Sep 14, 2020 22:02 UTC
  • Jumanne, tarehe 15 Septemba, 2020

Leo ni Jumanne tarehe 26 Mfunguo Nne Muharram 1442 Hijria sawa na Septemba 15 mwaka 2020.

Siku kama ya leo miaka 1378 iliyopita mji mtakatifu wa Makka ulishambuliwa ka mawe baada ya kuzingirwa na jeshi la mtawala mal'uni wa kizazi cha Banii Umayyah, Yazid bin Muawiya. Baada ya kumuua shahidi Imam Hussein na wafuasi wake katika medani ya Karbala na Watu wa Nyumba ya Mtume wakachukuliwa mateka, Yazid alidharaulika sana na kukosa heshima katika Umma wa Kiislamu. Waislamu katika maeneo mbalimbali walianzisha uasi dhidi ya utawala wake. Harakati hizo za uasi zilifika hadi Hijaz hapo mwaka 63 Hijria ambapo watu wa Makka walimfukuza gavana wa Yazid na kuchukua madaraka ya mji huo. Mtawala huyo alituma jeshi ambalo liliuzingira mji huo mtukufu na kushambulia Msikiti wa Makka na al Kaaba kwa mawe.

Makka

Miaka 419 iliyopita aliaga dunia Sheikh Abdullah Tostari faqihi na msomi wa Kiislamu wa Kiirani. Sheikh Tostari alifikia daraja ya ijtihad baada ya kuhitimu masomo ya kidini chini ya maustadhi wakubwa wa zama hizo. Sheikh Abdullah Tostari baadaye alielekea katika hauza ya kielimu ya mji wa Isfahan nchini Iran na kuanza kufundisha masomo ya dini. Darsa ya mujtahidi huyo ilikuwa ikihudhuriwa na wanafunzi wengi ambao walinufaika na bahari kubwa ya elimu yake. Allamah Majlisi na Mirza Muhammad Naini ni miongoni mwa wanafunzi wa Sheikh Abdullah Tostari.

Miaka 199 iliyopita yaani tarehe 15 Septemba 1821, nchi za Nicaragua, Honduras, el-Salvador, Guatemala na Costa Rica zilijitangazia uhuru kutoka kwa Uhispania. Baada ya Napoleone Bonaparte mtawala wa Kifaransa kuikalia kwa mabavu Uhispania na kudhoofika serikali ya kijeshi ya Madrid, nchi kadhaa za Latin America zikiwemo Nicaragua, Honduras, el-Salvador, Guatemala na Costa Rica zilijitangazia uhuru. Baada ya nchi hizo tano kujitangazia uhuru ziliunda Muungano wa Amerika ya Kati. Baada ya muungano huo kuvunjika mwaka 1838, nchi wanachama kila moja ilianza kujitawala na kujiendeshea mambo yake yenyewe.

Siku kama ya leo miaka 62 iliyopita, kwa mara ya kwanza katika elimu ya tiba, viligunduliwa virusi vinavyosababisha maradhi hatari ya trakoma yaani mtoto wa jicho. Pamoja na kugunduliwa virusi hivyo yapata miaka kadhaa iliyopita, hadi sasa maelfu ya watu hukumbwa na hali ya upofu duniani, kutokana na maradhi hayo. Virusi hivyo viligunduliwa na madaktari wawili wa Kiingereza.

Siku kama ya leo miaka 42 iliyopita, zilzala iliyokuwa na ukubwa wa 7.7 kwa kipimo cha Rishta ililitikisa eneo la kaskazini mashariki mwa Iran na kuuharibu mji wa Tabas na vijiji vya kando kando ya mji huo. Watu zaidi ya elfu 25 waliuawa na makumi ya maelfu ya wengine kujeruhiwa katika mtetemeko huo mkubwa wa ardhi. Zilzala ya Tabas ilitokea sambamba na kupamba moto mapambano ya wananchi wa Iran dhidi ya utawala wa Shah.

Mtetemeko wa ardhi wa Tabas