Alkhamisi tarehe 10 Septemba 2020
Leo ni Alkhamisi tarehe 21 Muharram 1442 Hijria sawa na Septemba 10 mwaka 2020.
Siku kama ya leo miaka 716 iliyopita inayosadifiana na tarehe 21 Muharram 726 Hijria, alifariki dunia faqihi na msomi mashuhuri wa ulimwengu wa Kiislamu, Hassan bin Yussuf bin Mutahhari Hilli, maarufu kwa jina la Allamah Hilli. Allamah Hilli alipata elimu kwa wanazuoni wakubwa kama Khaja Nasiruddin Tusi na anatajwa kama miongoni mwa wasomi wa kipekee wa zama zake. Aliandika zaidi ya vitabu mia moja katika taaluma mbalimbali za Kiislamu. Miongoni mwa vitabu mashuhuri vya mwanazuoni huyo ni Tadhkiratul Fuqahaa' ambacho kinaelezea mitazamo mbalimbali za madhehebu ya Kiislamu, tafsiri ya Qurani Tukufu ya 'Nahjul Imaan' na 'Muntahaal Matwalib'.
Miaka 106 iliyopita yaani tarehe 10 Septemba mwaka 1914 kulitokea vita baina ya majeshi ya Ujerumani na Russia kando kando ya ziwa la Mazury. Vita hivyo vilianza kufuatia kuzuka Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia na kujiunga Russia na kambi ya nchi waitifaki. Katika vita hivyo vya Mazury, Wajerumani wakiongozwa na kamanda Paul Von Hindenburg walifanikiwa kupata ushindi na kuwauwa takribani wanajeshi 20,000 wa Russia na kuwateka nyara wengine 45,000. Hatimaye mwaka 1917 baada ya kutokea mapinduzi nchini Russia, nchi hiyo ilijiondoa katika Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia.
Siku kama ya leo miaka 66 iliyopita, mtetemeko mkubwa wa ardhi ulitokea katika eneo la Orleansville kusini magharibi mwa Algeria. Janga hilo la mtetemeko wa ardhi lilisababisha mji mmoja uliokuwa na wakazi 30,000 kuangamia na watu 10,000 kupoteza maisha yao. Fauka ya hayo, makumi ya maelfu ya wananchi wa kusini magharibi mwa Algeria walibaki bila ya makazi. Mtetemeko huo vilevile ulitoa pigo kubwa kwa miundo mbinu ya uchumi wa nchi hiyo.

Siku kama ya leo miaka 39 iliyopita inayosadifiana na tarehe 20 Shahrivar 1360 Hijria Shamsia, aliuawa Shahidi Ayatullah Sayyid Asadullah Madani, Imamu wa Swala ya Ijumaa katika mji wa Tabriz, kaskazini magharibi mwa Iran wakati wa wa Swala ya Ijumaa. Shambulio hilo la kigaidi lilifanywa na kikundi cha kigaidi cha Munafiqin (MKO). Ayatullah Madani alipatia elimu kutoka kwa maulamaa kadhaa katika mji wa Qum na kisha akaelekea Najaf, Iraq ambako aliweza kujipatia daraja ya juu ya Ijitihad. Msomi huyo alikamatwa na kuteswa mara kadhaa na vikosi vya utawala wa Mfalme wa Iran, kutokana na misimamo yake ya kuupinga utawala huo. Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Imam Khomeini alimteua Ayatullah Madani kuwa Imam wa Swala ya Ijumaa katika mji wa Tabriz.
Na tarehe 10 Septemba mwaka 1990 Samuel Kanyon Doe aliyekuwa rais wa jamhuri ya Liberia aliuawa na kundi la waasi. Doe alishika madaraka ya nchi mwaka 1980 akiwa sajenti mwenye umri wa miaka 29 tu baada ya kufanya mapinduzi ya umwagaji damu akitumia umaskini, kupanda kwa gharama za maisha na hali mbaya ya wananchi. Hata hivyo utawala wa kidikteta wa Samuel Doe haukufanikiwa kupunguza machungu na mashaka ya Waliberia bali kinyume chake alipanua zaidi hitilafu za kikabila na kuzidisha matatizo ya kiuchumi na kijamii. Vilevile alitayarisha uwanja wa kuporwa zaidi utajiri wa madili ya almasi ya nchi hiyo kupitia njia ya kupanua zaidi uhusiano wa Liberia na Marekani na utawala haramu wa Israel. Mauaji ya Samuel Doe yalifuatiwa na vita vya ndani nchini Liberia ambavyo viliendelea kwa kipindi cha miaka 15 na kusababisha vifo vya watu karibu laki mbili na nusu.