani ya Kinazi alikataa kutekeleza takwa hilo. Hatimaye katika siku kama ya leo, Uingereza na Ufaransa zikaitangazia vita Ujerumani. Sio Adolph Hitler pekee ambaye hakutaraji kama Ufaransa na Uingereza zingeingia vitani kwa ajili ya Poand bali hata Joseph Stalin kiongozi wa wakati huo wa Umoja wa Kisovieti pia hakutarajia hilo.

Vita vya Pili vya Dunia

Katika siku kama ya leo miaka 77 iliyopita, mkataba wa kusalimu amri Italia katika Vita Vikuu vya Pili vya Dunia ulitiwa saini baina ya wawakilishi wa Italia na nchi waitifaki. Kwa mujibu wa mkataba huo, Waziri Mkuu wa Italia alikubali bila masharti kusalimu amri nchi yake na kwa utaratibu huo, mmoja wa waitifaki muhimu wa Ujerumani ya Kinazi katika vita hivyo, akawa ameondoka katika medani ya vita.

Waziri Mkuu wa zamani wa Italia Benito Amilcare Andrea Mussolini

Miaka 49 iliyopita katika siku kama ya leo, nchi ya Qatar ilipata uhuru toka kwa mkoloni Mwingereza. Qatar iliwahi kudhibitiwa na Ufalme wa Othmania. Hata hivyo kufuatia kudhoofika utawala huo, Qatar ambayo kuanzia mwaka 1882 na kuendelea kivitendo ilikuwa ikiendeshwa na Uingereza, mwaka 1916 nchi hiyo ya Kiarabu ikawa imetambuliwa rasmi kuwa koloni la Muingereza. Hadi mwaka 1971 Qatar ilikuwa bado inakoloniwa na Uingereza ambapo mwaka huo huo, kwa ushirikiano wa viongozi wa eneo la pambizoni mwa kusini mwa Ghuba ya Uajemi, likaundwa Shirikisho la Umoja wa Falme za Kiarabu. Hata hivyo mnamo Septemba mwaka huo huo, yaani 1971, Qatar ilijiondoa katika Shirikisho la Umoja wa Falme za Kiarabu na kujitangazia uhuru.

Bendera ya Qatar

Siku kama ya leo miaka 42 iliyopita, yalifanyika maandamano ya kwanza ya mamilioni ya wananchi Waislamu wa Iran dhidi ya utawala wa Shah. Maandamano hayo yaliyofanyika kwa mnasaba wa Sikukuu ya Eidul Fitr yalifanyika baada ya Swala ya Idi na yalianzia katika vituo au nukta nne tafauti mjini Tehran na yakapata idadi kubwa zaidi ya watu kadiri muda ulivyosonga mbele. Waandamanaji hao ambao walikuwa wamebeba mabango pamoja na picha kubwa za Imam Khomeini mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran walisikika wakipiga nara za kutaka uhuru, kujitawala na kuundwa mfumo wa utawala wa serikali ya Jamhuri ya Kiislamu.

Maandamano ya kwanza ya mamilioni ya Wairani dhidi ya Shah

Na siku hii ya leo tarehe 13 Shahrivar katika kalenda ya mwaka wa Kiirani ni siku ya kumuenzi Abu Raihan Muhammad bin Ahmad Kharazmi Biruni msoni mtajika wa Iran na Ulimwengu wa Kiislamu.

Abu Raihani Biruni alizaliwa katika mji wa Birun karibu na Kharazm, moja kati ya miji ya zamani ya Iran Abu Raihan Biruni msomi, mnajimu na mwanahisabati mkubwa wa Kiirani. Abu Raihan Biruni alikuwa mtaalamu katika elimu za historia, jiografia unajimu na hisabati. Akiwa safarini nchini India, msomi huyo wa Kiirani alikutana na kufanya mazungumzo na maulamaa na watawala wa zama hizo na baada ya kujifunza lugha ya Sanskrit ambayo ni lugha ya kale ya Kihindi Abu Raihan alikusanya taarifa muhimu alizokuwa akizihitaji kwa ajili ya kuandika kitabu chake alichokiita 'Tahqiq Ma Lilhind'. Mbali na kitabu hicho msomi huyo alipata kuandika vitabu vingi katika nyanja tofauti zikiwemo za unajimu na mantiki.

Abu Raihan Biruni