Jumatano tarehe 16 Septemba 2020
Leo ni Jumatano tarehe 27 Muharram 1442 Hijria sawa na tarehe 16 Septemba 2020.
Miaka 284 iliyopita katika siku kama ya leo, alifariki dunia Daniel Gabriel Fahrenheit mwanahesabati na mwanafizikia wa Kijerumani aliyevumbua kipimajoto yaani thermometer, akiwa na umri wa miaka 50. Fahrenheit alikuwa na fikra ya kubuni kifaa ambacho kingekuwa na uwezo wa kupima kiwango cha joto na mwaka 1724 mwanafizikia huyo Mjerumani akafanikiwa kutengeneza kipimajoto hicho. Kifaa hicho ambacho kimepewa jina la msomi huyo mwenyewe yaani Fahreinheit, bado kinatumika hadi leo.
Miaka 89 iliyopita mwafaka na siku hii ya leo, aliuawa Omar al Mukhtar kiongozi wa taifa la Libya katika mapambano ya ukombozi dhidi ya wakoloni wa Italia. Omar Mukhtar aliyekuwa kiongozi wa kidini alizaliwa mwaka 1859. Mwaka 1895 alielekea Sudan na kushiriki katika harakati za kupambana na ukoloni wa Uingereza. Baada ya kushindwa kwa harakati hizo, Omar Mukhtar alirejea nchini Libya. Mwaka 1911 Wataliano waliivaia Libya kwa lengo la kuitawala nchi hiyo. Kiongozi huyo wa kidini aliwahimiza wapiganaji wa makabila ya Libya kusimama kidete na kupambana dhidi ya wavamizi wa Kitaliano na kuwasababishia hasara kubwa. Hata hivyo kwa kutumia askari wengi zaidi na silaha za kisasa wavamizi hao walimzingira Omar Mukhtar na wenzake na kumkamata na kisha wakamnyonga katika siku kama ya leo.
Siku kama ya leo miaka 88 iliyopita Sir Ronald Ross daktari mashuhuri wa Kiingereza na mvumbuzi wa chanzo cha ugonjwa wa Malaria alifariki dunia. Alizaliwa Mei 13 mwaka 1857 katika mji wa Almora huko India. Alielekea Uingereza akiwa mdogo na kusoka akiwa huko ambapo alifanikiwa kupata shahada ya uzamivu PhD katika taaluma ya tiba. Ufumbuzi wake wa chanzo cha Malaria ulikuwa na nafasi muhimu sana kwani uliandaa uwanja wa namna ya kukabiliana na maradhi hayo. Mwaka 1902 Dakta Ronald Ross alitunukiwa tuzo ya Nobel. Hatimaye Daktari Ronald Ross aliaga dunia katika siku kama ya leo baada ya kuishi kwa muda wa miaka 75.
Tarehe 16 Septemba miaka 81 iliyopita Warsaw mji mkuu wa Poland ulizingirwa na Wajerumani, katika mwezi wa kwanza wa Vita vya Pili vya Dunia. Mashambulio ya wanajeshi wa Kinazi wa Ujerumani huko Poland yalianza siku 15 kabla ya kuanza vita hivyo.
Tarehe 26 Shahrivar miaka 40 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria Shamsia, utawala wa zamani wa Iraq ulifuta kwa upande mmoja makubaliano ya mipaka ya mwaka 1975 yaliyojulikana kwa jina la Mkataba wa Algeria kati yake na Iran. Siku hiyo, Saddam Hussein kiongozi wa zamani wa Iraq aliuchana mkataba huo wa Algeria mbele ya kamera za televisheni akiungwa mkono na madola ya kibeberu. Siku kadhaa baadaye, Saddam Hussein alianzisha uvamizi wa miaka minane dhidi ya ardhi ya Iran.

Tarehe 16 Septemba miaka 38 iliyopita, askari wa utawala haramu wa Israel walifanya mauaji makubwa ya Wapalestina zaidi ya 3300 katika kambi za wakimbizi wa Kipalestina huko Sabra na Shatila nchini Lebanon. Ilikuwa Juni mwaka 1982 wakati maelfu ya askari wa utawala haramu wa Israel walipoishambulia Lebanon na baada ya kuwalazimisha wapiganaji wa Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) kuondoka Beirut, waliukalia kwa mabavu mji huo. Menachem Begin Waziri Mkuu wa wakati huo wa Israel na Ariel Sharon aliyekuwa Waziri wa Vita wa utawala huo, tarehe kama ya leo waliliamuru jeshi la Israel kuzizingira kambi za Sabra na Shatila na kisha Mafalanja wa Lebanon wakaanza kufanya mauaji ya umati dhidi ya wakimbizi wa Kipalestina waliokuwa katika kambi hizo. Wapalestina zaidi ya 3,300 waliuawa shahidi katika mashambulio hayo.