Jumamosi, 23 Novemba, 2024
Leo ni Jumamosi 21 Mfunguo Nane Jamadul-Awwal 1446 Hijria sawa na 23 Novemba 2024 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1125 iliyopita sawa na tarehe 21 Mfunguo 8 mwaka 320 Hijria, alizaliwa Abu Jaafar Ahmad bin Ibrahim Qirawani, aliyekuwa mashuhuri kwa jina la Ibn Jazzar. Msomi huyo wa Morocco alikuwa tabibu, mwanafalsafa na mwanajiografia mashuhuri wa Kiislamu. Ibn Jazzar alikuwa tabibu mwenye moyo wa kujitolea na anayewatakia watu kheri na aliandika kitabu alichokipa jina la "Twibul Fuqaraa” au Tiba ya Watu Maskini." Mwanafalsafa huyo ameandika vitabu 20. Miongoni mwa vitabu vyake ni Risalatun Fii Ibdalil Adwiya na Zadul Musafir.
Miaka 118 iliyopita katika siku kama ya leo ambayo ni sawa na tarehe 3 Azar mwaka 1285 Hijria Shamsia, gazeti la 'Majlis' lililokuwa na kurasa 8 lilianza kuchapishwa nchini Iran. Mhariri Mkuu wa gazeti hilo alikuwa Adib al Mamalik Farahani ambaye alikuwa miongoni mwa waandishi mashuhuri wa zama hizo. Mbali na gazeti hilo kuandika habari za ndani na nje ya nchi, liliakisi pia mazungumzo yote ya Majlisi ya Ushauri yaani Bunge la Iran. ***
Katika siku kama ya leo miaka 87 iliyopita Jagadish Chandra Bose, msomi mtajika wa Bangladesh alifariki dunia. Jagadish alizaliwa Novemba 30 mwaka 1858 katika moja ya maeneo ambayo ni viungwa vya mji mkuu Dhaka. Miongoni mwa elimu alizokuwa amebobea Jagadish nii fizikia, sayansi ya mimea na akiolojia. Hata hivyo umashuhuri wa Jagadish Chandra Bose unatokana na kuvumbua kwake Radio na tanuri ya miale (Microwave).
Siku kama ya leo miaka 50 iliyopita Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipasisha hati ya kuundwa nchi huru ya Palestina. Suala la Palestina lilikuwa miongoni mwa mambo ya mwanzo kabisa kujadiliwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. Hata hivyo maazimio mengi ya Umoja wa Mataifa yamekuwa yakiathiriwa na nchi kubwa zinazowaunga mkono Wazayuni wa Israel na utawala huo ulitumia moja ya maazimio hayo hapo tarehe 14 Mei 1948 kuanzisha dola haramu la Israel katika ardhi ya Palestina.
Siku kama ya leo miaka 48 iliyopita, alifariki dunia André Malraux mwandishi na msanii maarufu wa Ufaransa. Malraux alizaliwa mwaka 1901 mjini Paris na katika ujana wake alikwenda nchini China na India zilizokuwa chini ya ukoloni wa Ufaransa na kujishughulisha na mapambano dhidi ya ukoloni wa nchi yake huko Mashariki mwa Asia. Wakati akirejea katika safari yake hiyo, aliandika kitabu maarufu kwa jina la ‘Hatma ya Mwanadamu.’ Katika vita vya ndani nchini Uhispania, Malraux alishirikiana na wapigania uhuru wa nchi hiyo. André alikuwa akipinga vita na umwagaji damu na alitetea pia uhuru wa mwanadamu. ‘Vilio vya Ukimya’, ‘Ushawishi wa Magharibi’, ‘Tumaini la Mwanadamu’ na ‘Washindi’ ni miongoni mwa vitabu vilivyoandikwa na msanii huyo wa Kifaransa.
Katika siku kama ya leo miaka 24 ilioyopita alifariki dunia mwanazuoni mkubwa wa Kiislamu Ayatullah Sayyid Mahdi Rouhani. Alizaliwa mwaka 1303 Hijria Shamsia katika familia ya kidini katika mji mtakatifu wa Qum nchini Iran na baada ya masomo ya mwanzo alielekea Karbala nchini Iraq kwa ajili ya elimu ya juu. Alifanya utafiti mkubwa kuhusu dini na madhehebu mbalimbali na kuwa gwiji katika taaluma hiyo. Wakati wa harakati za Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran, Ayatullah Rouhani alikuwa bega kwa bega na wananchi wa Iran katika mapambano yao dhidi ya utawala wa kifalme wa Shah wakiongozwa na hayati Imam Khomeini. Msomi huyo mkubwa wa Kiislamu ameandika vitabu vingi vikiwemo vile vya "Firqatus Salafiyyah", "Buhuth Ma'a Ahlisunnah Wassalafiyyah" na "Firaq wa Madhahibu Islamiyyah".