Sep 13, 2020 22:04 UTC
  • Jumatatu tarehe 14 Septemba 2020

Leo ni Jumatatu tarehe 25 Mfunguo Nne, Muharram 1442 Hijria sawa na Septemba 14 mwaka 2020 Milaadia.

Siku kama ya leo miaka 1347 iliyopita inayosadifiana na tarehe 25 Muharram mwaka 95 Hijria, kwa mujibu wa baadhi ya nukuu za historia, aliuawa shahidi Ali bin Hussein mwenye lakabu ya Sajjad na Zainul Abidiin AS, mtoto wa Imam Hussein bin Ali AS, na mjukuu wa Mtume Mtukufu Muhammad SAW. Imam Zainul Abidiin AS alizaliwa mjini Madina mwaka 38 Hijria. Mtukufu huyo alichukua jukumu la kuwafikishia Waislamu ujumbe mzito wa mapambano ya baba yake baada ya kuuawa shahidi huko Karbala. Imam Sajjad AS ameuachia Umma wa Kiislamu kitabu cha Al Swahifatu Sajjadiyya' chenye thamani kubwa ambacho kimejaa dua zenye mafunzo na maarifa ya Kiislamu.

Tarehe 14 Septemba miaka 208 iliyopita, moto mkubwa na wa kihistoria duniani ambao uliwashwa kwa makusudi ulitokea katika mji mkuu wa Russia, Moscow. Tukio hilo lilitokea siku moja tu baada ya mji huo kuvamiwa na kukaliwa kwa mabavu na majeshi ya Napoleone Bonaparte. Mtawala wa mji wa Moscow alitoa amri mji huo uchomwe moto kwa lengo la kuyafanya majeshi ya Ufaransa yashindwe kupata chakula na suhula nyingine za kuyawezeaha kubakia mjini humo. Moto huo mkubwa uliteketeza na kuharibu kabisa robo tatu ya mji mzima wa Moscow.

Moto mkubwa na wa kihistoria wa Moscow

Tarehe 25 Muharram miaka 183 iliyopita, lilichapishwa gazeti la kwanza la Iran lililojulikana kwa jina la 'Kaaghaze Akhbar'. Gazeti hilo lilichapishwa na Mirza Swaleh Shirazi mjini Tehran, likiwa na kurasa mbili kubwa. Gazeti hilo lilikuwa likichapishwa mara moja kwa mwezi na lilizungumzia habari za Tehran na miji mingine ya Iran, nchi za Kiarabu na Uturuki.

Kaaghaze Akhbar

Miaka 59 iliyopita katika siku kama ya leo, hati ya Jumuiya ya Nchi Zinazozalisha Mafuta kwa Wingi Duniani (OPEC) ilitiwa saini na nchi za Iran, Saudi Arabia, Iraq, Kuwait na Venezuela. Jumuiya hiyo ilianzishwa kwa lengo la kukabiliana na makampuni makubwa ya mafuta ya Magharibi ambayo yalikuwa yakisimamia uvumbuzi, uchimbaji na uuzaji wa bidhaa hiyo kimataifa na kuainisha bei ya bidhaa hiyo muhimu kwa maslahi yao binafsi na kwa madhara ya nchi zalishaji. Licha ya kwamba awali jumuiya hiyo haikuwa na nguvu wala ushawishi wowote, lakini ilikuja kupata nguvu zaidi baada ya nchi kadhaa zikiwemo, Algeria, Libya, Nigeria, Qatar, Imarat, Gabon, Indonesia na Ecuador ambazo ni wazalisha wa mafuta kujiunga nayo. 

 (OPEC)

Na siku kama hii ya leo miaka 17 iliyopita sawa na tarehe 24 mwezi Shahrivar mwaka 1378 Hijria shamsiya, alifariki dunia kwa maradhi ya moyo Dakta Abdulhussein Zarinkub mwanahistoria na mtafiti mashuhuri wa Kiirani. Dakta Abdulhussein alizaliwa mwaka 1301 Hijria Shamsiya katika mji wa Burujerd magharibi mwa Iran. Mwaka 1327 Hijria Shamsiya Dakta Zarinkub alitunukiwa shahada ya digrii katika taaluma ya historia na baadae akaendelea na masomo yake katika taaluma hiyo na kutunikiwa shahada ya udaktari. Mbali na historia msomi huyo wa Kiirani alipenda sana masomo ya fasihi ya lugha ya Kifarsi na irfani ya Kiislamu. Aidha aliandika vitabu na makala nyingi na moja kati ya vitabu vyake ni kile alichokiita "Alfajiri ya Uislamu."

Dakta Abdulhussein Zarinkub